NA MWANDISHI DIRAMAKINI
SIMBA SC wameuanza mwaka vyema wa 2022 baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Azam FC.
NI katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (Ligi Kuu ya NBC) uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Dakika 45 zilimalizika kwa milango kufunga huku wakiwa si Simba wala Azam waliopata bao.
Pengine matumaini yalikuwepo kipindi cha kwanza kupitia Rally Bwalya ingawa alikosa penalti iliyopanguliwa na kipa Mzanzibari, Ahmed Ally Suleiman (Salula) dakika ya 14.
Ni baada ya winga Msenegal, Pape Ousmane Sakho kuchezewa rafu na kiungo Frank Raymond Domayo.
Sadio Kanoute ndiye aliyefungua mlango kwa bao la kwanza la Simba dakika ya 68, kabla y Sakho kufunga la pili dakika ya 72 na Azam FC ikapata bao lake pekee kupitia kwa mshambuliaji Rodgers Kola dakika ya 80.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inafikisha alama 24 katika mchezo wa 10, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa alama tano na watani wao, Yanga ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi, wakati Azam FC inabaki na alama zake 15 za mechi 11 sasa katika nafasi ya saba.
Desemba 31, 2021 Yanga SC walifunga mwaka kwa ushindi wa kishindo wa mabao 4-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (Ligi Kuu ya NBC) katika dimba hilo hilo.
Fiston Kalala Mayele dakika ya 42, Jesus Ducapel Moloko dakika ya 57, Justin Billary aliyejifunga dakika ya 71 na kiungo Mganda dakika ya 81 ndiyo walipeleka kilio kwa Dodoma Jiji FC.