NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane inalizingatia kundi la vijana kuwa ni kundi maalumu lenye changamoto ambazo ni wajibu wa serikali kuzitafutia ufumbuzi.
Vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wakiwa wamebeba picha za viongozi wakishiriki katika matembezi ya kuadhimisha sherehe za Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, baada ya kuzinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika uwanja wa Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba leo.(Picha na Ikulu).
Ameyasema hayo leo Januari 3,2022 katika uzinduzi wa matembezi ya Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mikoa yote ya Tanzania, katika uwanja wa mpira Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar matukufu ya Januari 12,1964. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi ambaye ni Mlezi wa Matembezi hayo ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kuadhimisha Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,baada ya kuyazindua leo katika uwanja wa mpira Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt. Mwinyi amesema, jitihada za Serikali ni pamoja na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi mbali mbali pamoja na kuboresha mafunzo ya ufundi wa fani tofauti kwa vijana wanaojiunga kwenye vyuo vya mafunzo ya amali.
Amesema, hatua nyingine ni vijana kujiunga na mabaraza ya vijana yaliyoanzishwa katika Wilaya zote za Unguja na Pemba ambayo shughuli zake zinasimamiwa na kuratibiwa na wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo.
Ameongeza kuwa, uwepo wa mabaraza hayo, ni jukwaa la kuwaunganisha vijana kubuni miradi ya kiuchumi na kuwapatia mitaji, taaluma na masoko ya kuuzia bidhaa zao. Hivyo ni matumaini yake kuwa mabaraza hayo yakiimarishwa vyema yatasaidia sana vijana kukabiliana na tatizo la ajira.
Mlezi wa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akizungumza na Vijana wa Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar wanaoshiriki Matembezi ya kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yaliyozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika uwanja wa Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba leo.(Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi amesema, ujenzi wa uchumi wa kisasa unaodhamiriwa kujengwa, unalengo la kuziendeleza jitihada za mafanikio ya awamu za uwongozi zilizotangulia, na kuelekeza nguvu ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi.
Amesema, licha ya changamoto zilizotokana na athari za UVIKO-19 lakini Zanzibar imeanza kupiga hatua za kwenda ambako nchi imedhamiria, hivyo ni wajibu wa wananchi wote kuunga mkono na kushirikiana na serikali katika kuyafikia malengo.
Amesema, uwajibikaji, uzalendo na ushirikiano ni mambo ya msingi yatayowawezesha Wazanzibar kupiga hatua zaidi za kimaendeleo, na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili ikiwemo tatizo la ajira kwa vijana.
"Mimi binafsi nimevutiwa sana na utaratibu huu wa kuwajumuisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kuwa pamoja katika masuala haya ya kuhamasishana uzalendo na umoja pamoja na kukumbushana masuala muhimu ya mustakbali wa taifa letu,"amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt.Abdalla Juma Mabodi akizungumza na vijana wa UVCCM kabla ya kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi, kuzungumza na vijana washiriki katika matembezi ya kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yaliozinduliwa katika viwanja vya Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba.(Picha na Ikulu).
Sambamba na hayo amesema, sote ni mashahidi wa kuwa nchi yetu imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika kipindi cha miaka 58 ya Mapinduzi tokea kufuzu kwa mapinduzi yaliyoongozwa na waasisi walioongozwa na jemedari Mzee Abeid Amani Karume.
Alieleza kwa jitihada zao viongozi waliotangulia pamoja na wananchi wa Kisiwa cha Unguja na Pemba, walifanya kazi kubwa ya kuijenga nchi yao na ndio hadi leo wananchi wanafurahia jitihada hizo hivyo alisema, ni wajibu wa kila mmoja kuziendeleza jitihada hizo kwa faida yao na kizazi kijacho.
"Nimepata faraja kuona hamasa kubwa walionayo washiriki wa matembezi haya kama hatua muhimu ya kuona kila mshiriki yupo tayati kuanza na kukamilisha matembezi hadi mwisho wake yatakapopokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"amesema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikmkabidhi picha ya Kiongozi Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume,Mshiriki wa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.Mhe.Asya Sharif, baada ya kuyazindua katika viwanja vya Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba leo 3-1-2022, kuaza matembezi hayo Kisiwani Pemba.(Picha na Ikulu).
Amesema kuwa, ni wajibu wa kila Mzanzibari kuyadumisha na kuyaendeleza matunda ya Mapinduzi katika kuimarisha uchumi wa kuwezesha hali ya kipato cha wananchi na ustawi wao kuendelea kuwa bora.
Aidha, amesema ni wajibu wa vijana kuendelea kuwa wazalendo, kudumisha amani, wachapakazi, watetezi wa amani umoja na mshikamano na walinzi wa mapinduzi matukufu ya Zanzibar na muungano wa Tanzania kwa nguvu zao zote.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi amesema, matembezi hayo ya UVCCM ni kielelezo thabiti cha kuonesha vijana wanalinda chama na Mapinduzi yao.
"Ni vigumu sana kufahamu uzito walioupata wazee wetu wakati wa mapinduzi lakini leo vijana hawa sio kwa nadharia bali kwa vitendo wameonesha namna gani wazee wetu walipigana kwa ajili ya uhuru wan chi zetu,"amesema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikmkabidhi Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mshiriki wa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,Abdalla Koti, baada ya kuyazindua katika viwanja vya Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba leo 3-1-2022, kuaza matembezi hayo Kisiwani Pemba.(Picha na Ikulu).
Kwa upande wake mlezi wa matembezi ya vijana wa UVCCM ambae pia ni Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Maryam Hussein Mwinyi alisema, matembezi hayo yanafaida kubwa kwa jamii na kuacha alama.
"Nikiwa mlezi wa matembezi haya nakushukuru sana mgeni rasmi kwa kutufungulia matembezi yetu nasema asante sana kwa niaba ya wote, nawapongeza sana vijana kwa uwamuzi wao wa kufanya matembezi kila mwaka kuuwezi muungano wetu," amesema.
Alieleza, safari hii vijana watakwenda kuitangaza na kuwaeleza vijana juu ya sera ya uchumi wa buluu kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane kupitia sera hiyo ambayo ni muhimu yenye lengo la kutatua suala la ajira kwa vijana.
Mapema akitoa taarifa ya matembezi hayo Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar,Mussa Haji Mussa alisema, vijana hao watatembea jumla ya km 124.9 ya mikoa yote ya Kisiwa cha Pemba.
Vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wakishangilia wakati wa Uzinduzi wa Matembezi ya kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, katika viwanja vya Konde wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia na kuyazindua kuaza matembezi hayo katika Mikoa ya Pemba leo.
Amesema, matembezi hayo ya siku tano yameanza rasmi mara baada ya kufunguliwa hadi kufikia kilele cha matembezi Januari 7 mwaka huu katika Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Matembezi hayo yamewashirikisha vijana wa CCM zaidi ya 700 ambao watapita katika maeneo mbalimbali kufikisha ujumbe kwa jamii kuhimiza uhai wa chama na jumuiya zake na kuunga mkono juhudi za Serikali ya kudumisha Mapinduzi ya mwaka 1964 yakiwa na kaulimbiu isemayo uchumi wa buluu ni fursa yetu vijana tuitumie.
Katika uzinduzi huo pia, Rais Dkt. Miwnyi alikabidhi picha za viongozi pamoja na bendera za Taifa kwa vijana watembeaji.