NA ROTARY HAULE
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka wawekezaji wa viwanda waliopo ndani ya mkoa wake kuhakikisha wanatoa huduma za jamii kwa wananchi wanaoishi pembeni ya viwanda hivyo ili waone umuhimu wa uwekezaji wao.
Kunenge,ametoa kauli hiyo Januari 27,2022 wakati alipotembelea kiwanda cha Prance International Trade Co LTD kilichopo eneo la Saeni Kata ya Misugusugu Kibaha Mjini kinachozalisha vifaa vya ujenzi ikiwemo misumari,waya aina zote,sabuni ya Nice One na taulo za watoto.
Amesema kuwa, Serikali hapa nchini inawapenda wawekezaji kwa kuwa wanaleta faida ya ajira na mapato ya Taifa, lakini wakumbuke pale walipojenga viwanda lazima wakumbuke kutoa huduma za jamii kwa wananchi.
"Niwaombe wawekezaji mkumbuke kutoa huduma ya jamii kwa wananchi waliowazunguka ili kusudi waone umuhimu wa kuwepo kwa viwanda hivi katika maeneo yao maana kama mtakuwa hamuwajali wananchi ni wazi kuwa watashindwa kuwapa ushirikiano,"amesema Kunenge.
Aidha Kunenge,amekipongeza kiwanda hicho kwa kujitoa katika kusaidia jamii na kwamba tayari wameonyesha mfano wa kuchangia saruji mifuko 400 kwa ajili ya kuchangia ujenzi Zahanati ya Mtaa wa Saeni.
Amesema kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa kipaumbele kwa wawekezaji waliopo nchini ndio maana anajitahidi kuweka mazingira rafiki na kwamba wanapojitoa katika jamii inakuwa faraja kwake.
"Kuna huduma mnaweza kutoa katika jamii yenu kama vile kujenga Shule, kuchangia ujenzi wa Zahanati na mambo mengine mengi na endapo mtafanya haya wananchi watawapenda na watakuwa mabalozi wazuri wa kuhakikisha muda wote mali zenu zinakuwa salama," amesema Kunenge.
Kunenge,amewataka wawekezaji hao kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sera na Sheria za nchi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima baina ya Serikali, Taasisi ,wananchi kwa kuwa nchi bado inawahitaji kwa kiasi kikubwa wawekezaji.
Kwa upande wake Afisa Uajiri wa kiwanda hicho, Noel Mwasajone ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji huku akiomba changamoto ya umeme na barabara zifanyiwe kazi.
Mwasajone amesema, kiwanda hicho kilijengwa mwaka 2019 na kimekuwa kikifanya vizuri kwa kuwa kinazalisha bidhaa bora kupitia Watanzania wanaofanya kazi kiwandani hapo.
Amesema kuwa,mpaka sasa kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi wa Kitanzania 397 wakiwemo Wanaume 324 na Wanawake 73 huku raia wa kigeni ni 17 pekee.
Aidha, Mwasajone amewaomba Watanzania kujitokeza kukitumia kiwanda hicho kwa kuomba ajira na hata kutumia bidhaa zake kwakuwa uzalishaji wake umewalenga zaidi Watanzania.
Hatahivyo, Mwasajone amepongeza hatua ya Mkuu huyo wa Mkoa kwa kutembelea kiwandani hapo kwakuwa ameonyesha nia ya kutaka kuwasaidia wawekezaji huku akiomba ziara hizo ziwe za mara kwa mara kwakuwa zinasaidia kuwatia moyo wawekezaji.