Rais Dkt.Mwinyi amtunuku Nishani ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 Rais mstaafu Dkt.Ali Mohamed Shein

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemtunuku Nishani ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964, Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mstaafu wa Awamu ya Saba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimvisha Nishani ya Mapinduzi Rais wa Zanzibar Mstaafu wa Awamu ya Saba Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.

Hafla hiyo imefanyika Januari 11,2022 katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, siasa na dini pamoja na wakuu vya vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Nishani hiyo inatokana na uwezo aliopewa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi chini ya kifungu cha 10 (1) na (2) cha Sheria ya Mambo ya Rais Namba 3 ya mwaka 2020, na kama ilivyotangazwa katika tangazo la Kisheria No. 24 ya mwaka 2022 kupitia Gazeti Rasmi la Serikali la Januari 10,2022.

Akisoma wasifu wa Dkt. Ali Mohamed Shein,Kapteni Martin Alphonce Mabena alieleza kwamba Rais Mstaafu Dkt. Shein amezaliwa tarehe 13 Machi, 1948 huko Chokocho Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ambapo mnamo mwaka 1956 alianza masomo ya skuli ya msingi katika Skuli ya Msingi ya wanafunzi wa kiume ya Gulioni ambayo iliitwa Gulioni Boys Primary School Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa amesimama wakati ukipigwa wimbo wa Taifa wa Zanzibar, Tanzania na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika hafla ya kutunuku Nishani ya Mapinduzi kwa Rais wa Zanzibar Mstaafu wa Awamu ya Saba Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein,iliofanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Alieleza kuwa, mwaka 1965 hadi 1968 alipata masomo ya Sekondari katika Chuo cha Lumumba (Lumumba College Zanzibar). Dkt. Ali Mohamed Shein alianza masomo ya sekondari ya juu mnamo mwaka 1969 na kukamilisha mwaka 1970 katika chuo Kikuu cha Taifa kinachoitwa Vorenezh State University USSR.

Kapteni Mabena alieleza kuwa Dkt. Ali Mohamed Shein ni daktari kitaaluma, aliyehitimu katika fani ya Biokemia ya Utabibu kutoka Chuo kikuu cha Odessa nchini Urusi kati ya mwaka 1970 hadi 1975. Mnamo mwaka 1984 hadi 1988, alipata shahada ya uzamivu (Phd) ya fani kemikia na magonjwa ya binaadamu katika Chuo Kikuu cha Newcastle, Uingereza. 

Aidha, alieleza kuwa kati ya mwaka 1981 na 1994 alihudhuria programu mbalimbali za mafunzo, zilizofanyika ndani na nje ya nchi, zikiwemo Huduma za utoaji Damu na Uendeshaji wa Benki za Damu (Blood transfusion services and operation of blood Banks) yaliyofanyika Stockholm nchini Sweden na mwaka 1994 alipata mafunzo ya Uongozi (Management and situation leadership) mjini Dar es salaam Tanzania. 
Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Saba, Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein akiwa amesimama wakati ukipigwa wimbo wa Taifa wa Zanzibar,Tanzania na wa Afrika Mashariki katika hafla ya kutunuku kwa Nishani ya Mapinduzi na (kushoto kwake) Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu Balozi Seif Ali Iddi na Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Khamis Ramadha Abdalla.(Picha na Ikulu).

Alisema kuwa, mwaka huo huo alishiriki mafunzo ya masuala ya kupambana na VVU/UKIMWI katika nchi zinazoendelea (Planning for HIV/AIDs in Developing Countries) Mafunzo ambayo yalitolewa katika Chuo Kikuu cha East Anglia, Norwich nchini Uiengereza. 

Aliongeza kuwa, Dkt. Shein alianza kazi ya Ukarani katika Wizara ya Elimu Zanzibar Mei 1969 na baadae mwaka huo huo alipangiwa kazi ya Katibu Mkuu Msaidizi 'B' wa Wizara hiyo hiyo hadi Septemba 1969 alipoondoka kwenda USSR. Kati ya mwaka 1979 na 1984 alikuwa Mkuu wa Idara ya Huduma za Maabara ya Patholojia, Wizara ya Afya, Zanzibar. Aliporejea kutoka masomo ya Phd. mwaka wa 1989 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Patholojia katika Wizara ya Afya Zanzibar, ambapo alitumikia Idara hii hadi mwaka 1991. 

Aidha, alipata kuwa Meneja Programu wa Mpango wa Kudhibiti UKIMWI Zanzibar ndani ya Wizara ya Afya na Mshauri wa Kliniki ya Biokemia na Huduma za Uchunguzi kati ya 1991 na 1995.

Maisha yake ya kisiasa yalianza pale alipowania kiti cha Baraza la Wawakilishi kupitia Jimbo la Mkanyageni kisiwani Pemba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. 

Tarehe 29 Oktoba, 1995 aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya wa Zanzibar tarehe 13 Novemba, 1995. Tarehe 22 Novemba, 2000 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mambo ya Katiba na Utawala Bora.

Katika muendelezo wa shughuli za kisiasa, kwa maelezo ya Kampeni Mabena alisema kuwa Dkt. Shein aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 13 Julai 2001. 

Tarehe 17 Disemba, 2005 aliteuliwa kuwa mgombea mwenza katika Chama cha Mapinduzi CCM na hatimae kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuapishwa tarehe 21 Disemba 2005.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Saba Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein, baada ya kumtunuku Nishani ya Mapinduzi, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.

Aligombea Urais wa Zanzibar 2010 na kuchaguliwa kuwa Rais tarehe 31 Oktoba 2010. Aliapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 3 Novemba, 2010. 

Katika shughuli zake za kitaaluma, Dk. Shein amefanikiwa kuchapisha tasnifu za utafiti zipatazo mbili, ambazo ni Tasnifu ya utafiti alioufanya wakati akikamilisha masomo ya shahada ya uzamili na Tasnifu ya utafiti alioufanya wakati akikamilisha masomo ya shahada ya uzamivu. Aidha, amefanikiwa kuchapisha nyaraka mbalimbali za kitaalam. Dk. Shein alipata kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Pia, kwa mujibu wa maelezo ya Kapteni Mabena Rais Dkt. Shein ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Januari, mwaka 2021. Amepata kuwa mwanachama wa Vyama kadhaa vya Kitaalam ambapo Dk. Ali Mohamed Shein ameoa na ana Mke na Watoto. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news