NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MWAMUZI kutoka nchini Zambia, Janny Sikazwe amezua gumzo kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2022) inayoendelea nchini Cameroon.
Ni wakati wa mchezo wa kundi F kati ya Tunisia na Mali uliomalizika kwa Mali kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Maamuzi ya utata yaliyotolewa na mwamuzi huyo katika mchezo huo yamezua mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na kuzua sintofahamu ya utimamu wa mwamuzi huyo kiafya hususani katika kipindi cha pili cha mchezo huo.
Janny awali alipuliza kimakosa kipyenga cha kumaliza mtanange huo dakika ya 85 tu kabla ya kupata shinikizo kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi la Tunisia na kubatilisha uamuzi huo.
Mara tu baada ya kuruhusu mchezo kuendelea mwamuzi huyo akamuonesha kadi nyekundu iliyokuwa na utata mkubwa mshambuliaji wa Mali El Bilal Toure kabla ya kuibua utata mwingine kwa kupuliza kipyenga cha kumaliza mchezo huo dakika ya 89 bila ya kuwa na sababu maalumu kitendo kilichowakera Tunisia.
Bao la Mali limepatikana kupitia mkwaju wa penaliti ya Ibrahima Kone dakika ya 48 baada ya madhambi ya Elyes Skhiri.
Baadaye kipa wa Mali, Ibrahim Mounkoro aliokoa mkwaju wa penalti dakika ya 77 kutoka kwa Wahbi Khazri.Hivyo kuyapa heshima matokeo ya timu yake ya Taifa.
Katika mtanange huo uliopigwa katika katika dimba la Limbe mjini Limbe, Cameroon,mchezaji wa akiba wa Mali, Toure alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumshika kifundo cha mguu mlinzi wa Tunisia Dylan Bronn.