NA SOPHIA FUNDI
MADIWANI Halmashauri Wilaya ya Karatu mkoani Arusha wamelaani vikali kauli chafu zinazotolewa na maaskari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pale wanapoarifiwa kuhusu wanyama wanaoshambulia wananchi.
Walieleza masikitiko yao kwa wananchi waliopo pembezoni mwa Hifadhi ya Ngorongoro kushambuliwa na wanyama na kuuawa ambapo wameomba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuweka uzio wa umeme ili kuzuia wanyama wakali wanaotoka hifadhini na kuingia kwenye maeneo ya wananchi na kuwashambulia wananchi na kuwaua.
Akichangia hoja, Diwani wa Kata ya Oldian, Peter Mmassy amesema kuwa ni jambo la kusikitisha ndani ya mwezi mmoja wananchi watatu wanauawa na mbogo katika kata yake na kuacha hofu ya maisha ya wananchi wa maeneo ya pembezoni mwa hifadhi.
Amesema kuwa, mikakati hiyo wameweka kwenye kikao cha pamoja cha wadau wakiwemo wenye mashamba ya mikataba yaliyopo pembezoni mwa hifadhi kufyeka maeneo yao ambayo hayatumiki kwani wanyama wakitoka hifadhini wanajificha kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ambaye ni afisa mhifadhi daraja la 2, Mlungwana Mchomvu aliwaomba madiwani kushirikiana katika kuwakabili wanyama wanaotoka hifadhini kwani wanyama hawana mipaka.
Akizungumzia suala la kauli alisema kuwa watafuatilia suala hilo kwa maaskari wanaofanya hivyo na watachukuliwa hatua.
Tags
Habari