NA ROTARY HAULE
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewapiga marufuku walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kuacha tabia ya kuwazuia wanafunzi kuingia darasani kwa kisingizio cha kukosa michango.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo Januari 19, 2022 wakati alipokuwa akizungumza na walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maendeleo na Shule ya Sekondari Bundikani zilizopo Kata ya Mailimoja Kibaha Mjini.
Katika ziara hiyo
Kunenge amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefanyakazi kubwa ya kutafuta fedha na
hatimaye kufanikiwa kujenga madarasa na kwamba hakuna ruhusa kwa walimu
kuzuia wanafunzi kwasababu ya michango.
"Nataka kuona
wanafunzi wote wanaingia darasani kusoma na hii tabia ya kuwazuia
wanafunzi wasiingie darasani kwasababu ya kukosa michango isiwepo na
sipendi kusikia katika Shule yoyote ndani ya Mkoa wangu,"amesema
Kunenge.
Kunenge amesema kuwa, ikitokea shule mwanafunzi
amefukuzwa kwa sababu ya michango ni wazi kuwa mwalimu Mkuu au Mkuu wa
Shule ( HeadMaster) atachukuliwa hatua kali kwakuwa atakuwa ni moja kati
ya watu wanaomhujumu Rais Samia.
Amesema kuwa,wanafunzi wamepata
fursa ya kusoma bila malipo na itashangaza kuona wanazuiwa jambo ambalo
halitachekewa kwa namna moja au nyingine huku akisema madarasa hayo
lazima yazae matunda.
Kunenge,ameongeza kuwa Serikali kupitia
Rais Samia bado inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi na
kwamba matarajio ya Rais ni kuona watoto wakitanzania wananufaika na
madarasa hayo kwa kupata elimu bora.
Aidha, Kunenge amewataka
wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kamwe wasidanganywe na jambo lolote
kwakuwa Rais atapata faraja akiona juhudi zake za kujenga madarasa hayo
yanatumika kwa malengo.
Aidha, Kunenge amempongeza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mshamu Munde pamoja na Mkuu
wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa
madarasa hayo.
Kwa mujibu wa Kunenge,mpaka kufikia Junuari
18, 2022 tayari wanafunzi wa darasa la awali wameripoti shuleni kwa asilimia
44.68 ambapo maoteo yalikuwa 30,479 huku walioripoti Shuleni ni 13,618.
Kwa
upande wa wanafunzi wa darasa la Kwanza mwaka huu matoteo yalikuwa
52,709 lakini jumla ya walioandikishwa ni 29,724 sawa na asilimia
56.39.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bundikani Bernda Muyenjwa
,amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kupeleka fedha Shuleni kwani
walipokea jumla ya Sh.milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.Muyenjwa, amesema kuwa Shule yake imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka na kwa upande wa Shule za Kata zilizopo Kibaha Mjini inashika nafasi ya pili.
Hata hivyo,Muyenjwa,alimuomba Mkuu wa Mkoa kuangalia namna ya kuifanya Shule hiyo hiwe na kidato cha Tano na Sita kwakuwa eneo la ujenzi wa madarasa mengine lipo na walimu wake wapo vizuri katika ufundishaji.
Diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi, amemshukuru Rais Samia juu ya fedha hizo kwakuwa watoto wote wameingia darasani muda mmoja wa asubuhi na wanakaa kwenye viti tofauti na zamani walipokuwa wanakaa chini.
"Tunaendelea kumshukuru Rais kwa zawadi nzuri aliyotupatia na sisi hatuna cha kumlipa ila tunachoahidi ni zawadi pekee ya kutoa matokeo mazuri ya kidato cha nne yasiyokuwa na ziro,"amesema.
Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi wa kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Bundikani Abdul Hamad ,amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwajengea madarasa kwakuwa wanasoma katika mazingira mazuri.
Abdul,amesema hakuna cha kumlipa lakini wanaahidi kusoma kwa bidii na kumpa matokeo mazuri ya kidato cha nne na hata katika mitihani yao ya kila mwaka.