Rais Dkt.Mwinyi:Kufanya mazoezi ni kinga muhimu katika afya

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kufanya mazoezi ni kinga muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na sababu za mfumo wa maisha ya binadamu uliopo hivi sasa. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Marium Mwinyi (katikati) walipojumuika na viongozi na wanamichezo wa vikundi mbalimbali Bara na Zanzibar katika maadhimisho ya bonanza la Mazoezi ya Viungo Kitaifa kwa matembezi yaliyoanzia Michenzani hadi Uwanja wa Amaan. (Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi amesema hayo alipozungumza na wanamichezo katika Bonanza la 13 la mazoezi ya viungo lililofanyika Uwanja wa Amani jijini Zanzibar, ambapo kabla lilitanguliwa na matembezi kutoka Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge hadi Uwanjani hapo. 

Amesema wataalamu wa afya wamebainisha kuwa kufanya mazoezi ni jambo la msingi na lenye kusaidia sana katika kukabiliana na mfumo wa maisha uliopo, ambapo watu wengi wamepoteza utamaduni wa kutembea kwa miguu, kula vyakula vya asili, kutokupenda kunywa maji na badala yake kuegemea zaidi katika unywaji wa soda na juisi za viwandani. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi (katikati) wakiwapungia mikono wananchi leo walipojumuika na viongozi na wanamichezo wa vikundi mbalimbali Bara na Zanzibar katika maadhimisho ya bonanza la Mazoezi ya Viungo Kitaifa kwa matembezi yaliyoanzia Michenzani hadi Uwanja wa Amaan. 

Amesema hivi sasa wananchi wengi wamejikita katika matumizi ya muda mrefu wa simu janja, kompyuta na televisheni, sambamba na kuvuta hewa chafu pamoja na matumizi makubwa ya vipoza joto, mambo ambayo ni vigumu kuyaepuka katika mfumo wa sasa wa maisha. 

Amewahimizia wananchi ambao bado hawajawa na utaratibu wa kufanya mazoezi, kuanza mara moja kupitia mtu mmoja mmoja au kwa njia ya vikundi, pamoja na kuwahimiza Wakuu wa Vikundi hivyo vya mazoezi kuhakikisha utaratibu wa kufanya mazoezi unakuwa endelevu. 
Ameeleza kuwa, michezo ikiwemo ya vikundi vya mazoezi ina faida nyingi, miongoni mwake ni kuwaunganisha watu na kuwaleta pamoja na kushirikiana, mambo yanayohitajika katika jamii na Taifa kwa msingi kuwa huchangia kuwepo kwa amani na utulivu nchini na kuwa chachu katika kuleta maendeleo. 

Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali inakusudia bonaza hilo kufanyika Kisiwani Pemba mwaka ujao (2023) , na hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka wanamichezo hao kujiandaa. 

Amesema katika vikundi vya michezo, watu hupata fursa ya kuondoa msongo wa mawazo pamoja na kupata maarifa yanayowasaidia katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili. 
Amesema, wana Saikolojia wamebainisha kuwa kushiriki michezo husaidia sana kuchangamsha akili, kufikiri kwa haraka na kufikia maamuzi ya mambo mbalimbali, sambamba na kujiepusha kuingia katika makundi ya uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na udhalilishaji. 

Amesema amefurahishwa kuona kiwango cha washiriki wa Bonanza hilo kinazidi kuongezeka kwa watu wa jinsia zote na rika mbali mbali, licha ya kuwepo kwa athari za Ugonjwa wa Uviko – 19. 
Wanamichezo wakishiriki Bonanza la Mazoezi ya Viungo leo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi.

Katika bonanza hilo Rais Dk. Mwinyi pamoja na kupokea maandamano ya Vikundi vya Wanamichezo wa Viungo,pia alipata fursa ya kutoa vyeti kwa washiriki 

Nae, Waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema mazoezi hayo ya viungo ni mpango wa utekelezaji wa Sera ya Mchezo pamoja na Ilani ya CCM (2020-2025) , zenye azma ya kuwahamasisha wananchi kushiriki katika michezo. 
Alisema wastani wa wananchi 10,000 walishiriki katika Bonanza hilo, likiwa na lengo la kuimarisha afya, sambamba na kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa jamii. 

Aidha, alisema kumekuwepo ongezeko la wananchi wanaofanya mazoezi nchini kwa azma ya kulinda afya zao, hivyo akatumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwahamasisha wananchi kushirki katika mazoezi. 

Waziri Mwita alieleza kuwa Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa katika kusimamia na kuimarisha michezo, ikiwemo utatuzi wa migogoro inayovikabili Vyama vya Michezo. 
Mapema, Kamishna wa Michezo Ameir Mohamed alisema Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Wizara Afya na Ustawim wa Jamii Tanzania Bara pamoja na Shirika la Afya Duniani WHO) zimeandaa muongozo wa kitaifa utakaotumika kama Dira na kubainisha namna ya kufanya mazoezi kitaalamu, kwa wananchi wa rika na hali (maumbile) tofauti. 

Alisema wadau hao wana azma ya kusambaza nakala 200 za muongozo huo , ili kuwafikia wanachi nchini. 
Aliiomba Serikali kuridhia Wizara za Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutenga Bajeti ili kufanikisha suala hilo. 

Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanya mazoezi ya Viungo (ZABESA) Said Suleiman akigusia kauli mbiu ya Bonanza hilo isemayo ‘Afya bora ni mtaji , pata chanjo, jiepushe na Corona’ , alisisitiza umuhimu wa wananchi ambao hadi sasa hawajapata Chanjo ya Ugonjwa wa Uviko – 19, kuchukua hatua za kuchanja. 
Vile vile, kupitia Risala ya Vikundi hivyo vya mazoezi, ulivishukuru vikundi vyote vilivyoshirki katika Bonanza hilo kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, huku ikisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa utakapofika, baadae mwaka huu. 

Jumla ya Vikundi 127 vya mazoezi ya viungo 127 kutoka Mikoa yote ya Zanzibar na baadhi ya Mikoa ya Tanzania Bara, ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa na Mbeya vilishiriki katika Bonanza hilo. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news