Loliondo wapingana na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha

NA PAMELA MOLLEL

KAULI ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella kuhusiana na eneo lenye mgogoro wa muda mrefu la hekari 1500, lililolopo Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha imezua taharuki kubwa kwa wananchi wa eneo hilo na kusababisha kukutana na kutoa tamko la kupinga kauli hizo.
Wananchi jamii ya wafugaji wakiwa wamebeba mabango kupinga eneo lao la hekari 1500 kumegwa.

Kauli hiyo ya Mongela kuhusu eneo hilo la hekari 1500 aliitoa Januari 11, 2022 alipokuwa katika ziara ya siku tano ya kikazi katika Wilaya ya Ngorongoro ambapo alisisitiza kuwa, atasimamia maslahi mapana ya Taifa na ya Mkoa wa Arusha.

Wakizungumza na waandishi wa habari huku wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali ya kupinga kauli hizo, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kijiji cha Olorieni, Tarafa ya Loliondo wamesema, kauli hizo zimewapa mashaka na kushindwa kuelewa hatma yao na hivyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ngorongoro, wameomba kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye wana imani naye.

Akitoa tamko kwa niaba ya wananchi, mbele ya viongozi wa mila (Malaigwanani), madiwani, viongozi wa CCM wilaya ya Ngorongoro, Diwani wa Kata ya Alash, Mathew Siloma amesema Mkuu wa Mkoa kwa kujua au kutojua ameuanzisha upya mgogoro uliopo wakati ilishapita mamlaka yake ya kiutawala.
Wananchi jamii ya wafugaji wakiwa wamebeba mabango kupinga eneo lao la hekari 1500 kumegwa.

“Mwaka 2016, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa aliunda tume ya kukusanya na kuwasilisha kwake mapendekezo ya namna ya kumaliza mgogoro huo,”amesema.

Siloma amesema, baadae tume iliwasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu kwa maana ya Aprili 2017.Hata hivyo waziri Mkuu alisema Serikali itafanyia kazi mapendekezo ya tume ikiwemo suala la usimamizi na utumiaji wa pamoja wa eneo la mgogoro."Mpaka sasa Serikali haijaweza kurasimisha mapendekezo au kuweka hadharani,"amesema Diwani huyo.
Diwani wa kata ya Alash, Mathew Siloma akitoa tamko kwa niaba ya ya wananchi kupinga eneo lao la ardhi kumegwa.

Amesema, kitendo cha Mkuu wa Mkoa kuanzisha upya mgogoro kwa kutembelea eneo hilo na kusema linatengwa, inakiuka misingi ya utawala bora, kuingilia mahakama na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi wa Tarafa za Sale na Loliondo.

Siloma amesema, madiwani kutoka kata zinazoathirika, viongozi wa vijiji, viongozi wa mila na wanawake waliiomba Serikali kuchua hatua.

"Kwanza, kutambua hekari 1500 ni ardhi ya vijiji na sio eneo la hifadhi, kuachana kabisa na azma ya kutenga eneo la vijiji kwa ajili ya uwindaji, kwani wananchi wa Loliondo hawana ardhi ya ziada ya kuhamia, kuweka wazi taarifa za kamati ya Gambo (Mrisho Gambo, RC mstaafu Arusha) iliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu mwezi Aprili 2017.

"Pia kuheshimu kesi iliyopo mahakamani na kuacha kuwasumbua wananchi wakati kesi ikindelea kadri ya zuio lililotolewa Agosti 2018 na kuomba kumuona Rais Samia ili kumueleza uhalisia wa mgogoro huo wa kutungwa na wahifadhi kwa kuwalinda wawekezaji bila kutambua maslahi ya maisha ya wananchi,"amesema.
Diwani wa Viti Maalum kutoka Tarafa ya Sale, Kijoolu Kakeya akiongea kwa niaba ya wanawake ambapo alimuomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati sakata hilo.

Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Sale, Kijoolu Kakeya, kwa niaba ya wanawake amesema kuwa, wanawake wa wilaya hiyo wanapata shida hivyo kuomba wamuone Rais Samia awawapiganie wanawake wenzake kwani wao ndio wanaoteseka kutokana na kubeba mzigo mkubwa katika familia.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Ole Senge amesema kama chama wamepokea malalamiko hayo na watayafikisha kunakohusika yashughulikiwe kwa haki na kupata muafaka.

Kiongozi wa mila (Laigwanani), Rafaeli Long’oi alimuomba Rais Samia Suluhu kuangalia Wanangorongoro kwa jicho la pili kwani tangu Mwaka 1959 waliondolewa Serengeti na kupelekwa Loliondo na kujengewa miundombinu kama shule, majosho na mengineyo, lakini leo wanaambiwa waondoke.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alipokuwa ziarani wilayani Ngorongoro alisema Serikali imesikia mengi kuhusiana na eneo lenye mgogoro, lakini Serikali haitaonea mtu yoyote, awe mwekezaji au mwananchi ila kama kuna maslahi mapana ya Taifa yatazingatiwa hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news