Msemaji Mkuu wa Serikali aanika mafanikio ya kihistoria ya Serikali ya Awamu ya Sita

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kihistoria kuanzia mijini hadi vijijini, hatua ambayo inatoa ishara njema kwa ustawi bora wa uchumi wa Taifa letu na jamii kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa leo Januari 16, 2022 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kupitia taarifa kuhusu Serikali na utekelezaji wa majukumu yake unaoongozwa na Mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa. 
Sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020/25 na ahadi za viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taarifa hiyo ameitoa akiwa mkoani Njombe.

"Ndugu zangu Waandishi wa Habari na Watanzania wote mnaofuatilia mkutano huu kupitia vyombo vya habari. Nawasilimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...

"Ninayo furaha kukutana nanyi leo hapa Njombe kuendeleza utaratibu wangu wa kutoa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali. Awali ya yote napenda kuwatakia nyote heri ya Mwaka Mpya wa 2022, na nawaombea uwe mwaka wa mafanikio, ushindi, upendo na kama kawaida yetu Watanzania uwe mwaka wa kudumisha amani, utulivu, mshikamano na upendo wa dhati kama tulivyojiwekea misingi ya tangu uongozi wa Waasisi wa Taifa letu Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume. 

Kwangu, hapa Njombe ni nyumbani, mimi kwetu ni Ilembula kule Wilayani Wanging’ombe na Ilungu kule Makete. Kwa hiyo leo nipo nyumbani hasa, sasa sina hakika kama Waandishi wa Habari mliopo hata mnazijua lugha za hapa Njombe. 

Mapembelo Vhavhene??? 

Kamwene??? 

Ndugu zangu tumekutana hapa kwa utaratibu ule ule wa kupeana taarifa kuhusu Serikali na utekelezaji wa majukumu yake unaoongozwa na Mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ambayo sasa imebakiza miaka 3 na tunajiandaa kwa Dira nyingine na Maendeleo wa Taifa wa Miaka 5, utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020/25 na ahadi za viongozi wetu wakiongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mara ya mwisho nilikutana na Waandishi wa Habari Mjini Iringa tarehe 31 Novemba, 2021 na baada ya hapo sikutoa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali kwa lengo la kupisha taarifa za Waheshimiwa Mawaziri waliokuwa wakieleza nchi yetu imefanya nini katika kipindi cha miaka 60 tangu tupate Uhuru. Naomba ndugu zangu Waandishi wa Habari mpokee shukrani zangu za dhati kwa kufanya kazi nzuri ya kutangaza taarifa zilizotolewa na Waheshimiwa Mawaziri kuhusu sekta wanazozisimamia. 

Leo kama ilivyokawaida, nitatoa taarifa yang una baada ya taarifa hii nitawapa nafasi ndugu zangu Waandishi wa Habari kuuliza maswali, na pia nitawapa nafasi wananchi kuuliza maswali kupitia namba yetu ya simu ambayo ni 0733111111. 

Kabla sijaanza kutoa taarifa, naomba kwa unyenyekevu mkubwa niwasilishe salamu za upendo za Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenu wananchi wa Njombe. Mhe. Rais anawapenda sana, anatambua juhudi zenu za kujiletea maendeleo na anawashukuru kwa kumuungano mkono yeye na Serikali anayoiongoza. Zaidi atakapokuja kufanya ziara hapa Njombe mtamsikia yeye mwenyewe, sasa ndugu zangu atakapopanga ziara hapa Njombe naomba msiniangusha, tumkaribishe kwa bashasha mpaka atamani kukaa hukuhuku Njombe. 

Samia Suluhu Hasssan hoyeeeeee!!!!! Nilikuwa nachomekea tu. 

1. Taarifa yangu itaanzia hapa Njombe

Nyote mnafahamu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongoza nchi yetu kwa mafanikio makubwa katika kuleta maendeleo, kudumisha ulinzi na usalama na kuboresha ustawi wa wananchi wake. Njombe haikuachwa nyuma, kuna kiradi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa hap ana nyote ni mashahidi juu ya yanayoendelea kutekelezwa hapa Njombe. 

Kwa ujumla wake, Mhe. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani tarehe 19 Machi, 2022 hadi sasa ni miezi 9. Katika kipindi hiki Njombe imepokea shilingi Bilioni 375.4 ambazo zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo na kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. 

Njombe ni Mkoa wa kilimo kwa sehemu kubwa, ni moja ya Mikoa inayotegemewa kuzalisha chakula na sasa ni Mkoa ambao unaibuka kwa kasi kubwa kuzalisha mazao ya biashara. Kwa hiyo sehemu kubwa ya fedha zilizoletwa hapa Njombe zimeelekezwa katika ujenzi wa barabara ili kurahisisha shughuli hizi za maendeleo kwa wananchi wa Njombe na Taifa kwa ujumla. 

Katika barabara pekee yake Njombe imepokea shilingi Bilioni 277 ambazo zinajenga barabara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), kwenye afya Serikali imeleta shilingi Bilioni 7.2, Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 zimekuja shilingi Bilioni 4.7, fedha za tozo za miamala ya simu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa zimeletwa shilingi Milioni 150, kwa ajili ya vituo vya afya shilingi Bilioni 1.75, fedha za dawa kupitia MSD shilingi Bilioni 24, fedha nyingine za zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeletwa shingi Bilioni 11, ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe shilingi Bilioni 21.7 na nyingine nyingi. 

Kuna miradi mahususi ambayo imeendelea kutekelezwa bila kusimama na hapa ningependa kuitaja baadhi yake 

i. Ujenzi wa barabara ya Njombe – Makete kilometa 107.4 

>Sehemu ya Njombe – Moronga (kilometa 53.9), ambayo ujenzi wake utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 109.2, kazi imefikia asilimia 95.68 na nyote mnaona sasa watu wanateleza tu kwenye lami. Mkandarasi anamaliziamalizia kazi ndogo ndogo zilizobaki.

>Sehemu ya Moronga – Makete kilometa 53.5 ambayo ujenzi wake utagharimu shilingi Bilioni 110.4, kazi imefikia asilimia 86 (kilometa 49 kati ya 53.5 za lami zimekamilika) halikadhalika nyote mnaona kazi inayoendelea. 

ii. Kuna ujenzi wa barabara nyingine ya Itoni – Ludewa – Manda (Km 211.42) kwa kiwango cha lami na zege. 

>Ujenzi wa kipande cha pili cha Lusitu – Mawengi (kilometa 50) kwa zege kwa gharama ya shilingi Bilioni 159.2, ujenzi umefikia asilimia 83.46 ambapo kilometa 44.93 umekamilika. Kazi hii ilipaswa kuwa imekamilika Oktoba mwaka jana 2021. Japo kumetokea kuchelewa kwa kazi kidogo, lakini nyote mtakuwa mashahidi wa jinsi kazi kubwa ilivyofanyika, ya kukata milima na kujenga barabara ya ZEGE ya aina yake.

>Kipande cha Itoni – Lusitu kilometa 50, taratibu za kumpata Mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi zimefikia hatua za mwisho na wakati wowote akipatikana kazi zitaanza. 

iii. Kuna miradi mingine mingi ya ujenzi wa barabara za Mjini, hapa Njombe Mjini, pale Mji wa Makambako na sehemu nyingine nyingi. Hata Kijijini kwangu Ilembula kule ambako ni Kamji pia kuna mkandarasi anajenga kilometa 1 ya lami. Haya yote ni maendeleo ambayo Mhe. Samia Suluhu Hassan ameamua kuyaleta kwa Watanzania. 

iv. Natambua ipo kiu kubwa ya wananchi wa Njombe kuhusu mradi wa makaa ya mawe na chuma wa Liganga na Mchuchuma uliopo Wilaya ya Ludewa. Nataka kuwahakikishia wananchi wa Njombe kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa mradi huu sio tu kwa wananchi wa Njombe bali kwa Taifa zima kwa ujumla. 

Wote mtakumbuka kulikuwa na makubaliano ya kuanza kutekeleza mradi huu kwa ushirikiano kati ya Serikali yetu kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Mwekezaji kutoka China. 

Mradi huu haujaanza kwa sababu majadiliano kati ya Mwekezaji na Serikali hayajakamilika, lengo likiwa ni kulinda maslahi yenu wananchi wa Njombe na Taifa. Serikali imechukua hatua madhubuti za kusukuma kukamilika kwa majadiliano haya na wakati wowote mtajulishwa nini kinaendelea. Lengo ni mradi huu uanze kutekelezwa haraka. 

Kwa sababu kutoka Mchuchuma na Liganga tunatarajia;  

>Kupata makaa ya mawe takribani tani Milioni 428,

>Megawati 600 za umeme,

>Chuma takribani tani Milioni 126 ambacho kinahitajika sana ulimwenguni.

>Madini ya TITANIUM na VANADIUM, 

>Tutazalisha ajira takribani 6,414,

>Tutajenga barabara ya lami ya kilometa 52. 
 

>Uwekezaji katika mradi huu unatarajiwa kuwa Dola za Marekeni takribani Bilioni 3 (Sawa na takribani shilingi Trilioni 6.9) 

Kwa hiyo ndugu zangu wa Njombe, msiwe na shaka, mradi huu utatekelezwa. Serikali imeamua kuwa sasa mazungumzo yafike mwisho kama mwekezaji aliyepo anaweza kutekeleza kwa kadiri tutakavyokubaliana atatekeleza na kama sivyo basi tutatafuta mwekezaji mwingine wa kutekeleza mradi huu wenye manufaa makubwa kwa nchi yetu. 

v. Hapa Njombe Serikali inatekeleza ujenzi wa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba pale Idofi – Makambako. Tunajenga kiwanda cha kuzalisha gloves yaani mipira ile ya kuvaa mikononi kwa madaktari na wauguzi ( kitakuwa na uwezo wa kuzalisha gloves… kwa saa) na tunajenga viwanda vya kuzalisha vidonge na dawa za maji. 
 

>Kiwanda cha gloves ujenzi wake umekamilika na kimeanza majaribio.

>Kiwanda cha dawa za ngozi na majengo matatu ya viwanda vya vidonge, rangimbili na dawa za maji.

>Pia tunajenga maghala ya kuhifadhia malighafi na nyumba za watumishi

>Ujenzi wa viwanda hivi upo zaidi ya asilimia 50. Kwa ujumla gharama zilizotumika mpaka sasa ni shilingi Bilioni 16.779 

Ndugu zangu wa Njombe, viwanda hivi vikikamilika vitaokoa fedha nyingi ambazo Serikali imekuwa ikitumia kuagiza dawa kutoka nje ya nchi na pia vitatusaidia sana kupunguza gharama za dawa kwa wananchi. Kiwanda hiki tu cha Idofi kinatarajiwa kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni 33 kwa mwaka, achilia mbali kiwanda cha Keko kilichopo Dar es Salaam na vingine ambavyo Serikali yetu imeamua kuanza kuvijenga. 

Tunataka nchi yetu ifike mahali ambapo sehemu kubwa ya dawa itatengenezwa hapa hapa nchini. Kwa sasa ukiangalia bajeti yetu ya dawa na vifaa tiba kwa mwaka ni zaidi ya shilingi Bilioni 270, fedha hizi katibu zote zinapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kuagiza dawa na vifaa tiba. Sasa tunataka Mabilioni haya yaingie mifukoni mwa Watanzania. 

vi. Ndugu zangu wa Njombe, Serikali kwa dhati kabisa inawapongeza sana kwa juhudi zenu kubwa katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo. Tunatambua jinsi mlivyojikita katika uzalishaji wa viazi mviringo. Viazi hivi vinaliwa karibu nchi nzima ya Tanzania. Kule Wilayani Makete kuna viazi vinalimwa bila kutia mbolea na hivi ni viazi adimu kabisa duniani (Organic Potatoes). 

Njombe ni wazalishaji wa mbao. Wana Njombe mmepanda mashamba makubwa ya miti na mnavuna na kuuza mbao. Takwimu zinaonesha mwaka jana (2021) Njombe imezalisha meta za ujazo 1,005,281 za mbao ambazo zinapelekwa maeneo mbalimbali ya nchi yetu na nje ya nchi. Kutokana na uvunaji huu wa mbao Njombe imefanikiwa kukusanya ushuru wa shilingi Bilioni 7 na Milioni 423 ambazo zimeingia katika halmashauri kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi. Hongera sana wananchi wa Njombe. 

Pia katika siku za karibuni Njombe imeibuka kuwa mzalishaji mkubwa wa matunda aina ya parachichi (Avocado), takwimu zinaonesha katika mwaka 2020/21 Njombe imevuna na kuuza tani 9,402 za parachichi zenye Bilioni 15.6 ambazo zimelipwa kwa wakulima. Hongera sana wakulima wa parachichi. 

Ndugu zangu Serikali inawapongeza sana wananchi wa Njombe kwa juhudi hizi. Mimi mwananchi wa Njombe, wakati mwingine nikisikia watani wetu wanatutania kwa jinsi baadhi yetu tulivyokamata biashara kwa kutubambikiza zile tuhuma zile mnazijua huwa nacheka sana. Lakini huwa nawaambia kwa kujiamini kabisa kwamba Njombe kuna wachapa kazi wasiochoka, ndugu zangu naomba tuendelee hivyo. Kwa kuchapa kwetu kazi tunajenga uchumi wetu, tunajenga uchumi wa nchi na tunasaidia Serikali kupata mapato ambayo yanatusaidia sisi na Watanzania wenzetu kupata huduma za kijamii kama barabara, maji, dawa, umeme nk. 

vii. Mradi wa Mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19. 

Nyote mnafahamu kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuwapigania Watanzania alifanikisha nchi yetu kupata mkopo nafuu kutoka shirika la fedha dunia (IMF) kiasi cha shilingi Trilioni 1.3. Fedha hizi zimepeleta mapinduzi makubwa katika sekta za huduma za jamii hasa afya, elimu na maji kupitia mradi wa Mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19. 

Sasa Njombe haijaachwa kando katika fedha hizi. Nataka niwaambie ndugu zangu Serikali ya Awamu ya Sita imeleta nini hapa Njombe kupitia mradi huu;

>Njombe imepokea shilingi 7,160,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Afya na Elimu. Kati ya fedha hizo Tsh. 4,720,000,000/= ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa. Tumejenga madarasa 192 (Ludewa – 47, Makambako TC – 26, Makete – 22, Njombe DC – 24, Njombe TC 37 na Wangingómbe 36) katika shule za Sekondari.

>Tumejenga Madarasa 32 ( Mji wa Makambako – 12, Makete – 2, Halm Wilaya ya Njombe – 4 na Wangingómbe 14) katika Vituo Shikizi pamoja na mabweni matatu (03).

>Serikali imeleta shilingi 2,440,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Afya ya ‘’Emergency Medical Department (EMD)’’ katika Halmashauri za Makete, Wangingómbe na Makambako Mji, Ujenzi wa ‘’Intensive Care Unit (ICU)’’ katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, utumenunua mashine za ‘X-Rays’ katika Halmashauri za Wilaya za Njombe na Wangingómbe. 

Lakini pia mtakumbuka kuwa katika bajeti ya mwaka huu Serikali inatekeleza sheria kwa kukusanya tozo katika miamala ya simu, na maelekezo ya Mhe. Rais Sami ani kuwa wananchi waelezwe fedha hizo zinafanya nini. 

Nataka niwaambie ndugu zangu wa Njombe hapa Njombe tumepata mgao mkubwa wa fedha hizi, tumepokea Tshs 1,900,000,000 kutoka kwenye tozo ya miamala ya simu. Kati ya hizo Tshs. 150,000,000 kwa ajili ya umaliziaji wa maboma ya madarasa 12 ya shule za Sekondari katika Halmashauri za Ludewa (03), Wangingómbe (03), Makambako TC (03) na Njombe TC(03), na Tshs. 1,750,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vipya vya Afya kwenye Tarafa zisizo na Vituo vya Afya saba (07) katika Halmashauri za Ludewa (01), Makate (02), Njombe(01), Wangingómbe (01), Makambako Mji (01) na Njombe TC (01). 

Kuna miradi mingine mingi ambayo inatekelezwa hapa Njombe, wote mnaliona soko kubwa la kisasa kabisa lililojengwa hapa Njombe Mjini, lile soko 

Njombe hoyeee!!!!! 

BAADA YA KUUNGAZIA MKOA WA NJOMBE naomba sasa tuangazie masuala mengine ya Kitaifa ambayo yamejitokeza siku za karibuni na Serikali inaona ni vyema, nyie wananchi mkapata ufafanuzi. 

2. Umeme 

Nchi yetu imeendelea na juhudi mbalimbali za kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme. Uwezo wa mitambo yetu ya kuzalisha umeme (Installed Capacity ni Megawati 1,602 ilihali mahitaji yetu ni takribani megawati 1,400. Hata hivyo tumepata changamoto kidogo katika uzalishaji wa umeme katika miezi ya Oktoba na Novemba mwaka jana ambapo uzalishaji katika vyanzo vya kutumia maji ulishuka kwa kati ya asilimia 30 hadi 35. Hata hivyo Desemba na Januari mvua zimeanza kunyesha hasa maeneo ya Iringa na hali imeendelea kuimarika. 

Pamoja na juhudi hizi, Serikali kupitia TANESCO inaendelea kufanya juhudi za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo vingine. 

>Ubungo namba 3 – tunafunga mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ambapo tutapata megawati 112, mpaka sasa tayari megawati 60 zimeanza kuzalishwa na kuingizwa katika gridi ya Taifa, megawati 72 zilizobaki zitaingia kwenye gridi ya Taifa ifika mwishoni mwa mwezi huu Januari.

>Tunaendelea kufanya upanuzi wa mradi Kinyerezi namba 1 ambapo tutapata megawati 185, kazi hii tunatarajia itakamilika ifikapo Julai mwaka huu 2022.

>Bwawa la Kihansi linaendelea kujaa maji, matarajio yetu kadiri mvua zinavyoendelea kunyesha litapandisha uzalishaji wake hadi kufikia uwezo wake wa juu wa megawati 180, ikilinganishwa na megawati chini ya 100 za hivi sasa. 

Serikali inatambua kumekuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu ya kukatika kwa umeme. Changamoto hii pia inachangiwa na hitilafu katika miundombinu ya umeme (kuanguka kwa nguzo, kuharibika kwa transfoma na wakati mwingine matengenezo ambayo yanafanywa na mafundi wetu ambayo yanalazimu umeme kukatwa ili kuruhusu matengenezo hayo kufanyika). 

Shirika letu la umeme (TANESCO) linafanya juhudi kubwa kukabiliana na changamoto hii, tunachowaomba ndugu wananchi tuendelee kuwa watulivu wakati juhudi hizi zinafanyika. 

Lakini pia kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuomba kuunganishiwa umeme lakini wanachelewa kuunganishiwa umeme huo. Serikali imefanya tathmini juu ya jambo hili na kubaini kuwa pamoja na mafundi wetu kuelemewa na maombi mengi ya watu pia kiwango cha shilingi 27,000 cha gharama za kuunganishia kimesababisha TANESCO kushindwa kumudu gharama maunganisho. 

Kwa hiyo kwa sasa, TANESCO imetoa viwango vipya vya uunganishaji umeme vilivyoanza kutumika tarehe 05 Januari, 2022 kama ambavyo vimetolewa na Mamlaka ya udhibiti wa maji na nishati (EWURA). Viwango hivyo ni kwa wateja wa mijini, wateja wa vijijini wanaendelea kuunganishiwa umeme kwa bei ya shilingi 27,000. 

Naomba wananchi mliopo vijijini muwe macho kwa sababu kumeanza kujitokeza matapeli ambao wanakuja kuchukua fedha nyingi kwa madai ya kuwafanyia mipango. 

Gharama za uunganishaji kwa wateja wa Mjini wa njia moja walio ndani ya mita 30 kutoka kwenye miundombinu ya TANESCO (nguzo) watalipia shilingi 320,960, walio ndani ya mita 70 watalipia shilingi 515,618 na walio ndani ya mita 120 watalipia shilingi 696,670. 

Kwa wateja wa njia tatu waliopo Mjini, viwango ni kwa waliopo meta 30 kutoka miundombinu ya TANESCO watalipia shilingi 912,014, walio ndani ya meta 70 watalipia shilingi 1,249,385 na waliopo meta 120 watalipia shilingi 1,639,156. 

3. Miradi ya Kimkakati inaendelea vizuri 

· MAENDELEO YAUJENZI WA SGR, 

Mpaka sasa ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR imekalimilika kwa asilimia zifuatazo: 

a) Dar es Salaam – Morogoro (95%) 

b) Morogoro – Makutopora (77%) 

c) Makutopora – Tabora (Mkataba umesainiwa Disemba 28, 2021) 

d) Tabora – Isaka (taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea) 

e) Mwanza – Isaka (4%) 

Kwa Kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, kwa sasa maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kuanza treni ya majaribio ambayo inatarajiwa kuanza mwezi wakati wowote kabla ya mwisho wa Aprili 2022. 

Lakini majaribio mengine ya miundombinu YANAENDELEA kama vile madaraja, vituo vya kupooza umeme, booster station za umeme, mifumo ya majengo ambayo ina mawasiliano ya mtandao na simu, njia za mawasiliano, njia za umeme wa treni na mengineyo. 

Na pia mkumbuke katika njia ya Dar es Salaam hadi Morogoro hadi Kilosa inaendelea kutumika. Na sasa hivi kazi kubwa inaendelea kuunganisha kipande cha kutoka Pugu hadi Posta (pale inapoanzia stesheni ya Dar es Salaam). Tunatajia eneo kuwa limeunganishwa ifikapo mwisho mwa mwezi Februari na treni ya Wahandisi itafika hadi Mjini. 

Tayari Serikali imeagiza mabehewa 80 ambayo ni sawa na treni 10 za kisasa ziitwazo Electric Multiple Unit (EMU) kutoka Korea Kusini, hivi sasa utengenezaji wa unaendelea. Tumeagiza mabehewa ya abiria 59 na vichwa vya treni 17 vya umeme kutoka Korea Kusini kwa ajili ya kuanza kutumia katika njia hii. 

Kwa upande wa mabehewa ya mizigo tumeagiza mabehewa 1,430. Ndani yake kuna mabehewa ya kubebea kontena, kuna ya kuchukulia magari, ya kubebea vyakula kama nyama na mizigo ya kawaida. Utengenezaji wa mabehewa hawa unafanyika nchini China 

Nataka niwakumbushe tu, kipande hiki cha kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora Singida kitakapokamilika Mwishoni mwa mwaka huu 2022 wananchi watakuwa na uwezo wa kusafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa muda wa kati ya saa 2:45 hadi 3, badala ya saa 8 mpaka 9 wanazotumia hivi sasa kwa kutumia mabasi, au saa 10 kwa treni. 

Kwa wale waliowahi kusafiria treni hizi wanajua jinsi usafiri huu ulivyo salama, wa raha na haraka. Treni zetu zitakuwa na uwezo wa kutumia umeme na pia mafuta ya Diesel. Na zaidi ya hapo zitakuwa na uwezo wa kuhifadhi umeme ambao unaweza kutumika kwa dakika 48, endapo umeme wa kwenye njia utakuwa umekatika. 

Kwa hiyo wale wanasema treni hizi zitakwama kwa sababu umeme unakatika, basi wajue sio kwa treni hizi. Tuna umeme wa TANESCO, tuna Majenereta na tuna umeme wa treni yenyewe. 

Kupitia mradi huu jumla ya ajira za moja kwa moja zipatazo 16,000 zimetolewa na kuchangia mishahara yenye thamani ya Bilioni 224, zabuni na kandarasi zenye thamani ya shilingi trilioni 1.776 zimetolewa kwa wazabuni na wakandarasi wadogo 1,663. 

Aidha, hadi sasa malipo yenye jumla ya shilingi Trilioni 5.340 za kitanzania yamefanyika kwa wakandarasi wa vipande vitatu vinavyoendelea na ujenzi. Kipande cha tatu kati ya Makutupora – Tabora kilichosainiwa tarehe 28 Disemba, 2021 kinatarajiwa kutumia jumla shilingi Trilioni 14.73 za kitanzania. 

4. Ujenzi wa Bwawa la Nyerere 

Kama mnavyojua tunatajia kuzalisha megawati 2,115 kutoka kwenye chanzo hiki cha mto Rufiji. Kazi za ujenzi zinaendelea vizuri, hakuna kilichosimama na Wakandarasi wanalipwa kadiri wanavyowasilisha vyeti vya kazi. 

Na kwa sababu kumekuwa na upotoshaji kuwa kazi imesimama nataka niwaeleze kinachoendelea huko, kwanza utekelezaji wa Mradi wa huu sasa hivi unafanyika usiku na mchana. Mradi umetoa jumla ya ajira 8,500 ambapo asilimia 90 ni Wazawa na asilimia 10 ni wageni. 

Kufikia Desemba 21, 2021 (Power House), Jengo litalalosimikwa mitambo 9 ya kufua umeme megawati 235 kila mmoja, kazi ya uchimbaji imekamilika na kazi ya usimikaji mitambo inaendelea. 

Ujenzi wa Switch ya Yard (Kituo cha Kupokea na Kusafirisha Umeme wa kilovoti 400 kutoka katika transfoma 27 zilizoko kwenye jengo la mitambo la Power House) umefikia asilimia 60. Kituo hiki ndicho kitasafisha umeme kutoka bwawani hadi katika kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Chalinze, ambapo utaingizwa katika gridi ya Taifa. 

Katika kuhakikisha maji yanakuwepo wakati wote hata wakati wa ukame, Bwawa la Nyerere, lina Mabwawa makubwa 4 (Saddle Dams), yenye urefu wa kilometa 17, ambapo kazi ya hayo mabwawa ni kuzuia na kuhifadhi maji wakati wote. Kazi kubwa inayofanyika katika eneo hili ni kuchimba na kujaza vifusi vya zege kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuzuia maji. Katika eneo hili kazi imekamilika kwa asilimia 35.89, na watu wanafanya kazi usiku na mchana. 

Utekelezaji wa ujenzi wa Bwawa la Nyerere unaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu ya kudumu ikiwemo daraja kubwa na la kisasa litakalo rahisisha usafirishaji wa vifaa vyote vya ujenzi kwenda kwenye mradi lakini pia ndio daraja litakalotumika kuunganisha mikoa ya kusini na pwani. Ujenzi wa daraja hili umefikia zaidi ya asilimia 81.11 kukamilika, ambapo lina urefu wa mita 250, upana wa mita 12. 

Ujenzi wa Makazi ya Kudumu kwa ajili ya wafanyakazi wa mradi wa Bwawa la Nyerere umefikia asilimia 59.13. Nyumba nyingi zimekamilika na nyingine zinaendelea kumaliziwa. 

Eneo lingine ambalo lipo katika utekelezaji wa mradi ni njia kuu tatu za kupitishia maji, yaani Power Water ways. Mashimo haya matatu, ndipo ambapo maji kutoka kwenye bwawa yanapopita kwenda kwenye mashine 9 za kuzalisha umeme. Kazi katika eneo hili inaenda sambamba na mashimo matatu yani Surge Tanks, ambapo mpaka sasa mashimo haya ambayo ni kwa ajili ya maji kupumulia yameshakamilika kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni Pamoja na kuweka bati zito na nene ambalo litawezesha maji kuingia kwenye mashine zitakazozalisha umeme. Utekelezaji wa eneo hili umefikia asilimia 66.16 

Mradi huu ukikamilika utatuletea ongozeko la umeme katika gridi ya Taifa kwa asilimi 136. Mradi huu ndio mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki na ni wa 4 Barani Afrika. 

5. Kukosekana mvua katika baadhi ya maeneo. 

Kumetokea hali ya kukosekana kwa mvua katika baadi ya maeneo nchini, yapo baadhi ya maeneo ambayo bado hayajapata mvua ama mvua zimenyesha kidogo na mara chache. 

Taarifa kutoka Mamlaka ya hali ya hewa zinaonesha kumekuwa na mvua za msimu za chini ya kiwango na wastani katika mikoa ya Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati na Nyanda za juu kusini. Na haya ni maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na ufugaji. 

Serikali inatambua changamoto zinazojitokeza katika maeneo haya. Tunawasihi wakulima kuwasikiliza wataalamu wa kilimo, ambao wanashauri kupanda mazao ambayo yanakomaa haraka kutokana na kuchelewa kwa mvua na pia kutunza vizuri chakula. 

Serikali inatambua madhara ya ukame yaliyojitokeza katika baadhi ya maeneo nchini, nyote mmeona picha ambazo jana zimesambaa mitandano zikionesha mifugo iliyokufa kutoka kule Simbanjiro Mkoani Manyara. Hivi tunavyozungumza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Viongozi wa Mkoa wa Manyara wapo katika ziara ya kutembelea maeneo yote yaliyoathirika ili kujionea hali halisi na wakati wowote Serikali itatoa taarifa. Tunawaomba wananchi muwe watulivu. 

6. Mapambano dhidi ya Uviko -19. 

Ndugu zangu wana Njombe na ndugu Watanzania wote, ugonjwa huu bado upo na unaendelea kuwaathiri ndugu na jamaa zetu. Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana nao, ambapo pamoja na kutekeleza mradi huu unaotumia shilingi Trilioni 1.3 za mkopo nafuu kutoka IMF wataalamu wetu, vyombo vya habari na wadau mbalimbali wanaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu. 

Serikali inawakumbusha Watanzania kuendelea kuchukua tahadhali. Korona ipo na Korona inaua, jikinge na uwakinge na wengine. 

Sambamba na kutoa elimu, Serikali inaendelea kutoa chanjo. Mpaka sasa nchi yetu imepokea jumla ya dozi ……. za chanjo na Watanzania wanaendelea kupokea chanjo katika vituo mbalimbali. Mpaka jana Watanzania ……. Walikuwa wamepokea chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona 19 (Uviko-19). 

Tumesambaza huduma za upatikanaji wa chanjo katika vituo vyote nchini vinavyotoa chanjo. Sasa ni uamuzi wako tu Mtanzania kwenda kwenye vituo hivi na kupokea chanjo, ambayo ni bure na tunasisitiza uchanjaji ni hiari. LAKINI tusisahau wataalamu wanavyosema kuwa ukichanja unakuwa na uhakika kwamba hata virusi vikikupata huwezi kuwa mahututi utatibiwa na utapona, ukipatwa na virusi ukiwa hujachoma chanjo una uwezekano mkubwa wa kuwa mahututi ama kupoteza maisha. 

7. Miradi ya barabara na madaraja. 

Miradi hii inaendelea kutekelezwa, hakuna mradi uliosimama, wakandarasi wanajenga barabara na madaraja na kila hatua wanayofikia wakipeleka madai ya fedha wanalipwa kwa mujibu wa utaratibu. HAKUNA MRADI ULIOKWAMA 

Niwape mifano michache; 

>Barabara ya Chunya – Makongorosi (Mbeya) ujenzi wake unamaliziwamaliziwa, ujenzi wa kilometa 39 kwa gharama ya shilingi Bilioni 59.8 umefikia asilimia 97.

>Barabara ya Makutano – Nata (Mara) pia ujenzi wae upo mwishoni, ujenzi wa kilometa 50 kwa gharama ya shilingi Bilioni 54.6 umefikia asilimia 91.5.

>Barabara ya Rudewa – Kilosa (Morogoro) ujenzi wake wa kilometa 24 kwa gharama ya shilingi Bilioni 33 umefikia asilimia 84.4.

>Barabara ya Wasso – Sale (Arusha) ujenzi wa kilometa 49 kwa gharama ya shilingi Bilioni 89.2 pia unakamilika ukiwa umefikia asilimia 95.3

>Barabara ya Tanga – Pangani (Tanga), ujenzi wa kilometa 50 kwa ghara ya shilingi Bilioni 66.9 umefikia asilimia 22 na kazi inaendelea.

>Barabara ya Kimara – Kibaha (Dar es Salaam), yenye urefu wa kilometa 19.2 (ambayo ina njia nane) na inayojengwa kwa shilingi Bilioni 161.5 ujenzi wa umefikia asilimia 80.5

>Barabara ya Ruangwa – Nanganga yenye urefu wa kilometa 53.2 ambayo inajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 50.3. Ujenzi wake umefikia asilimia 40

>Ujenzi wa daraja la mto Wami (Pwani) lenye urefu wa meta 510 utakaogharimu shilingi Bilioni 67.8 umefikia asilimia 70.4

>Ujenzi wa daraja la JP Magufuli (urefu kilometa 3.2) lile linalounganisha Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria na ambalo ujenzi wake utagharimu shilingi Bilioni 600 ujenzi wake umefikia asilimia 36 

Kuna barabara za lami ambazo ujenzi wake umekamilika, kuna barabara ya Uselula-Komanga, Komanga-Kasinde na Kasinde-Mpanda Mkoani Katavi. 

Pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja, pia kuna ujenzi wa viwanja vya ndege kadhaa nchini mwetu, huko kote kazi zinaendelea; 

>Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato utakaokuwa na njia yenye urefu wa kilometa 2.8 kwa gharama ya shilingi Bilioni 165, kazi ndio imeanza 

>Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Mtwara wenye urefu wa kilometa 2.8 kwa gharama ya shilingi Bilioni 55.2 umefikia asilimia 80

>Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Iringa wenye urefu wa kilometa 2.1 kwa gharama ya shilingi Bilioni 41.1 umefikia asilimia 35

>Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songea wenye urefu wa kilometa 1.86 kwa gharama ya shilingi Bilioni 37 umefikia asilimia 69.7

>Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Geita wenye urefu wa kilometa 3 kwa gharama ya shilingi Bilioni 39.1 umefikia asilimia 95 

>Uwanja wa ndege wa Songwe unajengwa ile njia ya kurukia ndege kilometa 3.3 kwa shilingi Bilioni 14.8 umefikia asilimia 95. Kuna jengo la abiria linalojengwa kwa shilingi Bilioni 14.1 limefikia asilimia 17. Kuna njia zile za ndege kwa gharama ya shilingi Bilioni 5, ujenzi umefikia asilimia 40. 

8. Sekta ya Kilimo. 

Kama nilivyosema hapo awali, Njombe ni Mkoa wa kilimo. Kama ilivyo maeneo mengine duniani, nchi yetu imepata changamoto kubwa ya kupanda kwa pembejeo muhimu ambayo ni mbolea. Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto hii. 

Katika soko la dunia bei ya mbolea imepanda kwa asimilia 100. Wastani wa tani moja ya mbolea imepanda kutoka Dola za Marekani 400 (Ths. 920,000/-) hadi Dola 800 (Ths. 1,840,000/-). Lakini pia ghama za usafirishaji zimepanda kwa zaidi ya mara mbili. 

Na hii yote imesababishwa na madhara ya Uviko-19 (Korona) ambapo viwanda vingi vimepunguza uzalishaji, na hata kiasi kidogo kinachozalishwa kinazalishwa kwa gharama kubwa. 

Matokeo yake hapa nchini bei ya mbolea imepanda kutoka wastani wa shilingi 60,000 kwa mfuko wa kilo 50 hadi shilingi 100,000 na hata zaidi kwa baadhi ya maeneo. 

Kutokana na hali hiyo Serikali imechukua hatua ya kuruhusu wafanyabiashara wengi kuleta mbolea nchini na kurahisisha upakuaji na usafirishaji wa mbolea mara inapofika katika bandari. Sasa hivi mfanyabiashara yeyote anayetaka kuleta mbolea anaruhusiwa ilimradi alete mbolea bora ambayo inapitishwa na mamlaka zetu za udhibiti wa ubora. 

Lakini pia Serikali imeelekeza nguvu katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mbolea inayozalishwa ndani ya nchi. 

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wanaendelea kusimamia kwa karibu uwekezaji wa kiwanda cha mbolea ITRACOM kinachojengwa Dodoma ambacho kitatumia madini ya phosphate na samadi na ambacho tunatarajia kitazalisha tani 600,000 kwa mwaka kuanzia Julai mwaka huu 2022. 

Kiwanda hiki kinamilikiwa na mwekezaji kutoka Burundi ambaye kama nyote mtakumbuka alipatikana kufuatia ziara ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliifanya nchini Burundi na kuwaalika wawekezaji hao kuja kuwekeza Tanzania ili kutatua changamoto ya mbolea kwa wakulima. 

Lakini pili Serikali inakisaidia kiwanda cha mbolea cha Minjingu ambacho kina uwezo wa kuzalisha tani 170,000 kwa mwaka ili kuongeza uzalishaji zaidi wa mbolea zake. 

Viwanda hivi viwili vitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 770,000 ambazo zitatosheleza mahitaji yetu ya mbolea na kuwa na ziada kwa sababu nchi yetu inahitaji kama tani laki 7 hivi za mbolea kwa mwaka. 

Juhudi nyingine, Wizara zetu za Kilimo na Nishati zimeanza kufanya mazungumzo kuhusu uzalishaji wa mbolea kwa kutumia gesi asilia ya Pwani na Mtwara. 

9. Maendeleo ya Bandari 

Kwa ujumla bandari zetu zimeendelea kufanya vizuri, idadi ya meli zinazotumia bandari yetu ya Dar es Salaam imeendelea kuongezeka na hivyo kuongeza mapato kwa Taifa letu licha ya kuwepo kwa changamoto ya Uviko-19 dunia ambayo imeathiri bandari nyingi. 

Kati ya Septemba na Desemba 2021 meli zilizohudumiwa na Mamlaka yetu ya usimamizi wa Bandari (TPA) zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 8.2 (kutoka meli 413 zilizohudumiwa kwa kipindi kama hicho mwaka jana) hadi meli 493 kwa bandari zetu za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. 

Shehena ya mzigo pia imeongezeka kutoka tani Milioni 4.7 hadi tani Milioni 5. Makontena pia yameongezakwa kutoka 178,425 hadi makontena 188,650. Magari pia yameongezeka kutoka 37,503 hadi kufikia 56,139. 

Shehena ya mizigo ya nchi jirani inayopitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 17.1 kutoka tani Milioni 1.471 hadi kufikia tani Milioni 1.722. 

Sasa takwimu hizi maana yake ni kwamba nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kuongeza mapato ya bandari ambayo yameongezeka kwa wastani wa asilimia 4.9. Katika robo hiyo ya pili TPA imekusanya shilingi Bilioni 250 ikilinganishwa na shilingi Bilioni 243.4 za robo ya kwanza. 

Mafanikio haya yanatokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuboresha bandari zetu hasa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio lango letu la Biashara na Uchumi. Tunaboresha huduma za bandari na pia tunaboresha miundombinu ya bandari. 

Mradi wetu we takribani shilingi Trilioni 1 wa kuboresha bandari hii pia unaendelea vizuri. Tumekamilisha kuboresha gati namba 1 hadi 7 na gati ya magari yaani RoRo kwa kuongeza kina hadi kufikia meta 14.5 na sasa hata meli kubwa zinaweza kutumia gati hizi. Kazi ya kupanua lango la kuingilia meli bandarini na kuongeza kina hadi kufikia meta 15.5 inaendelea, mkandarasi ameshafikia asilimia 5 na malipo yake analipwa kama kawaida. 

Sasa hivi tunajiandaa kutekeleza mradi mwingine wa kuboresha mtandao wa reli ndani ya bandari. Tunataka makontena yakishuka kwenye meli yanaunganisha moja kwa moja kweli reli na kwenda kama ni bandari kavu yetu ya Kwara, ama kwenda nchi jirani ama mahali pengine ili kuharakisha ushushaji wa mizigo. Pia tunaendelea na maandalizi ya kupanua na kuongeza kina cha gati namba 8 hadi 11. 

Malengo yetu ni nini. Tunataka baada ya kukamilika kwa miradi hii, bandari yetu ya Dar es Salaam iongeze uwezo wake na kupokea meli kubwa za urefu wa hadi meta 305 (Post Panamax Ships) ambazo zina uwezo wa kubeba makontena kati ya 7,000 hadi 8,000 ikilinganishwa na meli za sasa za kizazi cha pili (second generation ships) ambazo zinabeba kati ya makasha 2,000 na 2,500. 

Tunataka kuongeza uwezo wa bandari ya Dar es Salaam kutoka kuhudumia tani Milioni 16 za sasa hadi kuhudumia tani Milioni 25 kwa mwaka. 

Juhudi kama hizi tunazifanya pia katika bandari zingine 

>Bandari ya Tanga tunaongeza kina katika gati, kazi imefikia asilimia 22. 

>Bandari ya Mtwara tumejenga gati ya meta 300, tumekarabati yadi ya mizigo. Kazi zimekamilika 

>Katika Ziwa Tanganyika ujenzi wa Bandari ya Karema umefikia asilimia 73, Bandari ya Kasanga asilimia 98.2 na tunaendelea kujenga bandari zingine za Kibwesa, Kabwe, Kipiri, Lagosa, Kibirizi na Ujiji Mkoani Kigoma. 

>Katika Ziwa Nyasa ujenzi wa Bandari ya Ndumbi umefikia asilimia 99, na tunajiandaa kuanza ujenzi wa bandari za Mbambabay, Manda na Matema. 

>Katika Ziwa Victoria nako pia uboreshaji wa bandari unaendelea kwa kujenga gati, majengo ya utawala na abiria, maghala ya kuhifadhia mizigo katika bandari za Magarini-Muleba, Nyamirembe-Chato, Bukoba, Kemondo, Mwigobero-Musoma, Lushamba na Nkome. 

Kwa hiyo ndugu zangu mambo yanakwenda vizuri, miradi yote inakwenda na wakandarasi wanaojenga wanalipwa kadiri wanavyokamilisha kazi na kuzalisha vyeti vya malipo. 

10. Miradi ya Maji 

Juhudi za Serikali kutatua changamoto za maji zinaendelea kwa lengo lilile la kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambayo inaitaka Serikali kuwafikishia Watanzania maji kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 Mijini. 

Mpaka sasa usambazaji majini upo wastani wa asilimia 72.3 vijijini na asilimia 86 Mijini. Kumetokea changamoto katika katika kipindi cha mwisho mwa mwaka 2021 miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba lakini sasa hali imeanza kutengemaa baada ya kuanza kwa mvua. 

Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa na midogo, na dhamira yake ya kuchukua maji kutoka kwenye vyanzo vikubwa vya maziwa na mito ambayo ni ya uhakika. 

Kuna miradi ambayo imekamilika hivi karibuni ambayo wananchi sasa wanapata maji ikiwemo Mradi wa maji ya Ziwa Victoria wa Tabora-Igunga-Nzega (Bilioni 617), mradi wa Kagongwa-Isaka (Bilioni 16), Mradi wa Magu (Bilioni 16), Mradi wa Misungwi (Bilioni 13), Mradi wa Lamadi (Bilioni 12) na kuna mradi wa Sumbawanga (Bilioni 35). 

Kuna miradi ambayo ujenzi wake unaendelea, mradi mkubwa wa maji wa Arusha (Bilioni 520) umefikia asilimia 70, mradi wa Mgando-Kiabakari (Bilioni 70) umefikia asilimia 20, mradi wa Orkesument-Simanjiro (Bilioni 40) umefikia asilimia 97, mradi wa Tinde-Shelui (Bilioni 24) umefikia asilimia 20, mradi wa Isimani-Kilolo-Iringa (bilioni 9.2) umefikia asilimia 40. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news