NA ROTARY HAULE
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameanza ziara ya kukagua viwanda mbalimbali vilivyopo mkoani humo huku akiahidi kushughulikia changamoto ya umeme inayowakabili baadhi ya wawekezaji wa viwanda hivyo.
Amesema,lazima
wawekezaji wapate huduma ya umeme wa kutosha ambao utawasaidia katika
kuendeleza uzalishaji wa bidhaa kwenye viwanda vyao kwa kuwa bila umeme
hakuna uzalishaji.
Kunenge
ametoa kauli hiyo leo katika ziara yake ya kutembelea viwanda vya
Kampuni ya Lake vilivyopo Mjini Kibaha vinavyoshughulika na utengenezaji
wa bidhaa mbalimbali.
Kunenge
ameanza ziara hiyo kwa kutembelea kiwanda cha Aluminum Trailers Limited
kinachotengeneza matenki ya kuhifadhia na kubebea mafuta, kiwanda cha
mitungi ya gesi,matenki ya maji,bomba za plastiki,nondo na kiwanda cha
Gypsum.
Aidha,katika
ziara hiyo Kunenge alipokea changamoto ya kuwepo kwa umeme hafifu
kutoka kwa wawekezaji hao wakieleza kuwa mara nyingi wanashindwa
kuzalisha kutokana na umeme kuwa mdogo.
Kutokana
na hali hiyo, Kunenge amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais
Samia Suluhu Hassan inawajali wawekezaji kwa kuwa ndio chanzo cha mapato
ya Taifa na hata ajira kwa Watanzania.
Amesema,suala
la umeme tayari Serikali kwa kushirikiana na TANESCO wanaifanyia kazi
changamoto hiyo na muda si mrefu ufumbuzi wake utapatikana na viwanda
vitafanya uzalishaji kama ilivyokusudiwa.
"Binafsi
niwapongeze kwa uwekezaji huu mkubwa katika mkoa wetu maana nimejionea
kazi kubwa mnayofanya,na kazi hii inaleta tija katika Taifa letu ikiwemo
ajira na hata kuongeza pato la nchi kwa hiyo niseme tu Serikali ipo
pamoja nawe,"amesema Kunenge.
Amesema,
uwekezaji uliofanywa na wawekezaji wa Kampuni ya Lake unatafsiri nia ya
Serikali na inaonyesha Rais jinsi anavyofanyakazi na kwamba lazima
wawekezaji hao wawekewe mazingira mazuri ya uzalishaji.
"Nimepita
katika kiwanda hiki cha Lake Steel nimeona wanatengeneza nondo aina ya
BS inayoendana na kiwango cha kimataifa na miradi mikubwa inayotekelezwa
nchini nondo zote zimetoka hapa, kwa hiyo lazima tuwaunge mkono
wawekezaji hawa,"amesema.
Amesema,kazi
ya Serikali ni kutengeneza mazingira bora zaidi ili wawekezaji wapate
kipato lakini hata Watanzania nao wapate ajira ndio Rais Samia
anaendelea kusisitiza namna ya kuwajali wawekezaji waliopo nchini.
Kuhusu
changamoto ya umeme, Kunenge amesema kuwa Serikali inafanya jitihada
kubwa ili umeme huwe wa kutosha na kusababisha uwekezaji huwe bora zaidi
huku akiwaomba kuwa na imani na Serikali yao.
Kunenge amewaomba Watanzania kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji hao kwa kuhakikisha wananunua bidhaa zinazozalishwa na wawekezaji wa ndani ili kusudi wapate moyo wa kuzalisha zaidi.
Hata hivyo, Kunenge ametoa wito kwa taasisi za Serikali zilizopo ndani ya mkoa wake kuhakikisha wanaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji huku wawekezaji wafuate sheria za Serikali kwa kuwa kufanya hivyo itawafanya kuongeza mapato.
Afisa rasilimali watu wa kiwanda cha Aluminum Trailers Limited, Hussein Ally amesema kuwa, kiwanda chao kinazalisha tenki 15 kwa mwezi huku wakitoa ajira kwa Watanzania 90.
Ally ameishukuru Serikali kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji wa Tanzania na huku akiomba Serikali ifanyie kazi changamoto zao ikiwemo umeme.
Naye Fadhili Msemwa,Afisa Uajiri wa kampuni ya Lake Group amesema, kampuni yake mpaka sasa imeajiri watu 400 ambapo hata hivyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara hiyo kiwandani hapo na kuomba ziara hizo ziwe za mara kwa mara ili kuwapa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili na baadae zifanyiwe kazi na Serikali.