NA MWANDISHI MAALUM
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo Januari 11, 2022 akiwa nchini Malawi amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Organ Troika Summit) pamoja na Jamhuri ya Msumbiji na nchi zinazochangia vikosi katika jeshi la utayari la SADC lililopo nchini Msumbiji.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akishiriki katika mkutano wa Dharura wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Organ Troika Summit) pamoja na Jamhuri ya Msumbiji na nchi zinazochangia vikosi katika jeshi la utayari la SADC lililopo nchini Msumbiji leo Januari 11,2022 Lilongwe Malawi. (Picha na OMR)
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Troika ambaye pia ni Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesisitiza umuhimu wa kuiunga mkono Jamhuri ya Msumbiji katika mapambano yake dhidi ya mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea katika Jimbo la Cabo delgado Kaskazini mwa Msumbiji.
Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Lazarus Chakwera akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Mpango Lilongwe, Malawi muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji, Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Amesema ni muhimu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana katika kuimarisha ulinzi na usalama na kurejesha hali ya amani na utulivu katika maeneo yalioathiriwa na mashambulizi ya ugaidi.