NA FRESHA KINASA
NAIBU Meya wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyasho, Mheshimiwa Haji Mtete amewaasa wazazi na walezi wa manispaa hiyo kushiriki kuchangia kwa hiari shughuli mbalimbali za maendeleo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo Januari 28, 2022 wakati akizungumza katika kikao cha wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari Nyasho iliyopo katika Manispaa ya Musoma kilicholenga kutafuta ufumbuzi wa kutatua changamoto uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi shuleni hapo.
Kutokana na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi shuleni hapo, Mheshimiwa Mtete amewaomba wazazi na walezi wa shule hiyo na anispaa kwa ujumla, kujitolea kwa hiari kuchangia maendeleo kwa manufaa yao ikiwemo fedha za kuajiri walimu wa muda wa masomo ya sayansi katika shule hiyo na maeneo mengine ndani ya Manispaa ya Musoma.
"Kama ambavyo walimu na Bodi ya Shule wamekuja na mapendekezo ya kuomba wazazi tuchangie fedha za kuajiri walimu wa sayansi, niwahimize kwa pamoja kupitia kikao hiki tukubaliane kushiriki kutoa michango kwa hiari ili tupate walimu wa sayansi ambao watatusaidia kufundisha masomo hayo. Tunawajibu wa kushirikiana na Serikali kuimarisha ufanisi wa elimu,"amesema Mheshimiwa Matete.
Mheshimiwa Mtete amesema kuwa, Serikali imetoa fedha Shingi Milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari katika eneo la Kigera itakayoitwa jina la Vedastus Mathayo Sekondari School ambapo kukamilika kwa shule hiyo kutapunguza idadi kubwa ya wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na Sekondari Nyasho, huku pia akiwahimiza wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya watoto wao kwa karibu kwa kushirikiana na walimu.
Aidha, Mheshimiwa Mtete amepata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyasho. Ambapo amewahimiza kusoma kwa bidii na kuzingatia nidhamu ya masomo sambamba na kuondoka na tabia ya utoro ili wafikie ndoto zao.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyasho, Charles Minene amesema kuwa, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,010, na walimu 18, ambapo shule hiyo ina mwalimu mmoja tu wa somo wa Hesabu, Biolojia 2, Kemia 2.
Katika kikao hicho, Wazazi na Walezi wa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyasho wamekubaliana kwa pamoja mbele ya viongozi wa kata hiyo na bodi ya Shule hiyo kila mmoja kuchangia elfu moja kila mmoja kuwezesha kufanya majaribio ya mara kwa mara, kuchangia fedha ya taaluma shilingi 15, 000 kila mmoja kwa mwaka ili kuwezesha kuajiri walimu wa masomo ya sayansi pamoja na shilingi 10,000 ya majengo.
Tags
Habari