NA MWANDISHI MAALUM
WATUMISHI wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) wamepongezwa kwa namna ambavyo wametumia sherehe za maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kutoa elimu kwa wananchi mbalimbali kuhusu mionzi.
Pongezi hizo zimetolewa leo Januari 12,2022 na wananchi hao kwa nyakati tofauti, wakati TAEC ikiendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya utekelezaji wa majukumu yake Kisheria kwenye Maonesho ya 58 ya Mapinduzi Matukufu, Viwanja vya Maisara jijini Zanzibar.
Wakiongozwa na kauli mbiu ya "Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa", watumishi wa TAEC walionekana wakitoa nafasi kwa kila mwananchi kujifunza na kuuliza maswali kadri wanavyoona huku wakipatiwa majibu ya papo kwa papo, jambo ambalo limewapa faraja wengi.
Mwananchi akipata maelezo juu ya mtambo maalum utakaotumika kuhifadhi bidhaa mbalimbali za kilimo ili zisiharibike mapema. Ni katika Viwanja vya Maisara jijini Zanzibar katika kumbukizi za miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu.(Picha na TAEC).
"Ni jambo la kheri, nimejifunza mambo mengi sana kuhusu Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania,nimeelewa kuwa mbali na kudhibiti mionzi, pia TAEC inatoa huduma ya matengenezo ya vifaa vya mionzi ili kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi. Niwapongeze sana kwa kazi nzuri, Watanzania tunawategemea sana maana kazi yao ni muhimu mno katika usalama wa maisha yetu ya kila siku,"amesema mmoja wa wananchi hao mkazi wa jijini Zanzibar.
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ni taasisi iliyoundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomiki Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003) inayoipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia nyuklia hapa nchini ili kulinda wafanyakazi, wananchi, wagonjwa na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.
TAEC yenye Makao yake Makuu jijini Arusha ina Ofisi za Kanda na Mipaka zipatazo ishirini na saba (27), huku Ofisi ya Kanda ya Dar es Salaam pekee ina jumla ya Ofisi ndogo ishirini na tatu (23), hii yote ni katika kuhakikisha udhibiti wa matumizi salama ya mionzi unafanyika kikamilifu sambamba na kuhakikisha TAEC inarahisisha ufanyikaji wa biashara kwa kutoa vyeti vya mionzi kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Bw. Peter Ngamilo ambaye ni Afisa Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwenye Maonesho ya 58 ya Mapinduzi Matukufu, Viwanja vya Maisara jijini Zanzibar.
"Huu ni muendelezo wa utoaji wa elimu kwa wadau na wananchi ambapo sisi TAEC kama taasisi yenye mamlaka ya udhibiti wa mionzi hapa nchini tuna jukumu kubwa la kuhakikisha hatuweki rehani afya na maisha ya watanzania dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi, kwani mionzi ina madhara makubwa ambayo yanaweza kuwa ya muda mfupi au muda mrefu ikitegemeana na kiwango cha mionzi alichokipata muhusika, kama vile magonjwa ya saratani, hivyo ushiriki wetu kwenye maonesho haya ni muhimu sana katika kufikisha elimu kwa watanzania juu ya majukumu tunayoyatekeleza ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," amesema Bw. Ngamilo.
Bw. Ngamilo amesema kuwa, matumizi ya mionzi ambayo ndio teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali hapa nchini zenye manufaa ya kiuchumi na kijamii kama vile Afya, Kilimo, Ufugaji Viwanda, Maji,Utafiti na ujenzi, hivyo katika kuhakikisha usalama wa matumizi hayo, TAEC ina jukumu la kuhakikisha inatoa vibali vya uingizaji, usafirishaji, utumiaji na umiliki wa vyanzo vyote vinavyoingia nchini ili kuhakikisha vyanzo hivyo viko katika ubora unaotakiwa kama ambavyo Sheria ya Tume ya Nguvu za Atomiki na Kanuni zake zinavyoelekeza.
Bw.Ngamilo ameenda mbali na kusema kuwa pia majengo yote ambako vyanzo hivyo husimikwa kwa ajili ya kutumika ni lazima yajengwe kwa utaratibu na viwango kama ambavyo sheria imeelekeza ili kuzuia uvujaji wa mionzi na kuweza kusababisha athari kwa wananchi na mazingira.
Amesema, mionzi ina faida nyingi kwa maendeleo na ustawi katika jamii kwani inatumika kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, mifugo, ujenzi, maji, nishati na viwanda.
Pamoja na kuwa na faida nyingi, lakini isipotumika inayotakiwa inaweza kuingia katika mnyororo wa chakula ambao ni hatari kwa afya ya binadamu na wanyama.