NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itazingatia maslahi mapana ya wananchi katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa uwekezaji uliopangwa kufanyika katika eneo la Kizingo, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amesema hayo wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini, mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kufuatia kukamilika kwa ziara yake ya siku tatu ya Kiserikali aliyofanya katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilivyopo Zanzibar kuhusiana na ziara yake katika Nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa VIP Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar. (Picha na Ikulu).
Amesema, Serikali inatambua na kuthamini shughuli mbalimbali zinazofanywa na wananchi ikiwemo wavuvi katika eneo hilo la Kizingo, hivyo itahakikisha inazingatia namna bora ya kuliendeleza eneo hilo na kuwapatia wazawa maeneo ya michezo, ajira na mafunzo kutokana na mradi utakaowekezwa, sambamba na maeneo mengine ya visiwa ambako miradi mingine ya aina hiyo itafanyika.
Amesema, kupitia ziara hiyo kuna kampuni kubwa zilizoonyesha nia ya kuwekeza hapa nchini na kubainisha sekta tano zitakazofanyiwa kazi, ikiwemo ya ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ambayo inahusisha bandari tofauti, ikiwemo ya Mafuta na Gesi.
Kuhusiana na sekta ya Uvuvi, Dkt.Mwinyi alisema kuna wawekezaji watakaoanzisha viwanda vya kuchakata samaki, hatua itakayokwenda sambamba na harakati zinazofanywa na wananchi katika ufugaji wa samaki.
Pia alisema katika kuimarisha sekta ya Utalii, kuna wawekezaji watakaokuja kwa ajili kuanzisha ujenzi wa Kumbi za Mikutano, hatua itakayochochea ujio wa watalii na wageni mbalimbali hapa nchini.
Aidha, Dkt.Mwinyi alieleza kuwa mwekezaji anayewekeza katika mradi mkubwa wa Hoteli eneo la Kizingo, atakuwa na mradi mwingine wa ujenzi wa Hoteli kubwa ya Kitalii ya Nyota sita katika eneo la Matemwe, Mkoa Kaskazini Unguja, huku akibainisha utayari wa mwekezaji kuwekeza katika moja ya Visiwa vidogo viliyopo hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi alitumia fursa ya ziara hiyo kukumbushia ahadi zilizotolewa na Serikali ya Abu Dhabi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (awamu iliyopita), kuhusiana na ujenzi wa Hospitali ya Wete Pemba, ujenzi wa Barabara ya Fumba – Kisauni pamoja na Fedha za Uwezeshaji wa Vijana Dola Milioni 10, na Serikali hiyo kuhakikisha fedha hizo zitapatikana hivi karibuni.
Vile vile, alisema Serikali hiyo imekubali kurejesha safari za ndege zilizokuwa zikifanywa na Shirika la Ndege la Fly Dubai hadi Zanzibar, pamoja na safari za Ndege za Shirika la Emirates zilizokuwa zikifanyika hadi Dar es Salaam na kubainisha kuwa safari za shirika hilo hivi sasa zitafika hadi Zanzibar.
Amesema hatua hiyo imekuja baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuahidi kutumia njia bora na sahihi katika upimaji wa Ugonjwa wa UVIKO-19.
Rais Dkt.Mwinyi aligusia juu ya uendelezaji wa mji mpya katika eneo la Hoteli ya Bwawani, ambapo eneo la Hekta 260 litatumika, na kueleza kuwa kuna wawekezaji walionyesha nia ya kuja kuendeleza mazungumzo kati yao na Serikali kupitia mradi huo unaotarajiwa kuzalisha ajira kwa kiwango kikubwa.
Amesema, ana matumaini makubwa kuwa ziara hiyo itafungua milango ya Uwekezaji hapa Zanzibar na kusema tayari Serikali imetoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Ubalozi mdogo wa UAE hapa Zanzibar ili kurahisisha shughuli za uwekezaji wa miradi mbali mbali na shughuli za kidiplomasia.
Alisema, Serikali itaendelea kuwajengea mazingira bora wawekezaji, kwa kuhakikisha hawapati usumbufu au urasimu katika shughuli wanazofanya, sambamba na miradi inayoanzishwa kuhakikisha inazinufaisha pande zote mbili.
Katika ziara hiyo, ambapo Rais Dkt.Mwinyi aliondoka nchini Januari 16, 2022, pamoja na mambo mengine alishuhudia utiaji wa saini wa miradi mikubwa ya Uwekezaji kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya ‘Eagle Hills Regional Properties’ ya UAE.