USOMAJI SHAHADA YA UZAMILI YA KISWAHILI CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA

Sehemu ya Kwanza

LEO Tunapenda kuzungumza na wote wanaopenda kujiunga na masomo ya programu ya Umahiri ya Kiswahili ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. 
Katika sehemu hii tumezungumzia juu ya njia za ufundishaji na ujifunzaji kama ifuatavyo;

Mihadhara kwa njia ya ZOOM

Programu yetu ya Umahiri ya Kiswahili inafundishwa kupitia mtandao wa ZOOM ambapo walimu hutoa mihadhara kwa wanafunzi wa ndani na nje ya Tanzania. 

Mihadhara hiyo hufanyika muda baada ya kazi na siku za mwisho wa wiki. Ratiba ni nyumbufu kutegemea na aina ya wanafunzi na shughuli zao za kujiajiri au kuajiriwa wanazofanya. Jiunge sasa upate mihadhara ukiwa mahali popote.

Semina kupitia ZOOM 

Wanafunzi wa Shahada ya Umahiri ya Kiswahili hufanya semina kupitia mtandao wa ZOOM. 

Wanafunzi hupangwa katika vikundi vya wanafunzi wanne na kupatiwa maswali ya mjadala kwa ajili ya mawasilisho ya semina. Wanafunzi hao hukutana kwa ZOOM na kufanya mjadala wa kina katika kikundi chao na baada ya hapo huandaa wasilisho ambalo huwasilishwa kwenye semina ya darasa zima. 

Baada ya uwasilishaji wanadarasa hutoa maoni yao na maswali katika wasilisho husika. Baadae waandaji wa wasilisho hupata fursa ya kujibu na kupokea au kukataa maoni kwa hoja zenye mashiko.

What's App Kimbwetta 

Baada ya wawasilishaji kupewa maoni juu ya wasilisho lao, hutakiwa kwenda kuandika kazi yao vizuri kwa misingi ya kitaaluma. Baada ya kazi kukamilika huwasilishwa kwenye group la What's App katika mfumo wa PDF. Hapo sasa wanafunzi wote hupata fursa ya kujisomea kazi iliyoandaliwa na wenzao ambayo pia ilipata maoni kutoka kwa wanafunzi wote wa darasa au kozi husika.

Kutuma kazi kwenye Email

Kazi hiyo ya wasilisho la wanafunzi iliyotumwa kwenye What's App hutumwa pia kwa mhadhiri wa kozi kupitia email ili kumwezesha mwalimu kuipakuwa na kuisahihisha kama sehemu ya tamrini ya kozi husika. Njia hii ya email hutumika pia wakati wa utafiti na uandishi wa tasinifu.

Moodle Platform

Huu ni mfumo Mama katika ufundishaji na ujifunzaji hapa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Katika mfumo huu kila kozi imepakiwa maalumati (notes) za kutosha kwa kila kipengele kilichopo kwenye muhtasari (course outline) wa kozi. Wanafunzi wote wa Shahada ya Umahiri katika Kiswahili hupatiwa Nywila ya kuingia kwenye mfumo na kujisomea kozi zake zote chini ya usimamizi na maelekezo ya mhadhiri ambaye naye yupo ndani kwenye mfumo huo wa Moodle Platform. Maalumati yaliyopo kwenye mfumo ni pamoja na matini za maandishi, sauti, video, picha na orodha ya marejeleo ambayo mwanafunzi anapaswa kuyasoma katika kozi husika.

Baada ya mwanafunzi kupata mafunzo kupitia mifumo hii anakuwa yupo tayari kwa ajili ya mitihani na atasajili mitihani yake kwa kufuata Almanac ya chuo na mitihani yote ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania husimamiwa na Kurugenzi ya Mitihani. Kimsingi usomaji wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania umeimarika sana kutokana na matumizi makubwa ya TEHAMA na tunawafikiwa wanafunzi popote pale ulipo.

Njoo ujiunge Programu ya M.A Kiswahili ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na programu nyingine zote kwani nazo pia hufunzwa kupitia mfumo huu. 

Karibu sana ufuatilie sehemu ya pili ambayo itaelezea sifa, namna ya kujiunga, ada na muda wa kozi mpaka kumaliza.

WENU


Dkt. Mohamed Omary Maguo

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

2/1/2022

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news