NA JOHN MAPEPELE
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan ameukaribisha mwaka 2022 kwa kupongeza mafanikio makubwa ya Michezo na Sanaa yaliyofikiwa na Tanzania kwenye medani za kimataifa.
Mhe. Samia ameyasema hayo kwenye hotuba yake ya kufunga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka 2022 ambapo amesema, kwa ujumla nchi yetu imepata mafanikio makubwa kwenye sekta za michezo na sanaa.
"Kwa upande wa Sanaa, michezo na utamaduni tunajivunia vijana wetu wa Tembo Warriors kwa kufuzu kushiriki katika kombe la dunia la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu,"ameeleza Rais Samia.
Timu ya Tembo Warriors inashiriki kombe la Dunia la watu wenye ulemavu nchini Uturuki, Oktoba mwaka huu.Pia ameipongeza timu ya mpira wa miguu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20 ya Tanzanite kwa kubakiza hatua mmoja kufuzu kushiriki kwenye kombe la dunia nchini Costa Rica.
Tanzanite inatarajia hivi karibuni kuvaana na Ethiopia kwenye mchezo wa kufuzu mashindano hayo baada ya kuishinda kishujaa timu ya Burundi 1-1 ikicheza pungufu uwanjani ikiwa na wachezaji nane tu nchini kwao.
Pia amepongeza washindi wa Afrika wa mashindano ya urembo na utanashati ya viziwi watakaoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Dunia mwaka huu nchini Brazil.
"Haya ni mafanikio makubwa katika medani za michezo. Ni fahari kwetu pia kuona vijana wetu wa tasnia ya muziki wameweza kushiriki na kupata tuzo Mali Bali katika ngazi za kimataifa". Amezisitiza Mhe. Rais
Naye, Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini. Mhe, Innocent Lugha Bashungwa amesema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha Tanzania inafanya vizuri katika mashindano yote ya kimatafa yanayofanyika kuanzia mwaka huu.
"Kipekee namshukuru sana, Mhe. Rais kwa maelekezo na kutoa kipaombele kwenye sekta za michezo hali ambayo imetuwezesha kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, tunamwahidi kuendelea kusimamia vizuri zaidi ili kupeperusha bendera ya nchi yetu kimataifa katika michezo". Amesisitiza Mhe. Bashungwa
Aidha, amefafanua kuwa tayari Wizara imejiweka mikakati kabambe ya kushinda kwenye michuano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na michezo ya jumuiya ya madola ya mwaka huu nchini Uingereza na Olympic.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Hassan Abbasi ameongeza kuyataja mafanikio mengine makubwa kwenye michezo katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe, Rais. Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kurejesha kwa Mashindano ya Michezo kwa Shule za Msingi ( UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) na mashindano ya Taifa CUP yaliyoshirikisha zaidi ya mchezo mmoja tofauti na awali.
Pia amesema kwa mara kwanza nchini kumeanzishwa tamasha maalum la wanawake kwa ajili ya Michezo ya wanawake (Tanzania Women Festival) lililotoa mahasa kubwa na kuibua vipaji vya wachezaji wanawake hapa nchini.
Ameongeza kuwa Serikali imeratibu Tamasha la utoaji wa Tuzo mbalimbali kwa wasanii ili kuthamini na kutambua mchango wao pia kuwapa ali wasanii ya kufanya vizuri katika viwango vya kimataifa na hivyo kujipatia kipato.
Amesema sambamba na hayo Wizara iliandaa tamasha la kimataifa la Utamaduni na Sanaa la Bagamoyo ambalo lilitumika katika kutangaza utalii wa kiutamaduni kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia ambalo lilipata mafanikio makubwa.