NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa siku saba kwa vyombo vya upelelezi nchini kuhakikisha wahalifu waliotekeleza mauaji ya watu wa tano wa familia moja katika Kijiji cha Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wanapatikana.

Makamu wa Rais ameoneshwa kusikitishwa na kitendo cha mauaji ya wanafamilia hao licha ya kuwepo kwa majirani wengi wanaozunguka eneo hilo. Amesema jamii inapaswa kubadilika na kuishi kama ndugu pamoja na kuchukua tahadhari kwa wageni wote wanaoingia na kutoka katika vijiji hivyo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameliagiza jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua kukomesha vitendo vya mauaji yanayojitokeza hapa nchini. Amesema hivi karibuni maeneo mbalimbali ya nchi vimeibuka vitendo vya mauaji hivyo ni lazima wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Makamu wa Rais amemuagiza Mkuu wilaya ya Bahi pamoja kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya kufanya mkutano na wananchi wa eneo hilo ili kuimarisha ulinzi wa maeneo hayo.


Aidha ameuagiza uongozi wa Kijiji cha Zanka kufanya vikao vya mara kwa mara juu ya ulinzi na usalama wa maeneo hayo.
Makamu wa Rais amewasilisha rambirambi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa familia hiyo iliopoteza watu watano na kuwaeleza kwamba Rais ametoa pole na amesikitishwa na mauaji hayo.

Makamu wa Rais amewaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa mafundisho ya kukemea vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji hapa nchini.
Miili ya watu hao watano wa familia moja baba, mama, watoto wawili na mjuku mmoja walikutwa wameuwawa ndani ya nyumba yao Januari 22 mwaka huu na miili yao kutelekezwa.