NA MWANDISHI DIRAMAKINI
CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimemtangaza, Maimuna Said Kassim kuwa mgombea wa nafasi ya uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maimuna ametangazwa kwenda kuwania nafasi hiyo ambayo iliachwa wazi hivi karibuni na Spika wa Bunge hilo, Mheshimiwa Job Ndugai baada ya kujiuzulu.
Baada ya kutangazwa kuteuliwa na chama hicho leo Januari 21, 2022 jijini Dar es Salaam, Maimuna amekishukuru chama chake kwa kumuamini na kumpatia fursa ya kwenda kupambana kwenye nafasi hiyo ambayo pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemteua Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson.
"Kikubwa nitahakikisha Bunge letu linakuwa la kisasa na linaenda kutenda haki kuhakikisha linasimamia maslahi ya Watanzania,” amesema Maimuna.
Pia amesema, uwezo katika nafasi ya ungozi ni moja ya mambo yaliyomsukuma kuwania nafasi hiyo huku akielezea endapo atapata nafasi atahakikisha miimili yote ya Serikali kwa maana ya Serikali, Bunge na Mahakam inafanya kazi kwa ushirikiano.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa chama hicho, Hamad Rashid ameeleza kuwa Maimuna anatosha kushika nafasi hiyo baada ya kupikwa ndani ya chama hicho.