NA NTEGHENJWA HOSSEAH-OR TAMISEMI
MIJI mitano mikubwa nchini inatarajia kuanzishwa usafiri wa umma wa (mwendokasi) baada ya mapendekezo ya sheria ya usafiri wa umma mijini itakapopitishwa, lengo likiwa ni kuweka mfumo rasmi wa kuboresha usafiri wa umma na ukuaji wa Miji Endelevu.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka Dkt. Edwin Mhede wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa kutembelea na kuangalia kazi mbalimbali zinazotekelezwa na DART.
Dkt. Mhede amesema Miji hiyo ni Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Tanga. Hii ni kutokana na miji hiyo kuwa na uhitaji wa usafiri wa umma ukiondoa jiji la Dar es Salaam ambalo tayari lina usafiri.
Aidha, aliongeza kuwa, "lazima tuwe mbele ya mipango ya wananchi, tupange miji yetu kwa maendeleo endelevu, sio tunawasubiri mpaka wananchi wameendeleza maeneo yao kisha ndio tunakuja na mipango ambayo inawaathiri kiuchumi na kisaikolojia.
Hivyo maoni yetu ni kuhakikisha kuwa Kadri miji hii inavyoendelea kukua inapata mfumo mzuri wa usafiri ili kuepusha msongamano huko mbeleni na kuwa ni Miji yenye uchumi endelevu," alisisitiza Dkt. Mhede.