RC PWANI ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI,ATAKA FAMILIA ITAKAYOWAOZESHA WATOTO WA KIKE WAKAMATWE HARAKA

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewaagiza viongozi wa halmashauri wakiwemo wakurugenzi na wakuu wa wilaya kuhakikisha wanachukua hatua kali za kisheria dhidi ya familia itakayobainika kushiriki vitendo vya kuwaozesha watoto wa kike wanaopaswa kwenda shule Januari 17, mwaka huu.

Kunenge ametoa agizo hilo leo Januari 9,2022 katika ziara yake aliyoifanya Wilayani Kibiti na Mkuranga ikiwa ni sehemu ya kukagua miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yaliyojengwa kwa fedha za maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika ziara hiyo Kunenge ameambatana na kamati yake ya Ulinzi na Usalama ambapo akiwa wilayani Kibiti alikagua Shule ya Sekondari Mtawanya iliyopo Kata ya Mtawanya,Shule Shikizi ya Nyambangala iliyopo Kata ya Dimani huku katika Wilayani ya Mkuranga akitembelea Shule ya Sekondari Kiparang'anda.

Kunenge amesema, Rais Samia ametambua changamoto za kielimu pamoja na kero mbalimbali katika sekta hiyo ndio maana aliona aanze na kipaumbele cha kujenga shule bora mkoani humo ili kuwakomboa watoto katika elimu.
Amesema kuwa, Rais amefanya kazi kubwa ya kukopa fedha zenye riba nafuu kwa ajili ya kuhakikisha Shule zinajengwa na watoto wanakwenda shule ili wapate elimu bora.

Amesema kuwa,nguvu alizozionyesha Rais Samia lazima zizae matunda kwa kuhakikisha watoto wote wanaostahili kwenda shule wanakwenda Shule kwa wakati ili wamtie moyo wa kuendelea kusaidia katika changamoto nyingine.

Kunenge ameongeza kuwa, mtoto yoyote akikutwa Mtaani hajaenda shule au hajaandikishwa ni lazima wazazi ,ndugu wa familia, viongozi chama na wa Serikali wa eneo husika wakamatwe na wachukuliwe hatua maramoja moja kwakuwa watakuwa hawatoshi.

"Akina mama pelekeni watoto wa kike shuleni ndoa zipo na mtazikuta baadae ,watoto wakisomeshwa vizuri,afya zao zikiwa vizuri watakuja kuwasaidia kutatua changamoto katika familia,"amesema Kunenge.
"Kwanza nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya jambo kubwa la kuwapa watoto maisha kupitia elimu na ni wazi kuwa Mheshimiwa Rais ameona atekeleze hilo kwa faida ya Watanzania na hiyo ni ibada kwake," amesema Kunenge.

Kunenge,ameongeza kuwa kazi kubwa aliyoifanya Rais sio mwisho kwani ataendelea kuifanya lakini wawakilishi wake wanawajibu wa kuhakikisha wanajituma kusimamia yale yote yanaanzishwa na Rais kwa maendeleo ya Taifa.

Amesema, Serikali inatoa elimu bila malipo kwa ustawi wa Taifa lakini hakuna sababu ya watoto kubaki nyumbani hivyo lazima tumuunge mkono Rais kwa kazi anayoifanya huku akisema Rais kazi yake ameifanya na kazi iliyobaki ni wajibu wa wawakilishi wa Rais.
"Serikali inatoa elimu bila malipo,kwahiyo hakuna sababu ya watoto kukaa nyumbani lakini lazima tujue Rais Samia amefanyakazi yake vizuri na imebaki kwetu kuendelea kutimiza wajibu wetu naomba tumsaidie kiongozi wetu ili hapate moyo wa kututafutia fedha nyingine,"amesema Kunenge

Amesema,Rais anataka kuona matunda mazuri ya kazi aliyofanya na kinachotakiwa ni kumsaidia kujibu maneno ya watu kwa kueleza matokeo ya fedha alizokopa ili kupunguza maneno yasiyofaa yanayotolewa na watu.

"Mheshimiwa Rais ametoa kipaumbele cha elimu kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania na sasa ni muhimu sana kuhakikisha elimu inayotolewa iendane na majengo haya mazuri na matokeo yakiwa mazuri itakuwa faraja kwa mama Samia,"ameongeza Kunenge.

Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Magogo matatu katika Kata ya Mtawanya Wilayani Kibiti Hamza Bakari , amesema kuwa juhudi za Rais zinapaswa kuungwa mkono kwakuwa kazi aliyofanya ya kuleta fedha za kujenga vyumba vya madarasa ni mkombozi kwa watoto wa Kitanzania.

Bakari amesema awali wanafunzi wa Kitongoji chake walikuwa wanasafiri umbali wa kilomita nne kwa ajili ya kufuata elimu Shule nyingine lakini kwasasa changamoto hiyo imekomeshwa.

Hata hivyo,Msikwa Isale amesema shukrani yake anaitoa kwa Rais kutokana na juhudi zake huku akimuahidi Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuwa watashirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wakike wanakwenda kama ambvyo Serikali imeelekeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news