NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha wanasiasa kuwa makini na kauli wanazotoa kwa wananchi, pamoja na kuhakikisha Sera za Vyama vyao vinazingatia umuhimu wa kuwaunganisha Watanzania badala ya kuwafarakanisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dkt. Khalid Salum Mohamed na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Tanznia, Mhe.Jaji Francis S. Mutungi pamoja na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar, Bw.Mohamed Ali Ahmed wakati alipowasili katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki katika Uzinduzi wa Kikosi kazi kitakachopitia Hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa.(Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi ametoa ukumbusho huo katika uzinduzi wa Kikosi Kazi cha kuchakata hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip - Airport Zanzibar leo Januari 10,2022.
Amesema, masuala ya kisiasa yanagusa hisia za wananchi kwa namna mbalimbali, huku wananchi hao wakipokea matamko na kauli za wanasiasa kwa upeo na uwono tofauti, hivyo ni jukumu la wanasiasa kuwa makini na kauli wanazotoa pamoja na vitendo vyao ndani ya jamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (mbele) akifuatana na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Tanznia Mhe.Jaji Francis S. Mutungi wakati alipowasili katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki katika Uzinduzi wa Kikosi kazi kitakachopitia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
Amesema,wajumbe wa kikosi kazi walioteuliwa wana wajibu wa kutumia hekima, busara, uzalendo na uzoefu katika uchambuzi watakaoufanya na kuepuka hoja zitakazobainika zinaweza kuleta migongano au kuwa kikwazo cha maendeleo.
Aidha, aliwataka wajumbe hao kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kufanya kwa kazi kuzingatia maadili na kanuni zinazowaongoza kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Baadhi ya wajumbe wa Kikosi kazi kitakachopitia hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa wakisimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa kabla Uzinduzi wa Kikosi hicho uliofanywa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki Nje ya Jiji la Zanzibar.
“Msilazimishe hoja kwa kulinda na kutetea sera na maslahi ya vyama vyenu.Demokrasia itawale wakati wa kufanya maamuzi mazito ambayo mmetofautiana kimawazo na mitazamo,"amesema.
Dkt. Mwinyi, amesema mchakato wa hoja hauna budi ulenge katika kuendeleza siasa zenye lengo la kuzidi kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha misingi ya usawa, umoja na mshikamano.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) pamoja na viongozi wengine akiwepo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Othman Masoud Othman (wa pili kulia) wakisimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa kabla Uzinduzi wa Kikosi Kazi kitakachopitia Hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa hafla ilyofanyika leo katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki Nje ya Jiji la Zanzibar.
Aliahidi Serikali zote mbili (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika katika kutekeleza na kukamilisha majukumu ya kikosi hicho.
Alieleza kufurahishwa kwake na wajumbe walioteuliwa, wakiwemo wataalamu wabobezi katika masuala ya uongozi, usuluhishi wa migogoro, utawala bora na haki za binadamu pamoja na masuala mbalimbali ya kisheria, huku akibainisha imani yake kuwa maamuzi yatakayopitishwa yatakuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Baadhi ya wajumbe wa Kikosi kazi kitakachopitia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa wakiwa katika hafla ya Uzinduzi wa Kikosi hicho uliofanywa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki Nje ya Jiji la Zanzibar.
Amesema, wajumbe hao kuelewa kazi waliyokabidhiwa ni yenye maslahi mapana kwa Taifa, hivyo ni vyema wakatekeleza majukumu yao kwa umahiri na umakini mkubwa ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
Nae, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman alisema kuundwa kwa kikosi hicho ni uwekezaji mkubwa katika mustakbali mwema wa nchi na hivyo akawataka wananchi kuthamin hatua hiyo, sambamba na kupongeza ushirikishaji wa wajumbe kutoka makundi tofauti.
Mwenyekiti wa Kikosi kazi Prof.Rwekeza S.Mukandara alipokuwa akitoa shukurani zake katika hafla ya uzinduzi wa Kikosi kazi kitakachopitia hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa uliofanyika leo katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki Nje ya Jiji la Zanzibar mgeni rasmi alikuwa RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi .
Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Tanznia Mhe.Jaji Francis S. Mutungi alipokuwa akitoa maelezo na kuwatambulisha wajumbe wa Kikosi kazi kitakachopitia Hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa wakati wa Uzinduzi rasmi uliofanywa na RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) leo katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesaki Nje ya Jiji la Zanzibar.
Aidha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohamed alimshukuru Rais wa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuliongoza Taifa kwa weledi na dhamira ya kujenga umoja na mshikamano na kutaka ari iliyoonyeshwa na viongozi hao kuteremka hadi ngazi za chini.
Dk. Khalid alipongeza uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo na kusema ana imani kubwa watakwenda kufanyakazi kwa weledi na kuzingatia maslahi mapana ya taifa.
Waalikwa wa vyama vya siasa katika Uzinduzi wa Kikosi kazi kitakachopitia Hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa wakifuatilia kwa makini wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alipotoa hutuba yake katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesaki Nje ya Jiji la Zanzibar .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) alipokuwa akitoa hutuba yake katika hafla ya Uzinduzi wa Kikosi kazi kitakachopitia Hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesaki Nje ya Jiji la Zanzibar.
Mapema, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi, Profesa Rwekaza Mukandara alitoa shukurani kwa Marais wa serikali zote mbili kwa dhamira ya kuzitafutia suluhisho changamoto mbali mbali za kisiasa zinazokabili Taifa na akatumia fursa hiyo; kutoa ahadi ya wajumbe kukubali uteuzi huo huku wakifahamu jukumu kubwa lilioko mbele yao.
Kikosi Kazi cha kuchakata Hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa Wadau wa Demokrasia ya Siasa za Vyama vingi uliofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma, kinaundwa na Wajumbe 25, chini ya Uenyekiti wa Profesa Rwekaza Mukandara na Makamo Mwenyekiti wake Hamad Rashid Mohamed.