NA MWANDISHI MAALUM
NAIBU Waziri wa Kilimo,Mheshimiwa Anthony Mavunde ametembelea kiwanda cha kuchakata viazi mviringo na kuwahimiza wakulima mkoani Iringa kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo cha mkataba pindi kiwanda hicho kitakapoanza kazi.
Mhe. Mavunde ameyasema hayo leo Januari 25, 2022 alipotembelea kiwanda cha kutengeneza chipsi na crisps (chipsi baridi) kinachomilikiwa na Kampuni ya SAI Energy and Logistics Services Ltd kilichopo Manispaa ya Iringa na kupata maelezo kutoka kwa mwekezaji wa kiwanda hicho,Rajan Mwaruhaa.
Mwaruhaa ameeleza kuwa, kiwanda hicho kina zaidi ya miaka mitatu kimesimama uzalishaji kutokana na ukosefu wa malighafi, ambayo inahitajika kuzalishwa na wakulima kwa kuotesha mbegu bora ya viazi mviringo iliyosafishwa na hivyo kuwa na tija kubwa na kwamba kiwanda hicho kitahitaji tani 18,000 za viazi mviringo na kutoa fursa kwa wakulima 5000 watakaokuwa kwenye mfumo wa 'block farming' (vizimba).
Akiwa kiwandani hapo, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa, uwepo wa kiwanda hicho ni fursa ya ajira kwa wananchi hususani makundi maalum ya wanawake na vijana, hivyo ni muda mwafaka kuitumia ipasavyo.
"Nitakuomba Mheshimiwa Mohammed Moyo, Mkuu wetu wa Wilaya ya Iringa, utusaidie kukaa na wataalam hapa ili mtenge eneo ambalo tutaanzisha shamba la mfano la kilimo cha viazi mviringo kwa kutumia vizimba (block farming) ili wakulima wetu waweze kunufaika na soko linaloletwa na kiwanda hiki,"aliongeza Mhe. Mavunde.
Wakati huo huo, Mhe. Mavunde ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kesho asubuhi tarehe 26 Januari, 2022 wataalam wa viazi mviringo wafike kwa mwekezaji huyo ndugu Rajan na kuhakikisha wanatatua haraka changamoto hiyo ya mbegu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ya Iringa,Mhe. Mohammed Moyo na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini,Mheshimiwa Jesca Msambatavangu wamemuhakikishia Mheshimiwa Mavunde kuwa, watakaa na wataalam wao wa Halmashauri na kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya kutekeleza kilimo cha mkataba kupitia mfumo wa kizimba baina ya wakulima na mwekezaji huyo.
Kuhusu Crisps
Crisps (chipsi baridi) ni vipande bapa na vyembamba sana vya chipsi ambavyo vinakaangwa katika mafuta hadi kukauka kabisa.
Aidha, chipsi hizo huliwa mara nyingi peke yake na mara nyingi vimekuwa na soko kubwa katika maeneo mbalimbali huku vikiuzwa madukani vikiwa katika vifungashio ambapo uliwa kama chakula baridi.
Crisps (chipsi baridi) ni vipande bapa na vyembamba sana vya chipsi ambavyo vinakaangwa katika mafuta hadi kukauka kabisa.
Aidha, chipsi hizo huliwa mara nyingi peke yake na mara nyingi vimekuwa na soko kubwa katika maeneo mbalimbali huku vikiuzwa madukani vikiwa katika vifungashio ambapo uliwa kama chakula baridi.