NA MWANDISHI DIRAMAKINI
NDOTO za Simba SC kwenda kileleni mwa Msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwemo kutwaa ubingwa msimu huu imeendelea kudhoofishwa baada ya wenyeji Mbeya City kuharibu ratiba na mipango yao leo.
Wenyeji hao wa Jiji la Dar es Salaam wamepoteza mechi ya kwanza ya msimu wa ligi hiyo baada ya kuchapwa 1-0 na Mbeya City.
Mshambuliaji Paul John Nonga dakika ya 41 katika dimba la Sokoine jijini Mbeya ndiye aliyevuruga mipango yote ya mabingwa hao watetezi.
Ni baada ya kumsoma kwa kina mlinda mlango namba moja nchini, Aishi Salum Manula baada ya kumtoka beki, Hennock Inonga.
Aidha,Chris Mugalu aligongesha mwamba wa mkwaju wa penalti dakika 48 na Nahodha, John Raphael Bocco alipojaribu kwenda kumalizia ndani ya sita, kipa Deogratius Munishi (Dida) alidaka na kuzidi kuwapa maumivu wageni hao.
Aidha, penalti hiyo ilitolewa baada ya beki Juma Shemhuni kuangukia mpira wakati akijaribu kuokoa shambulizi la winga wa Simba, Kibu Dennis.
Mbeya City awali ilicheza pungufu baada ya beki wake, Mpoki Mwakinyuke kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 43 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Yanga SC ikiwa kileleni inaendelea kujigamba na alama zake 32 baada ya mechi 12 huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Simba SC wenye alama 24 ikiwa imecheza mechi 11.
Hata hivyo, huu unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Simba kupoteza ndani ya Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2021/22.
Jana watani zao Klabu ya Yanga ilianza vema baada ya kuondoka na alama tatu huku ikiwapa kichapo cha mabao 2-0 wenyeji Coastal Union.
Mtanange huo wa Ligi Kuu ya NBC ulipigwa katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga jan Januari 16,2022.
Fiston Mayele dakika ya 40 ambaye alimalizia krosi iliyopigwa na beki Djuma Shabani na Said Ntibanzokiza dakika ya 89 ambaye alimalizia pasi kutoka kwa Farid Mussa ndio walioharibu mipango ya wenyeji hao.