NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WADAU wa Jukwaa la Maji, Bodi ya Maji Bonde la Kati wameitaka jamii kutunza na kutumia vizuri maji na vyanzo vyake ili viwasaidie hapo baadae.
Wamesema, kuna uwezekano wa kutokea uhaba wa maji kutokana na uchache wa mvua unaoendelea katika maeneo mbalimbali ambazo ndio chanzo kikuu cha asili ya maji.
Wadau wa maji Bodi ya Maji Bonde la Kati wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa jukwaa la pili lililofanyika mwishoni mwa wiki mkoani Singida.
Waliyasema hayo katika jukwaa la pili lililolenga kuandaa na kuidhinisha mipango kazi ya vikundi kazi pamoja na mambo mengine wameisisitiza jamii kutumia vizuri maji pamoja na kutunza vyanzo vya maji katika maeneo yao.
Wamesema,uchache wa mvua uliojionyesha msimu huu unatishia kuwepo kwa kiwango cha maji ya kutosha ambapo Mwenyekiti wa Bodi za Maji za Mabonde nchini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Segule Segule amesema licha ya uchache wa maji uliopo hivi sasa jamii pia inapaswa kutumia vizuri maji yaliyopo.
Aliongeza kuwa, kama serikali kupungua kwa maji inatoa ishara ya kutengeneza miundombinu ya kutunza maji kwa ujenzi wa mabwawa na miundombinu ya kuifadhia maji kutokana maji mengi ya asili yatokanayo na mvua yanaenda kwenye maziwa na mengine yanapotea.
“Mwishoni mwa 2021 mpaka hapa tulipofikia hali za rasilimali ya maji nchini sio nzuri hususani bonde letu la kati tuna mikoa nane, mikoa hiyo ipo katikati ya nchi na inaongoza kwa idadi ya mifugo nchini asilimia 58 ya mifugo nchini inayopatikana na ukiangalia athari za kwenye vyanzo vya maji, ukame unazidi mabadiliko ya tabia nchi hali hiyo imeathiri vyanzo vya maji , mifugo imeanza kufa na hali hii kama itaendelea hivi itaweza kuleta migogoro ya matumizi ya maji,”alisema Nelea Bundala.
Lazaro Msagu Mwenyekiti wa jukwaa la wadau wa maji bodi ya maji bonde la kati Akitoa Ushauri wake kwa wanajukwaa kufanya tathmini ya namna ya kutafuta suluhu kulikomboa bonde hilo.
Nelea hakuishia hapo akataoa wito na pendekezo kwa wadau wote wa maji kupitia idara mbalimbali kutoa elimu kwa jamii namna ya kutunza vyanzo vya maji ili viweze kusaidia katika kipindi hichi ambacho kuna tishio la ukame.
Alisema, kupotea au kupungua kwa maji katika maeneo mbalimbali kunachagizwa na shughuli za kibinadamu kama vile kulima ndani ya vyanzo vya maji, uchenjuaji wa madini, utifuaji wa ardhi.
“Upungufu wa sasa hivi unasababishwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo kulima ndani ya mita 60, kufanyatua matofali kwenye mito, uchenjuaji wa madini hasa dhahabu kwenye vyanzo vya maji kama vile mito au maziwa,”alisema Danford.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wadau wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati, Lazaro Msagu amesema wao kama wadau wanapaswa kufanya tathmini ya namna ya kutatua changamoto za maji katika bonde hilo la kati.
Kwa mujibu wa jukwaa la wadau wa maji bodi ya maji bonde la kati zaidi ya watu 200 wa bonde la kati wana maji, lakini hawana vibali vya kutumia rasilimali hiyo jambo ambalo jukwaa limepaswa kuitatua changamoto hiyo.
Jukwaa la Wadau wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati liliundwa mwaka 2019 mara baada ya kuanzishwa kwa Jukwaa la Wadau wa Maji wa Bonde la Taifa 2017 ambapo katika kikao cha Januari 14, mwaka huu kilijikita kuangazia majukwaa mengine yaliopita.
Sambamba na kupendekeza wajumbe wa bodi ya maji bonde la kati ambao wataenda kuchaguliwa na Waziri wa Maji.