Tanzania Commercial Bank yazindua tawi jipya mkoani Katavi, yapokelewa kwa shangwe

NA MWANDISHI MAALUM

TANZANIA Commercial Bank (TCB) imezindua tawi jipya Mkoa wa Katavi Wilaya ya Mpanda ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma za kibenki karibu kwa wateja na wananchi kwa ujumla.

Tawi hilo la kwanza kwa taasisi za fedha kuzinduliwa Mkoa Katavi Wilaya ya Mpanda, limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko .
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Mwamvua Mrindoko (kushoto), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Tanzania Commercial Bank (TCB) katika Manispaa ya Mpanda mjini mkoani Katavi, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Onesmo Buswelu na Meneja wa Tawi la Mpanda, Julius Mlang'a pamoja na maofisa wa kamati ya ulinzi ya mkoa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Sabasaba Moshingi alisema huo ni mwendelezo wa Tanzania Commercial Bank katika kusogeza huduma kwa wateja wake.

Alisema, tawi hilo jipya la Mpanda litarahisisha utoaji huduma za kibenki kwa wateja wake, hali ambayo itapunguza mzunguko wa wananchi kuzifuata huduma za kibenki maeneo mengine ya mbali.

Aliongeza kuwa, Tanzania Commercial Bank (TCB) imezingatia shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa wilayani humo kwa wafanyabiashara, wafugaji na wakulima kwa kufungua tawi hilo hivyo wateja hawatalazimika kwenda mjini kupata huduma za kibenki kama hapo awali.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Mwamvua Mrindoko wa (kushoto), akipokea kadi ya ATM kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Commercial Bank TCB, Sabasaba Moshingi, alipofungua akaunti alipoalikwa kuwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tawi jipya la Tanzania Commercial Bank lililofunguliwa katika Manispaa ya Mpanda mjini mkoani Katavi, wengine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Onesmo Buswelu na Meneja wa Tawi la Mpanda, Julius Mlang'a pamoja na maofisa wa wengine kutoka TCB.

Alisema,TCB sio kwamba tu ni benki kubwa nchini, bali inatoa mchango mkubwa katika shughuli za kijamii hasa kuinua elimu pamoja na afya.

"Kwa kuona umuhimu wa kusongeza huduma kwa wateja hasa maeneo ya vijijini Tanzania Commercial Bank (TCB) inaendelea kuwawezesha mawakala watakaosaidia kutoa huduma hizo jambo ambalo litasaidia kusogeza huduma kwa wateja wetu nchi mzima,"amesema.

Ameongeza, kwa sasa benki hiyo ina matawi 82, "Mawakala tunao zaidi 3,800, mashine za kutolea pesa ATM zetu tunazozitegemea kama Tanzania Commercial Bank ni 84, lakini zile ATM ambazo tupo chini ya Umoja Switch ni zaidi ya 250,"amesema.

Akizungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Tawi jipya la Tanzania Commercial Bank, mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko ameupongeza uongozi wa Tanzania Commercial Bank kwa kuja kuwekeza katika mkoa huo na anaamini kwa wingi wa watu waliojitokeza katika tukio hilo watakwenda kufungua akaunti.

Mrindoko pia ameipongeza Tanzania Commercial Bank (TCB) kwa kufika mkoani Katavi na kuwakaribisha, kwani fursa zipo nyingi katika mkoa huo zikiwemo za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na mazao mengine ya kimkakati.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliuhakikishia uongozi wa Tanzania Commercial Bank (TCB) kwamba Katavi ni mkoa unaokua kwa kasi sana kutokana na shughuli za uzalishaji na za kimaendeleo hivyo huduma ya Tanzania Commercial Bank kwa kufungua tawi hilo limekuja wakati muafaka

“Kuzinduliwa kwa Tawi la Tanzania Commercial Bank (TCB) hapa Katavi maana yake ni kwamba huduma za kibenki zitapatikana kwa urahisi zaidi hivyo wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara wa Katavi changamkieni fursa hii na kuja kufungua akaunti na kufanya miamala mingine kama kulipa kodi za serikali," amesisitiza Mrindoko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news