Simba SC yawafuata Yanga kimya kimya, Dar City hoi!

NA GODFREY NNKO

SIKU moja baada ya Yanga SC kuwachapa Mbao FC bao 1-0 na kutinga Hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), watani zao Simba SC wameonesha jeuri kwa kuwatandika Dar City mabao 6-0.

Ushindi wa Yanga waliupata Januari 29, 2022 katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya mshambuliaji wao tegemeo,Fiston Kalala Mayele dakika ya 54 kupachika bao safi kwa kichwa akimalizia krosi ya Farid Mussa Malik kutoka kulia.

Aidha,leo Januari 30,2022 Simba SC imezinduka usingizini baada ya siku za karibuni kuonekana kuchechemea baada ya kulitumia vema dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwa kutwaa alama zote tatu zikisindikizwa na mabao hayo.
Dar City ambayo ni timu ya daraja la pili iliyoanzishwa mwaka 2016 ikiwa na maskani yake jijini Dar es Salaam, walijitahidi kwa kadri ya uwezo wao, lakini matokeo hayakuwa mazuri kwao.

Kwa Dar City, licha ya kushindwa kusonga mbele, mtanange huu unaweza kuwa ni heshima na kumbukumbu kwao kwa kukutana na klabu kubwa ndani na nje ya Tanzania. Pia, huenda imewapa picha halisi juu ya namna ya kukabiliana na vilabu vikubwa katika michezo ijayo siku za usoni.

Mabao yote ya Simba SC yamefungwa na Meddie (2), Clatous Chama, Rally Bwalya,Pascal Wawa na Chris Mugalu ambaye alimalizia kazi.

Aidha, Simba SC imewachukua mechi nne kupata ushindi kwa mara ya kwanza,na kuwaacha mahasimu wao Yanga kuendelea kushika usukani wa Ligi Kuu ya NBC.

Pablo atapona?

Iwapo wataendelea na kasi hii, pengine Kocha wa Simba, Pablo Franco raia wa Hispania anaweza kupona, hivyo kuendelea kuhudumu katika kukinoa kikosi hicho.

Mara nyingi, hitaji na matamanio ya mashabiki wa klabu hiyo na hata watani zao Yanga huwa ni ushindi kila mechi, hivyo ikionekana kocha ameshindwa kutekeleza majukumu yake, huwa anawekwa pembeni. Ikizingatiwa kuwa, mechi nne zilizopita, furaha ya wana Simba ilizima ghafla.

Pablo akiyumba huenda akamfuata Didier Gomes aliyetimuliwa baada ya Simba SC kung’olewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneg Galaxy ya Botswana.

Watetezi hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa wanasaka rekodi nyingine ya kutetea ubingwa msimu huu ikiwa ni wa tano mfululizo.

Aidha, wapo nafasi ya pili nyuma ya Yanga SC wakiachwa kwa tofauti ya alama 10 baada ya mechi 13 huku kukiwa hakuna mechi kiporo.

Wekundu hao wa Msimbazi kwa sasa,wamesaliwa na mechi mbili za kukamilisha duru ya kwanza dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza na mechi tatu mfululizo za Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Kundi D.

Mechi hizo za CAF ni pamoja na ile ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, US Gendermarie ya Niger na RS Berkane ya Morocco zitakazochezwa kati ya Februari 13 hadi 27,2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news