RC Kunenge awapigia wakulima chapuo katika Kiwanda cha Sayona Fruits Limited

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amekitaka Kiwanda cha Sayona Fruits Limited kuelimisha wakulima aina ya matunda yanayotakiwa kuzalishwa ili waweze kufaidika na fursa ya uwepo wa kiwanda hicho.
Kunenge ametoa wito huo alipotembelea kiwandani hapo Januari 28,2022 ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake ya kutembelea viwanda vikubwa vilivyopo mkoani humo kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili.

Kunenge amesema, uwepo wa kiwanda hicho ni fursa kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani hususani wakulima lakini ili waweze kufaidika ni lazima waelimishwe kulima matunda ambayo yanahitajika na kiwanda.

Amesema kuwa,hakuna haja ya wakulima kulima matunda au mazao ambayo hayana faida kwako lakini inawezekana wakipata elimu ya kutosha watabadilika na kulima matunda yenye maslahi ambayo yatanunuliwa na kiwanda hicho.
"Kiwanda hiki ni kikubwa lazima nitoe pongezi kwa mwekezaji Subhash Patel ambaye kwasasa ni marehemu lakini tunapaswa kurudi kwa wakulima wetu kuwaelimisha namna ya kulima mazao ambayo soko lake lipo hapa,"amesema Kunenge

Kunenge ,ameongeza kuwa kama wakulima wataelimishwa ni wazi kuwa watafaidika na hivyo kukua kiuchumi ambao utasaidia familia zao na hata Taifa kiujumla.

Kunenge,amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan mara zote anawapigania wawekezaji lakini anapenda kuona pia hata wananchi wake wananufaika na uwepo wa viwanda hivyo .

"Rais wetu ni msikivu na anafanyakazi kubwa,lakini anawathamini wawekezaji kwahiyo kama kuna haja ya kubadilisha baadhi ya sera semeni tushughulike kwakuwa hiyo ndio kazi yetu kwani tunataka muwe katika mazingira rafiki,"amesema
Amesema,anafahamu changamoto ya maji katika kiwanda hicho na kwamba muda si mrefu maji yatakuwa yakutosha kwakuwa mradi mkubwa wa maji kutoka Rufiji utaanza kutelezwa hivi karibuni na mkandarasi amepatikana.

Kwa upande wake Afisa Rasilimali Watu wa kiwanda hicho, Godlove Mngwamba amemueleza mkuu huyo wa mkoa kuwa kiwanda hicho kimegharimu dola za Kimarekani milioni 55.5 huku milioni 500 zikitumika kuwema maji na kutengeneza barabara ya kufika kiwandani hapo.

Mngwamba amesema, kwa sasa kiwanda hicho kinazalisha tani 18 za matunda kwa siku lakini uwezo wake ni kuzalisha tani 280 na kwamba kwa wiki kinazalisha tani 150.

Kuhusu ajira Mngwamba amesema kiwanda kimeajiri wafanyakazi wa ajira za kudumu 146 huku wafanyakazi wa muda 135 na raia wa kigeni 14 ambapo hata hivyo zaidi ya wakulima 30,000 wananufaika na kiwanda.
Amesema, kiwanda kimekuwa msaada kwa jamii kwakuwa mbali na kutoa ajira lakini wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ikiwemo kujenga maabara na kununua vifaa tiba na kujenga nyumba ya mganga katika Zahanati ya Kijiji cha Mboga.

Hata hivyo, Mngwamba amemshukuru Mkuu wa Mkoa pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wawekezaji huku akiomba Serikali iwasaidie kutatua changamoto ya maji inayokikabili kiwanda hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news