Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Nishati ambayo inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Said wakati akikabidhiwa ofisi na Mtangulizi wake, Mhandisi Amos Maganga, Oktoba 29, 2021 aliwaasa watumishi kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu.
Mhandisi Said alisema, matumaini ya Watanzania, hasa wa vijijini, yanategemea dhamana ambayo REA imepewa.
“Tukitetereka katika kutimiza majukumu yetu, tutafifisha matumaini ya Watanzania wengi ambao wanategemea nishati kama nyenzo ya kubadilisha maisha yao,” alisisitiza Mhandisi Said.
Maono ya Mkurugenzi Mkuu REA,ni mwelekeo chanya kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambayo imedhamiria kuwaletea maendeleo wananchi kuanzia vijijini hadi mijini.
Mheshimiwa Rais Samia anaamini kila mtumishi na Watanzania wakitimiza wajibu na majukumu yao kwa ufanisi,Taifa litapata maendeleo ya haraka ikiwa ndiyo dhamira ya Serikali anayoiongoza.