TARURA inavyofungua barabara kufika kusikofikika mkoani Rukwa na Katavi

NA ERICK MWANAKULYA-TARURA

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kufungua barabara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwezesha wananchi kufika sehemu mbalimbali ambazo hapo awali zilikuwa hazifikiki.
Katika Mkoa wa Rukwa, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nkasi pamoja na Manispaa ya Sumbawanga.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Mhandisi Samson Kalilo ameeleza kuwa ongezeko la bajeti limewezesha ufunguzi wa barabara ya Miyangalua-Movu yenye urefu wa Km 8 ambayo imegharimu shilingi Milioni 80 na ukarabati wa ujenzi wa daraja na barabara ya Laela-Mission uliogharimu shilingi milioni 161.

“Barabara hii ambayo tumeifungua kwa kiwango cha changarawe kutoka Miyangalua-Movu ilikuwa ni korofi hasa kipindi cha masika na kusababisha wananchi hasa wakulima wa mazao ya mahindi na maharage kushindwa kusafirisha mazao yao kwa urahisi kwenda kwenye masoko,”amesma.

Naye, Mkazi wa Sumbawanga vijijini, Ndg. Alfred Hassan ameishukuru Serikali kwa uboreshwaji wa miundombinu na kusema walikuwa wanapata changamoto ya kusafirisha mazao yao kwenda Mji mdogo wa Laela na Manispaa ya Sumbawanga kutokana na ubovu wa barabara lakini ufunguaji wa barabara hiyo umewasaidia sana wakazi wa maeneo hayo kusafirisha mazao yao.

Katika Manispaa ya Sumbawanga, TARURA imetekeleza ujenzi wa Daraja la Kankwale linalounganisha Sumbawanga Asilia na Kijiji cha Kankwale ambalo limegharimu shilingi Milioni 238 mpaka kukamilika kwake, ujenzi wa barabara ya Tawaqal Petrol station-Mahakama Kuu yenye urefu wa Km 1 kwa kiwango cha lami ambayo imegharimu shilingi milioni 500, pamoja na ujenzi wa daraja la Momoka linalounganisha Kata ya Senga na Momoka ambalo limegharimu shilingi Milioni 244.

Meneja wa TARURA Manispaa ya Sumbawanga, Mhandisi Samson Kalesi ameeleza kuwa uboreshwaji wa miundombinu unafanyika ili kuwezesha wananchi kufika kusiko fikika na kupata huduma za kijamii kiurahisi.

Diwani wa Kata ya Momoka, Mch. Charles Chakupewa ameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kuchukua jitihada za haraka za ujenzi wa Daraja la Momoka linalounganisha Kata ya Senga na Momoka na kueleza kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa ni kiungo muhimu kwa wakazi wa Kata hizo mbili kupata huduma za kijamii kwa urahisi.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Mhandisi Elly Mkwizu ameeleza kuwa TARURA ipo katika ujenzi wa Daraja la Kavunja lililopo Mto Kavunja ambalo limefikia asilimia 70 kukamilika na litagharimu shilingi bilioni 1.79. Ujenzi wa daraja hilo utasaidia kutatua kero ya muda mrefu ya usafiri kwa Wakazi wa Korongwe ambao wanatumia umbali wa zaidi ya Km 200 kwenda Namanyere lakini kupitia ujenzi wa daraja la Kavunja watatumia Km 35 kuweza kufika Namanyere kwa kupitia Kilando.

“Ujenzi wa Daraja la Kavunja ni muhimu katika kutatua changamoto wanayoipata wananchi hasa wakati wa mvua kutokana na maji yanayotoka ziwa Tanganyika kujaa katika eneo hili na kusababisha adha ya usafiri kwa wakazi wa Korongwe ambao hutumia umbali mrefu kwenda Namanyere lakini daraja hili likikamilika litasaidia wananchi kufikia huduma za kijamii kwa urahisi”, amesema Mhandisi Mkwizu.

Naye Mkazi wa Kijiji cha Masengule, Kata ya Kilando, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Ndg. Rogata Kapeta amefurahia ujenzi wa Daraja la Kavunja kwa kuwa ni kiunganishi kikubwa kwa wakazi wa maeneo hayo na kuongeza kuwa hapo awali watu wengi wamefariki kwa kuliwa na mamba na mama wajawazito kushindwa kwenda kupata huduma za afya kwa sababu ya maji kujaa katika mto huo, hivyo ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo.

Katika Mkoa wa Katavi Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea Kufungua barabara kufika kusiko fikika katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mlele, Tanganyika na Mpimbwe.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Mhandisi Nolasco Kamasho ameeleza kuwa TARURA imefungua barabara ya Nshama-Songambele yenye urefu wa Km 5, barabara ya Inyonga-Imarauduki yenye urefu wa Km 10 na ujenzi wa barabara ya Inyonga-Nswekwa yenye urefu wa Km 3 kwa kiwango cha lami kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuwezesha wananchi kusafirisha mazao yao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Imarauduki, Ndg. Richard Fabiano ameishukuru Serikali kwa kuwafungulia barabara kufika kusiko fikika kwani hapo awali iliwalazimu kuzunguka umbali wa Km 20 kwenda Inyonga ila kwa ujenzi wa barabara ya Inyonga-Imarauduki itakapokamilika itawasaidia sana katika shughuli zao za kiuchumi.

“Tunaishukuru Serikali kwa kututengenezea barabara hii kwani eneo hili kipindi cha masika linajaa maji na inapelekea tuzunguke linajaa maji na kupelekea tuzunguke umbali wa Km 20 kwenda wilayani kusafirisha mazao yetu, kwa sasa tuna imani barabara hii itakuwa mkombozi sana kwetu”, alisema Ndg. Richard.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo TARURA imefungua barabara ya Tambazi-Mtambo Km 16, Katumba HC-Kalungu Km 1.5, Mnyeki-Kambulonge Km 13, Mtapenda-Ndurumo Km 6.82 na Msaginya-Kanonge-Kambona Km 3.95 ambazo zitagharimu shilingi milioni 500, pia imefanya matengenezo ya daraja la Mtapenda ambalo limegharimu shilingi milioni 232 ili kuwezesha wananchi kusafirisha mazao yao.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Rukwa unahudumia mtandao wa Barabara wenye urefu wa Km 1818.823 ambapo lami ni Km 38.70, changarawe Km 747.46 na udongo Km 1032.663. Mkoa wa Katavi TARURA inahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa Km 2475.65 lami ni Km 36.42, changarawe ni Km 442.841 na udongo ni Km 1996.367.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news