Mwanga yatakiwa kukarabati jengo la Wagonjwa wa Nje Kituo cha Afya Kisangara

NA FRED KIBANO

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange ameagiza kufanyika ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje katika Kituo cha Afya Kisangara wilayani Mwanga kabla ya Aprili 30, mwaka huu. 
Kauli hiyo ya Dkt. Dugange ameitoa Januari 17,2022 baada ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro ambapo amesema miundombinu hiyo haivutii wagonjwa katika kutoa huduma bora, lakini pia wanakusanya mapato yanayozidi shilingi laki nane kwa mwezi kutokana na malipo ya wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu katika kituo hicho.

“Sijaridhishwa na uchakavu mkubwa wa majengo haya ya OPD (wagonjwa wa nje) na sisi kama watawala tupo hapa na gharama za utengenezaji haizidi shilingi milioni moja na nusu kwa jengo la OPD peke yake, sasa sio busara na wala haipendezi kwa wananchi kupata huduma katika kituo hiki chakavu wakati mnakusanya shilingi laki nane kwa mwezi,” alisema Dkt.Dugange. 

Aidha, amewataka Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuchukua hatua kwa watumishi ambao wamekuwa wanalalamikiwa na wagonjwa wakati wakiwapatia huduma hali inayopelekea kupungua kwa hadhi ya utoaji wa huduma bora kwa jamii kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Dkt. Dugange amewaasa viongozi wa kada ya afya na nje ya kada hiyo kusimamia nidhamu ya kazi kwani baadhi ya watumishi wachache wamekuwa na lugha isiyo na staha kwa wagonjwa na hivyo kuwakatisha tamaa kupata huduma kwenye vituo ambavyo watu hao hufanyia kazi.

“Baadhi ya maeneo kumekuwa na malalamiko ya lugha zisizofaa kwa baadhi ya wahudumu wa afya wanaofanya kazi bila kufuata maadili, miongozo, taratibu na kanuni za utoaji wa huduma za afya, sasa tuwe na mfumo wa kufuatilia zahanati, kituo cha afya au hospitali inayolalamikiwa na wananchi,”amesema.

Amesema ni muhimu kujua jambo linalolalamikiwa kwa sababu, watumishi wanaotajwa ili wawajibishe kwa mujibu wa sheria za kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bi. Mwajuma Nasombe amesema wameyapokea maelekezo ya Serikali na kwamba watayafanyia kazi kwa wakati kwa kuondoa kasoro zote zilizojitokeza.

Miradi mingine aliyotembelea Dkt. Dugange ni pamoja na barabara ya Cleopa David Msuya chini ya TARURA na shule ya sekondari Mandaka zote za wilayani Mwanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news