NA MWANDISHI MAALUM
MJUMBE wa Kamati Kuu cha Chama Cha ACT- Wazalendo, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema wanawake wenye upeo wa kubuni na kutekeleza program na mipango mbali mbali ya chama ni mtaji na hazina kubwa ya chama chochote cha Siasa.
Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo leo Januari 26, mara baada ya kuzindua rasmi Kadi ya Wanawake ya Chama hicho huko katika Hoteli ya Lamada,Ilala jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwepo wanawake wa aina hiyo ni muhimu katika juhudi za kujenga na kuimarisha chama, kwa vile watabuni na kutekeleza mipango na program mbali mbali ambazo watazisimamia wenyewe kwa ufanisi.
Mhe. Othman aliyeambatana na mke wake Mama Zainab Kombo Shaib, sambamba na kuwapongeza wanawake wa chama hicho kwa kuwa wabunifu na kuonesha uwezo mkubwa katika kuendesha mipango yao, pia amewataka kusimamia dhamira ya kweli katika umoja na mshikamano ili kuyafikia malengo ya Chama hicho.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo amewasili mjini Dar es Salam kushiriki vikao mbali mbali vya Chama ikwemo Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano mkuu wa Chama hicho, unaotarajiwa kufanyika Januari 29.
Naye Mjumbe wa Kikosi kazi cha Ngome ya Wanawake wa Chama hicho Bi. Severina Mwijage, amesema kwamba Chama chao kimeamua kuanzisha kadi ya wanawake wa chama hicho kwa dhamira ya kuongeza ushajihishaji na ushiriki zaidi wa wanawake katika harakati za kujenga chama.
Picha zote na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.