RC Kunenge ang'aka, asema ole wao wazazi watakaowapeleka watoto kuchunga ng'ombe

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka watendaji waliopo mkoani humo kuhakikisha watoto wote wanaostahili kuanza shule Januari 17,mwaka huu waripoti katika shule walizopangiwa ili kutimiza azima ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya elimu nchini.
Aidha,Kunenge amewapiga marufuku wazazi wenye tabia ya kuwapeleka watoto wao kuchunga ng'ombe kuwa waache vitendo hivyo mara moja kwa kuwa Serikali imejenga miundombinu mizuri ili watoto wa kitanzania wapate haki ya kusoma.

Kunenge ametoa kauli hiyo wilayani Mkuranga alipofanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa miradi ya elimu iliyojengwa kwa fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia miradi ya 5441 TCRP.

Amesema,Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutafuta fedha na hatimae akafanikiwa kupata fedha za mkopo zisizo na riba akiwa na lengo la kujenga miundombinu ya elimu na afya.

Amesema,baada ya kupatikana kwa fedha hizo,Mkoa wa Pwani umenufaika kwa kupata bilioni 13.39 na kati ya hizo sh.bilioni 10.9 zimekwenda katika ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza na madarasa shikizi.

Kunenge amesema kuwa, Mkoa wa Pwani umefanikiwa kujenga madarasa 535 yakiwemo madarasa ya sekondari kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 422 na madarasa shikizi 133 lakini madarasa Sita ya Shule Shikizi yatakamilika hivi karibuni.
Amesema kuwa,jumla ya wanafunzi 32,399 wataanza masomo Januari 17, mwaka huu kwa hiyo lazima watoto wote waende shule ili kusudi Rais apate moyo wa kuendelea kutafuta fedha nyingine kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa faida ya nchi na wananchi wake.

"Mkoa wetu umekamilisha ujenzi wa madarasa yote kwa asilimia 99 isipokuwa yamebaki madarasa Shikizi Sita ambayo yatakamilika muda mfupi ujao na hii ni kazi nzuri ya Rais Samia ambayo inapaswa kuungwa mkono," amesema Kunenge.

"Nampongeza Rais kwa kutafuta fedha hizi za mkopo usio na riba na namuomba akipata mkopo mwingine azidi kuuangalia Mkoa wa Pwani, lakini sote tunajua fedha hizi zimewekwa wazi na hapakuwa na usiri wowote,kwa hiyo niwaombe madiwani na watendaji toeni elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya fedha hizo,"amesema.

Katika ziara hiyo Kunenge alikagua Shule ya Msingi Jamhuri iliyopo Kata ya Vikindu iliyojengwa madarasa sita pamoja na Shule ya Sekondari Dundani iliyopo Kata ya Mkuranga ambapo kwa pamoja zimejengwa kwa fedha za mradi wa 5441 TCRP.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ally amesema kuwa kuna kila sababu ya kumpongeza Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kuwa, amekuwa mkombozi mkubwa wa wananchi wa Wilaya ya Mkuranga na kwamba lazima wananchi wafahamu juhudi hizi za Rais.

Khadija, amesema kuwa Wilaya ya Mkuranga ndio Wilaya pekee ya Mkoa wa Pwani zilizofaidika kwa kujenga madarasa mengi ambapo imejenga madarasa 151 yatakayokwenda kutumika na wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari.

"Nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa upendo mkubwa aliohuonyesha kwa Watanzania kwa kuwatafutia fedha za kujenga madarasa hapa Mkuranga na nchi nzima kwahiyo ni vizuri tukamuunga mkono kwa juhudi hizi ,"amesema.

Hatah hivyo, Khadija amesema atahakikisha watoto wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka wanafuatiliwa kwa ukaribu ili waweze kusoma kama ambavyo Serikali ilivyokusudia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news