TANESCO yawatoa hofu Watanzania kuhusu upatikanaji wa umeme, yasisitiza hakuna giza

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewatoa hofu wateja wake kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini wakati wa uboreshaji wa mfumo wa gesi asilia kwenye visima vya gesi vya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Pan African Energy Tanzania kama yalivyotangazwa kuanza Februari Mosi hadi 10,2022. 
Akifafanua kuhusu matengenezo hayo leo Januari 31,2022 wakati wa ziara aliyoifanya na waandishi wa habari kwenye Kituo cha Kupoza Umeme cha Kunduchi jijini Dar es salaam,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande amesema, nchi haitakuwa gizani na kwamba hakuna maeneo yatakayoathirika kwa siku zote 10 mfululizo kwa kukosa umeme.

‘‘Visima vile vya gesi asilia si vya TANESCO ni vya TPDC, SONGAS na PAET sisi ni wateja tunaochukuwa gesi kutoka kwao na ili wao watupatie nishati hiyo zaidi ni lazima kufanya maboresho ndani ya siku hizo 10 tulizozitangaza, hakuna eneo litaathirika zaidi ya siku tatu kwa kukosa umeme ndani ya siku hizo kumi za kupisha matengenezo na tayari tumeshatoa ratiba kwa maeneo yote yatakayoathirika kwa kila mikoa husika nchi nzima,’’amefafanua Maharage.
Aidha, amesema sambamba na matengenezo ya visima hivyo shirika litaendelea na maboresho yake na matengenezo mbalimbali kwenye miundombinu yake ndani ya muda wa siku 10 katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha matengenezo yatakapokamilika huduma ya umeme inarejea katika hali yake ya kawaida.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema kazi ya kuongeza uwezo wa kupokea na kupoza umeme katika Kituo cha Kunduchi kilichopo eneo la Salasala jijini Dar es salaam ipo ukingoni na tayari transfoma mpya yenye ukubwa wa MVA 195 imekamilika kufungwa.
‘‘Transfoma hii inategemewa kuwashwa ili kuanza kutumika wakati wa kipindi cha matengenezo ya visima vya gesi na umeme kama nilivyozungumza wiki ya jana,"amesema Maharage.

Akieleza kwa undani faida za transfoma hiyo kwa wateja wanaohudumiwa na kituo hicho Meneja mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Mhandisi Regina Mvungi amesema transfoma hiyo itasaidia kuondoa matatizo ya umeme kucheza, kuwa mdogo na kuboresha hali ya upatikanaji umeme kuwa ya kutabirika na ya uhakika.
Vilevile faida zingine ni itasaidia wateja kutokosa huduma pindi transfoma moja itakapopata hitilafu tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali na kuwezesha mikoa mingine ya Kitanesco kama Kinondoni Kusini kuwapa wateja huduma wanapokuwa na matengenezo mbalimbali ya umeme.

Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Kunduchi kilianzishwa mwaka 1995 ambapo kutokana na ongezeko la mji kukuwa kwa kasi na uhitaji wa umeme ililazimu TANESCO kununua transfoma mpya kubwa itakayosaidia kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news