NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu waliofariki kutokana na ajali ya kuzama kwa boti huko Mkoa wa Kusini Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kusikitishwa na vifo hivyo na kuzisihi familia za marehemu hao kuwa na subira na ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha misiba hiyo.
Rais Dkt. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu awalaze Marehemu wote mahali pema peponi, Amin.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amewaombea kwa Mwenyezi Mungu wale wote waliopata madhara kufuatia tukio hilo kupona kwa haraka.
Ajali hiyo imetokea jioni ya Januari 4,2022 baada ya boti waliyokuwa wakisafiria wananchi hao kuelekea msibani huko Kisiwa Panza wakitokea Chake Chake Pemba kuzama, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Matar Zahor Masoud, vyombo vya uokozi bado vitaendelea na taratibu za kuwatafuta waliofariki ama wale walionusurika na ajali hiyo.