NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Juma Raibu akiwa katika ziara ya kutembelea madarasa yaliyojengwa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 amezungumza na waalimu na wanafunzi huku akifafanua faida kedekede za ujenzi wa madarasa hayo.
Meya huyo amedai tayari kwa asilimia kubwa ujenzi umekamilika na madarasa hayo yameanza kutumika na yamekuwa msaada mkubwa katika manispaa hiyo.
Amesisitisa walimu wakuu kuacha mara moja kuwarudisha nyumbani watoto kwa kisingizio cha michango, kwani Rais Samia amekuwa akitoa Shilingi Bilioni 28 kila mwezi nchini kote kugharamia uendeshaji wa shule za serikali.
"Ndugu zangu walimu kwanza niwapongeze kwa kufanya kazi njema na bora sana ya kuwafundisha watoto wetu, lakini pili niwatake muongeze bidii ili Manispaa yetu ipae zaidi na zaidi kielimu katika nafasi za kitaifa na tatu niwatake walimu wakuu kuacha mara moja kuwarudisha mjumbani wanafunzi kisa michango, kwani hela hizi zimeshalipwa na Rais Samia kila mwezi Bilioni 28,"amesema.
Pia Mstahiki Meya huyo amewataka wazazi wote wa manispaa hiyo kuwaleta na kuwaandikisha shuleni watoto wote wanaopaswa kuanza shule za msingi na sekondari, kwa sababu ni elimu bila malipo.
"Watoto waambie wazazi wote wawalete watoto waliobaki majumbani waje kupata elimu ili iwe mkombozi wa maisha yao na taifa kwa ujumla na hivi sasa elimu ni bila malipo, kwani serikali ya Rais Samia inamaliza yenyewe kila jambo,"amesema.
Meya amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waje kulisaidia taifa siku za usoni.
Aidha,kwa msisitizo Meya huyo amewafundisha wanafunzi wa kidato cha kwanza somo la Biolojia katika mada ya utangulizi.