Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar atoa maelekezo muhimu kwa wasomi nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema jukumu kubwa la vyuo vikuu ni kusaidia kutatua matatizo ya jamii, kwa kufanya tafiti ili kutoa mwangaza na muelekeo wa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika hafla ya Mahafali ya 21 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-sumait, yaliyofanyika Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar. 

Amesema, suala la vyuo vikuu kufanya tafiti linahitaji msisitizo wa hali ya juu kwani ni eneo muhimu la kujivunia, na hazina katika kufanikisha maendeleo, kama ambavyo mataifa yaliyotutangulia kimaendeleo duniani yameshuhudia.

Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa vyuo vikuu vya Zanzibar kufuatilia kwa karibu maeneo mengine ya kupewa kipaumbele cha utafiti kama yalivyoainishwa katika Agenda ya Utafiti ya Zanzibar (Zanzibar Research Agenda).
“Hapa tunajifunza dhima na jukumu la kila chuo kikuu kuzingatia umuhimu wa kufanya tafiti zenye tija, ili kuyakabili matatizo sugu yanayokabili jamii na hasa nchi zetu ndani ya Bara la Afrika,”amesema Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman ameshauri kwamba kutokana na ongezeko la vyuo vikuu nchini hali ambayo inapelekea kuongeza ushindani wa udahili na kuwania wanafunzi, ni vyema kujipanga kwa kuweka mikakati imara na juhudi endelevu ili kukitangaza chuo, ikiwemo utoaji wa ‘courses’ zinazovutia, zenye soko duniani sambamba na wahitimu bora wanaoajirika.
Aidha, Mheshimiwa Othman amelipongeza Shirika la ‘Direct Aid’ ambalo ni wamiliki wa Chuo Kikuu cha SUMAIT, kwa juhudi zake za kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika visiwa vya Unguja na Pemba, na nje ya Zanzibar.

Pamoja na kuwapongeza na kuwatakia mafanikio mema maishani, wahitimu wa mahafali hayo, Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa wasomi hao kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa, katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Alsumait, Dokta Amani Ameid Karume amesema ni jambo la faraja kwa Zanzibar, Tanzania, na Afrika ya Mashariki kwa ujumla kutokana na uwepo wa taasisi hiyo muhimu ambayo ni kivutio kwa wanafunzi kutoka mataifa ya nje.

Dokta Karume ambaye ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amepongeza juhudi kubwa zinazochukuliwa na Chuo Kikuu hicho katika kufanikisha maendeleo ya elimu ya juu nchini kwa takriban miaka 23 iliyopita tangu kilipoanzishwa.
Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Msafiri Mshewa amesema wameweza kufanikisha masomo ya Shahada ya Umahiri katika Shariah na Fiq-hi ya Kiislamu mwaka jana na sasa wanaelekea kuanzisha shahada za umahiri katika Saikolojia ya Ushauri nasaha na Teknolojia ya Mawasiliano, hatua ambayo itawapa fursa wahitimu kujiendeleza hapa nchini.

Amesema chuo hicho kimeamua kupitia upya mitaala yake kwa kuzingatia vipengele vya Uchumi wa Buluu ambao ni eneo pana la kufanyia tafiti, ili kusaidia katika kutimiza ndoto ya Wazanzibari na kuhamasisha maendeleo ya nchi kiuchumi.
Chuo Kikuu cha Al-Sumait kimetoa wataalamu wengi katika nyanja za Elimu, Teknolojia ya Mawasiliano na Saikolojia ya Ushauri Nasaha ambao ni kutoka Zanzibar, Tanzania, Afrika Mashariki na kwingineko ulimwenguni.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia na wa Kijamii, wamejumuika katika Mahafali hayo ambao ni pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Simai Mohamed Said, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Dokta Saada Mkuya Salum, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, na baadhi ya Wakuu wa Vyuo Vikuu vya ndani na nje ya Zanzibar.

Jumla ya wahitimu 278 wametunukiwa Shahada za Kwanza na Stashahada (diploma) katika masomo ya Sanaa na Sayansi, miongoni mwao wahitimu 238 wa Shahada za Kwanza, na wahitimu 40 wa Stashahada katika fani mbali mbali za taaluma na hivyo kufikisha idadi ya whitimu 4,551 wa Shahada ya Kwanza, waliopitia katika Chuo Kikuu hicho tangu kianzishwe mnamo mwaka 1998.
Hafla ya Mahafali hayo ilipambwa na harakati mbali mbali ambazo ni pamoja na maandamano ya wahitimu, Bendi ya Jeshi la Polisi, kutunuku vyeti na zawadi kwa wanachuo waliofanya vyema zaidi katika masomo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news