NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Maharage Chande amesema, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo aliyoyatoa ambayo anaamini yanakwenda kuongeza ufanisi na kuharakisha utoaji wa huduma ya usambazaji wa umeme nchini.
"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake aliyoyatoa yataharakisha mipango yetu.Maelekezo tumeyapokea na tayari tumeanza utekelezaji wake kwa kuhakikisha gharama za kuwaunganisha wateja zinaendana na uhalisia, kwa maana ya maeneo ya mjini na vijijini.
"Mabadiliko haya yatatusaidia sisi kutuongezea uwezo, tutakwenda kwa kasi zaidi katika kutoa huduma kwa kasi zaidi, kwa hiyo mabadiliko haya msingi wake mkubwa ni kuhakikisha kwamba huduma inaboreka na vilevile kuwahudumia wateja kwa haraka;
Mkurugenzi Mtendaji huyo ameyasema hayo leo Januari 6,2022 wakati wa mahojiano na runinga ya Azam ya jijini Dar es Salaam.
"Hatari ya kutofanya mabadiliko haya itakuwa ni vigumu kutoa huduma bora zaidi ambapo wote tunataka iwe hivyo, vilevile itakuwa vigumu sisi kukarabati miundombinu yetu na kuhakikisha kuwa ipo katika hali nzuri.
"Mabadiliko haya yatatusaidia sisi kuongeza uwezo, tutakwenda kwa kasi zaidi katika utoaji wa huduma zetu kimsingi tutahakikisha kwamba huduma inaboreka na pia kuwahudumia wateja wetu kwa wakati,"amefafanua Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Maelekezo ya Rais
Awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alisema, kuna maeneo nchini gharama za kuunganishwa umeme haitakuwa shilingi 27,000.
Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo Januari 4,2022 baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 Ikulu jijini Dar es Salaam.
"Tuliharibiwa kwa kusema mwananchi ataungiwa umeme kwa 27,000,gharama za umeme haziko hivyo,kuna maeneo tutafanya hivyo kuwabeba wananchi,kuna maeneo lazima gharama ya umeme irudi pale pale,Waziri umeogopa kusema,nakusaidia nenda katekeleze.
"Kuna maeneo lazima gharama ya umeme ibebe uhalisia unapompangia TANESCO aende akaunge umeme kwa elfu 27 kwa kila mtu yeye anatoa wapi hizo fedha? Hana pa kuzitoa lazima aunge umeme kwa gharama inayopaswa kwa kila pahala, Waziri nenda kasimamie hilo.
"Juzi nilikuwa naona watu wanalalamika kwenye TV wameshalipa miezi kadhaa umeme hawaungiwi ukiuliza TANESCO wanasema hatuna nguzo, hatuna vifaa elfu 27 tunafanyaje?Kwa hiyo waziri nenda usimamie watu walipe fedha inayotakiwa.
"Kila anayetaka umeme alipe gharama stahiki msiende juu, lakini nendeni kwenye gharama ambayo mwanachi atamudu kulipa na wale wa hali ya chini kabisa tuwabebe kama sera yetu inavyosema,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hatua za TANESCO
Chini ni gharama za kuunganisha umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO);