RC Kunenge azikunjulia makucha taasisi zinazowawekea vikwazo wawekezaji

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amezitaka taasisi za Serikali zinazoshughulika na masuala ya uwekezaji kuacha kuwawekea vikwazo wawekezaji hao na badala yake ziwasaidie kutatua changamoto zinazowakabili.
Kunenge ametoa kauli hiyo Januari 28,2022 wakati akiwa katika ziara yake ya kutembelea viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya Hill Group vilivyopo Mapinga Bagamoyo mkoani Pwani.

Hill Group ni kampuni inayomilikiwa na Mtanzania, Hillal Shoo ambapo kwa ujumla wake kampuni hiyo inamiliki kiwanda cha kuzalisha maji ya Hill,kiwanda cha vifungashio pamoja na kiwanda cha vyakula vya kuku.

Akiwa kiwandani hapo Kunenge,ameeleza kufurahishwa na teknolojia inayotumika kiwandani hapo hususani ile ya kuzalisha maji ambapo amesema mwekezaji wa namna hiyo anapaswa kuungwa mkono.

Amesema kuwa, mwekezaji huyo anapaswa kuungwa mkono kwakuwa amekuwa na msaada kwa Taifa lake hasa katika kutengeneza ajira kwa Watanzania hususani vijana wa kutoka Bagamoyo lakini ni sehemu pia ya mapato ya Wilaya,Mkoa na Taifa.
Amesema,Rais wa Awamu ya Sita,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameweka mkazo na msisitizo kwa wasaidizi wake juu ya kuwasaidia wawekezaji, lakini wapo baadhi ya watu na taasisi zinakwamisha juhudi zake.

Amesema,kama itabainika kuna mtu au taasisi yoyote inaleta vikwazo kwa mwekezaji basi mtu huyo atakuwa matatani kwa kuwa Serikali haitamvumilia kwa kuwa atakuwa analeta hujuma dhidi ya Rais.

"Nimekuja hapa nimeona hiki kiwanda, lakini nimefurahi sana na huu uwekezaji mkubwa uliopo hapa,lakini kikubwa zaidi nimependezwa kuona teknolojia mpya na yakisasa inayotumika kuzalisha maji haya ya Hill,"amesema Kunenge.

Amesema, uwekezaji huo ndio unatakiwa ndio maana Rais Samia ametoa kipaumbele kwa wawekezaji kwa kuwawekea mazingira bora na hata kuwaondolea vikwazo visivyo na msingi.

Amesema, kazi ya Serikali ni kuwasaidia wawekezaji wake ili Serikali hipate na mwekezaji hapate ambapo kwakufanya hivyo itakuwa ni njia sahihi ya kuleta maendeleo hapa nchini.

Aidha, Kunenge ameongeza kuwa ziara yake ya kutembelea viwanda hivyo inania njema ya kuvikagua na kujua changamoto zinazowakabili pamoja na kueneza ujumbe wa Rais wenye nia njema kwa wawekezaji.
"Napita kuleta salamu za Rais Samia,Rais ameeleza nia ya kuufungua Mkoa wa Pwani kwa kuwa ni mkoa ambao unaongoza kwa viwanda, hivyo amewatoa wasiwasi juu ya changamoto zinazowakabili kwa kuwa zinafanyiwa kazi,"amesema.

Amesema kuwa, miongoni mwa changamoto ambazo Rais anazofanyia kazi ni pamoja na ukosefu wa maji kwa wawekezaji ambapo kwa sasa tayari changamoto hiyo inakwenda kwisha muda mfupi ujao.

"Rais ameanza kuchukua hatua ya kutatua kero ya maji kwa wawekezaji kwani tayari mkataba umesainiwa na mkandarasi kwa ajili ya kutoa maji katika mradi wa Rufiji na kusambaza katika Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, mradi ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 750 kwa siku,"amesema Kunenge.

Kuhusu,umeme Kunenge amesema changamoto ya umeme kwa Mkoa wa Pwani itakwenda kuwa historia kwa kuwa Mkoa wa Pwani umepata bahati kubwa kupitia mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere wilayani Rufiji.

Amesema,mradi huo ukikamilika utakuwa na kituo kikubwa(Substation) eneo la Chalinze ambacho kitakuwa kinasambaza umeme katika maeneo ya Chalinze na Bagamoyo umeme ambao utakuwa wa kutosha hivyo na kuweza kuondoa kero kwa wawekezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hill Group, Hillal Shoo, amemshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na anaamini changamoto zake zinakwenda kuisha.

Shoo amesema, changamoto kubwa kiwandani hapo ni suala la umeme kwani unapokatika au kuwa chini ya kiwango mitambo inasimama kufanya uzalishaji na hivyo kupunguza mahitaji katika jamii na hata kuwepo hasara katika kiwanda.

Amesema,kutokana na ujumbe uliotolewa na Mkuu wa Mkoa amemletea faraja na hivyo kumshukuru Rais huku akimpongeza Mkuu huyo kwa kutembelea kiwandani hapo kwani inaonyesha jinsi ambavyo Serikali inawajali.

Hata hivyo,Shoo amesema kiwanda chake kinazalisha maji Safi na Salama yaliyotengenezwa kwa kuzingatia viwango bora ,aina mbalimbali ya vifungashio pamoja kuzalisha vyakula vya kuku ambapo amewaomba Watanzania waunge mkono kwa kununua bidhaa hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news