NA MWANDISHI DIRAMAKINI
CHAMA Cha Alliance For Democratic Change( ADC) kimesema hadi kufikia sasa ni mwanachama mmoja tu wa chama hicho Maimuna Said ndiye aliyefanikiwa kuchukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa kwa chama chake kwa ajili ya kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zoezi hilo la uchukuaji na urejeshwaji wa fomu lilianza Januari 16 na limeitimishwa leo Januari 18,2022.
Mwanachama wa Chama cha ADC,Maimuana Saidi akirejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho,Doni Mnyamani jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza baada ya kukabidhi fomu hiyo, Maimuna Said kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Bara wa ADC, Doni Mnyamani amesema, tayari amejaza fomu kwa ufasaha na anaomba ridhaa ya chama kiweze kumteua ili aweze kuingia katika kinyanganyiro hicho kwa kuwa, uwezo anao.
Maimuna amesema, endapo atateuliwa na chama chake na kushinda nafasi ya Usipika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahakikisha anaunganisha mihimili ya serikali ambayo ni Mahakama,Bunge na Serikali ili ifanye kazi kwa ushirikiano.
"Nina haki ya kikatiba ya kugombea nafasi hii ya Uspika,pia nitahakikisha Bunge linakuwa na ushirikiano na mihimili mingine ili ifanye kazi kwa pamoja kwa kufuata haki sawa katika kusimamia ,kukosoa na kushauri serikali,"amesema Maimuna.
Aidha, ameongeza kuwa, ana uwezo wa kuongoza kwani mwaka 2020 aliweza kugombea nafasi ya ubunge Kilindi mkoani Tanga.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Katibu Mkuu ADC, Doni Mnyamani amesema baada ya kupokea fomu za wagombea wote Januari 20,Mwaka huu chama hicho kitapitisha jina la mgombea ambaye ataweza kuwania nafasi ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Leo Januari 18,2022 Maimuna Saidi amerudisha fomu ambayo alichukua Jumapili ya tarehe 16 kwa ajili ya kuomba kugombea nafasi ya Usipika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya aliyekua Spika wa Bunge hilo Job Ndugai kujiuzulu, mpaka sasa tuna mtu mmoja tu aliyejitokeza kuchukua fomu," amesema Mnyamani.