NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman ameishauri Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kutumia fursa za uzuri wa asili wa Visiwa vya Unguja na Pemba, ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Nchi na kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Januari 8,2022 wakati akilifungua rasmi Tamasha la Nane la Biashara la Zanzibar la Mwaka 2022, katika Viwanja vya Maisara, jijini hapa ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Miaka 58 ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema, ni vyema kwa Wizara husika kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo na wa maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla, ili kubadilishana mawazo na kisha kufikia ujenzi wa mahusiano mema yatakayoleta tija kwa pande zote, serikali pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Othman ameeleza kwamba ni vyema kuwapatia fursa wadau wa maendeleo wakiwemo wafanyabiashara, taasisi za kifedha, wawekezaji katika viwanda, kilimo na Utalii, kujitambulisha kwa wateja na wadau, kwa azma pia ya kubaini fursa mpya ziliopo na huduma zilizoboreshwa ili kuharakisha kasi ya kukuza uchumi na maendeleo ya Zanzibar na kuchangia pato la Taifa kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Othman amebainisha kuwa hatua hiyo italenga pia katika kuwawezesha wananchi kutafakari namna bora ya kutumia fursa mbalimbali za kibiashara zilizopo Zanzibar, na hatimaye kutoa fursa ya kubainisha changamoto zinazozuia maendeleo ya sekta ya biashara hapa visiwani.
“Kwa kupitia Tamasha hili, Zanzibar inapata fursa ya kujitathmini kupitia kona nyingine ya mtazamo wa kibiashara ‘non-traditional business practice’, na fursa mbalimbali zinabainishwa kwa wadau na washiriki kuonesha bidhaa mpya walizonazo na zile za zamani ambazo zimeboreshwa ili kukidhi mazingira ya sasa ya maendeleo ya Zanzibar,” amesema Mheshimiwa Othman.
Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mheshimiwa Omar Said Shaaban, amesema kuna haja ya kuangalia njia zote muhimu ambazo zinaweza kutumika katika kulitangaza Tamasha hilo na kuvutia washiriki wengi zaidi wa kitaifa na kimataifa.
Amesema kwamba wakati umefika kwa Serikali kupitia Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kukamilisha miundombinu inayohitajika katika eneo la Maonesho la Nyamanzi ‘exhibition centre’ na kupelekea maonesho hayo kuwa makubwa zaidi katika Kanda ya Afrika Mashariki, na kwa kuzingatia kuwa historia ya Zanzibar kama ‘kitovu cha biashara’, bila ya shaka hilo linawezekana.
Mwenyeji wa tamasha hilo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Bw. Idrisa Kitwana Mustafa amesema siri kubwa ya mafanikio ni pamoja na wafanyabiashara kuitumia vyema fursa ya kutangaza bidhaa zao, na kwamba hapana budi kwa Serikali kuweka miundombinu bora ili kuliendeleza na kufikia haja ya kuwa la kimataifa.
Wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali za ndani na nje ya Bara la Afrika, zikiwemo Ghana na Misri, Wawekezaji, Watendaji, Wasimamizi wa Mabenki na Taasisi za Fedha, Wananchi, na Viongozi mbali mbali, akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Saada Mkuya Salum, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Leyla Mohamad Mussa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dokta Islam Seif Salim, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, Ndugu Rashid Simai Msaraka, na Wakuu wa Vikosi vya Idara Maalum za SMZ, wamehudhuria katika hafla hiyo.
Lengo la Tamasha hilo, lililoasisiwa tangu mwaka 2014, na kwa mwaka huu likibeba kauli mbiu ya TEKNOLOJIA NA UBUNIFU KWA UKUZAJI BIASHARA na ambalo linatarajiwa kuendelea hadi tarehe 15 Januari 2022, ni kutoa fursa na kuchangamsha ari ya wadau wa biashara, maendeleo na viwanda hapa Zanzibar, katika kuitikia kwa vitendo Sera ya Kukuza Uchumi wa Nchi, na kunyanyua kipato cha wananchi.