NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KLABU ya Simba yenye maskani yake jijini Dar es Salaam imekomba tuzo zote katika Kombe la Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Ni baada ya mtanange wa aina yake uliopigwa leo Januari 13,2022 baina yake na Azam FC ambao pia ni wenyeji wa jijini Dar es Salaam.
Katika fainali hizo za Kombe la Mapinduzi, Simba SC wameanzia kulichukua kombe lenyewe,mfungaji bora akawa Meddie Kagere.
Kwa upande wa golikipa bora ni Aishi Manula,mchezaji bora wa fainali ni Henock Inonga huku mchezaji bora wa Mapinduzi Kombe la Mapinduzi 2022 akiwa ni Pape Sakho.
Mtanange huo ambao umepigwa katika dimba la Amaan jijini Zanzibar, mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Azam ambao ni washindi wa pili wamevuta mkwanja wa zaidi ya milioni 10 baada ya maboresho makubwa katika kombe hilo mwaka huu.
Dakika 90 zilikamilika kwa ubao kusoma Azam FC 0-1 Simba na mfungaji ni Meddie Kagere aliyefunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti.
Aidha,Tepsi Evans wa Azam FC amepewa zawadi ya kuwa mchezaji bora muungwana.
Hili linakuwa taji la nne kwa Simba huku Azam FC ikiwa imetwaa mataji matano na ni mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi.
Mbali na Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliyewaongoza maelfu ya wananchi kushuhudia fainali za Kombe la Mapinduzi, pia mechi hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo.