NA MATHEW KWEMBE-NEC
MCHAKATO wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Ngorongoro na ule wa udiwani katika kata tano za Likombe Manispaa ya Mtwara Mikindani, Nalasi Mashariki wilayani Tunduru, Naumbu wilayani Mtwara, Handali wilaya ya Chamwino, na Nyabulanda katika wilaya ya Nyang’hwale ulikamilika tarehe 11 Disemba, 2021 kwa wananchi wa maeneo hayo kuwachagua wawakilishi wao wanaowataka.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ngorongoro, Dkt.Jumaa Mhina (kushoto) akikabidhi cheti cha ushindi wa kiti cha ubunge kwa mbunge mteule wa jimbo la Ngorongoro, Emmanuel Lekishon Shangai baada ya kuibuka mshindi kwa kupata kura 62,017 kati ya kura 62, 528 zilizopigwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Desemba 11,2021.
Pia kata za Ipwani katika wilaya ya Mbarali na Bomalang’ombe katika wilaya ya Kilolo zilipata wawakilishi wake wa udiwani baada ya wagombea wake kupita bila kupingwa.
Kufanyika kwa uchaguzi huu mdogo katika maeneo hayo ni kwa kuzingatia Ibara ya 76 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343), Kifungu 76 (3) na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mitaa (Sura ya 292), Kifungu 13 (6).
Ibara na vifungu hivyo vya sheria vimebainisha kwamba Chaguzi Ndogo za Ubunge na Udiwani hufanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kupita na haziendelei kufanyika baada ya kubakia miezi 12 kabla Bunge halijavunjwa kupisha Uchaguzi Mkuu mwingine.
Kuelekea uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani uliofanyika tarehe 11 disemba, 2021, Tume ya Taifa ya uchaguzi kupitia Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura ilifanya kazi kubwa ya uhamasishaji wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutumia gari la matangazo na kampeni ya nyumba kwa nyumba walifanikiwa kupita katika kata zote ili kuleta hamasa kwa wananchi ambao ndiyo walioshiriki zoezi la kupiga kura.
Makala hii inalenga kuelezea wajibu wa wananchi na vyama vya siasa katika kufanikisha chaguzi za kidemokrasia nchini Tanzania kwa kuangazia ushiriki wa wadau hawa katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani uliofanyika hivi karibuni.
Wananchi wa jimbo la Ngorongoro na kata za Likombe, Nalasi Mashariki, Handali, Naumbu na Nyabulanda walishiriki kikamilifu mchakato wote uchaguzi huo wa kidemokrasia ambapo walijitokeza kwa wingi kuhudhuria mikutano ya kisiasa ili kuwasikiliza wagombea wa vyama mbalimbali.
Katika hatua zote za uchaguzi huu mdogo wa ubunge na udiwani wananchi walipata fursa ya kujielimisha juu ya sheria, kanuni na taratibu za chaguzi za kidemokrasia za namna hiyo.
Kadhalika, wananchi waliotimiza masharti ya kupiga kura na ambao walikwishajiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura katika jimbo la Ngorongoro na kata nne zilizoshiriki uchaguzi mdogo wa udiwani walijitokeza kupiga kura na kumchagua mgombea wanayemtaka bila ya kutishwa ama kurubuniwa.
Wananchi wote waliokuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura kama ilivyobainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 10 (1) na (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 15 (1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, walipata fursa hiyo na kutimiza wajibu wao.
Miongoni mwa sifa hizo ni pamoja na kuwa Raia wa Tanzania, kutimiza umri wa miaka 18, na awe hajapoteza sifa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge.
Kwa mantiki hiyo wananchi waliotimiza vigezo tajwa ambao waliweza kufika katika vituo vya kupiga kura walishiriki kikamilifu zoezi hilo na kutimiza wajibu wao wa kufanikisha chaguzi za kidemokrasia nchini.
Wananchi wa Ngorongoro na kata tano zilizoshiriki kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani walipata fursa ya kuwachuja wagombea kwa kusikiliza sera zao na kuona ni mgombea yupi anayefaa kuwa mwakilishi wao, ambaye ataweza kuwawakilisha ipasavyo katika vikao vya uamuzi.
Ili kufanikisha chaguzi za kidemokrasia, wananchi wana wajibu mkubwa wa kushiriki mchakato mzima wa uchaguzi kwani kwa kufanya hivyo siyo tu wanatimiza wajibu wao lakini pia wanachochea maendeleo ya eneo lao kwa kuchagua mgombea ambaye atawasaidia katika harakati zao mbalimbali za kujikwamua kiuchumi.
Kwa hakika haipendezi kuona mwananchi ambaye hapendi kushiriki chaguzi za kidemokrasia akilalamika kuwa eneo lake limepata Mbunge au Diwani asiyefaa bali mwananchi huyo anapaswa kujilaumu mwenyewe kwani anachangia kurudisha nyuma maendeleo ya eneo lao.
Hii ni kwasababu vipaumbele vya eneo husika katika vikao vya uamuzi hupendekezwa na wawakilishi wa wananchi ambao ni waheshimiwa wabunge, na madiwani, hivyo mwananchi anapaswa kuitumia vizuri kura yake ili aweze kumchagua kiongozi mchapakazi na anayependa maendeleo.
Kura moja ina thamani kubwa katika kumchagua kiongozi unayemtaka katika chaguzi za kidemokrasia hivyo mwananchi mmoja anaposhindwa kushiriki zoezi la kupiga kura analikosesha jimbo/kata yake kuchagua mtu sahihi wa kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wa vyama vya siasa ambavyo vilishiriki uchaguzi wa Ngorongoro na Udiwani, vilikuwa na wajibu wa kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwasisitizia wanachama wao kuheshimu na kufuata sheria za uchaguzi pamoja na sheria nyingine za nchi pamoja na kanuni na taratibu zilizowekwa.
Uzoefu unaonyesha wananchi huhamasika kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye mikutano ya kampeni lakini wanaoshiriki zoezi la upigaji kura siyo wengi kama wanaojitokeza kipindi cha kampeni.
Hivyo vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani, kwa mujibu wa maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020, viliwajibika kuheshimu na kufuata Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi, kanuni za uchaguzi na maelekezo ya Tume ya Taifa ya uchaguzi pamoja na sheria nyingine za nchi katika kipindi chote cha uchaguzi.
Pia vyama vya siasa na wagombea wake vilitakiwa kuhakikisha kuwa mikutano ya kampeni inazingatia ratiba rasmi iiyoratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi au wasimamizi wa uchaguzi katika kutangaza sera zao.
Wajibu mwingine kwa vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo ulikuwa ni kuhakikisha kuwa vyama vyote vya siasa, wagombea, wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa wanachukua hatua za makusudi kwa mujibbu wa sheria za kuhakikisha kwamba uchaguzi unakuwa wa amani, huru na wa haki.
Picha juu zikionyesha miongoni mwa wananchi wa Kijiji cha Endule katika kata ya Endule Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha wakipata elimu ya mpiga kura kutoka kwa Maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Pia vyama vya siasa kujiepusha na vitendo vinavyoashiria vurugu, na vitisho, kujiepusha na aina yoyote ya ubaguzi katika misingi ya jinsia, ulemavu, ukabila, udini, maumbile au rangi.
Jambo lingine kwa vyama vya siasa ni kuhakikisha kuwa taarifa kuhusiana na uchaguzi na mchakato wake zinazotolewa ni sahihi na viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao wanazingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari katika kutekeleza shughuli za uchaguzi.
Kwa ujumla wananchi na vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Ngorongoro na udiwani katika kata tano walichangia kufanikisha chaguzi za kidemokrasia kwa kila kundi kutekeleza wajibu wao kikamilifu.
Mwandishi wa Makala hii ni Afisa Habari Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi anapatikana kwa simu 0656577945.