NA MWANDISHI DIRAMAKINI
JESHI la Polisi mkoani Pwani linashikilia watu 63 wakiwemo wanawake 10 kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na watatu wanashikiliwa kwa tuhuma za kuvunja kiwanda cha kukamua alizeti na kuiba mota 13 zenye thamani ya shilingi milioni 77.
Hayo yamesemwa leo Januari 28,2022 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Wankyo Nyigesa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha.
Nyigesa amesema kuwa, watuhumiwa hao watatu walivunja kiwanda hicho mali ya wajasiriamali Patrick Sungura (65) mkazi wa Kibamba na Fredrick Chacha (32).
Amesema kuwa, tukio hilo lilitokea Januari 22,mwaka huu majira ya saa 10:45 huko Misugusu Kata ya Misugusu wilaya ya Kibaha.
Watuhumiwa hao ni Nicolaus James (28) fundi mota mkazi wa Mbagala, Makoye Athuman (46) fundi magari mkazi wa Kimara Matosa na Machea Mzamilo (21) fundi mota mkazi wa Kimara.
Amesema, jeshi hilo limefanya misako mbalimbali kuanzia Januari 15 hadi 27 na kukamata jumla ya watuhumiwa 63 huku wanaume wakiwa 53 na wanawake 10.
Katika hatua nyingine jeshi hilo linamshikilia mtu ambaye jina lake limehifadhiwa akiwa na pikipiki ikikiwa na vipande 37 vya nyaya za copper ambazo zinadhaniwa ni kutoka katika miradi inayoendelea kujengwa mkoani Pwani.
Kamanda huyo amesema kuwa, tukio hilo lilitokea Januari 24, mwaka huu majira ya saa 11:30 huko Kijiji cha Mdaula Kata ya Ubena ambapo Polisi walikamata pikipiki yenye namba za usajili Mc 275 BEY aina ya SANLG.