NA MWANDISHI MAALUM
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango leo Januari 29, 2022 ametembelea Makumbusho ya Kihistoria ya Dkt. David Livingstone iliyopo Ujiji mkoani Kigoma.

Makamu wa Rais amejionea eneo la kihistoria alipofikia Mmisionari na mpelelezi Dkt. David Livingstone mwaka 1869 ambapo pia baadae eneo hilo alifika mwandishi kutoka Uingereza, Henry Stanley mwaka 1871.

Akitoa maelezo kwa Makamu wa
Rais muongoza watalii katika makumbusho hiyo, mzee Kassim Mbingo amesema
eneo la Makambusho hayo licha ya kuhifadhi historia muhimu ya ujio wa
David Livingstone, lakini pia imebeba historia na utamaduni wa wakazi wa
mkoa wa Kigoma ikiwemo maisha yao, vyakula, mavazi , silaha za jadi ,
vyombo vya kale pamoja na vyombo vya usafiri walivyotumia katika Ziwa
Tanganyika.
Akizungumza baada ya kutembelea makambusho hayo Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuendelea kutunza na kuhifadhi historia adhimu ya nchi yetu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.
Amewaasa watanzania kuona umuhimu wa kufika katika maeneo ya
kihistoria ya nchi ili kuweza kujifunza mengi ikiwemo utamaduni katika
maeneo husika. Amewataka viongozi kuwapa motisha wanafunzi wanaofanya
vizuri darasani kwenda katika vivutio vya utalii na utamaduni.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakimsikiliza muongoza watalii mzee Kassim Mbingo juu ya eneo alilofikia mpelelezi Dr Livingstone mwaka 1869 Ujiji mkoani Kigoma. Januari 29,2022.

Aidha, Makamu wa Rais
ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii wakishirikiana na Wizara ya
Utamaduni kukisaidia kituo cha Makambusho ya Dkt. Livingstone ili kiweze
kuendelea kutoa elimu na kuhifadhi vema historia hiyo.
Aidha amemsihi
muongoza watalii katika kituo hicho mzee Kassim Mbingo kuandika kitabu
kitachoweza kurithisha maarifa alionayo kwa vizazi vijavyo.


Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ametembelea pembezoni mwa Ziwa Tanganyika na kuwasalimia wavuvi na watumiaji wa ziwa hilo ambapo amewataka watanzania wote kuendelea kulinda vyanzo vya maji pamoja na usafi katika maeneo ya vyanzo vya maji.
Amesema rasilimali ya maji ni muhimu katika maendeleo ya nchi hivyo kila mmoja aone umuhimu wa kulinda kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadae.
Tags
Habari