NA NTEGHEJWA HOSSEAH-OR TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi Rais Tawala za Mikoa (OR-TAMISEMI),Mheshimiwa Innocent Bashungwa ameagiza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuendelea kuboresha njia za ukusanyaji mapato na kuwafichua wale wote wanaohusika na upotevu wa mapato hayo.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo Januari 26, 2022 wakati wa ziara aliyoifanya katika Ofisi za Wakala huyo pamoja na kutembelea miundombinu inayotoa huduma na ile inayoendelea kujengwa.
Amesema, nia ni kuona mapato hayo yanakusanywa ipasavyo na yanasaidia maendeleo ya mradi na taifa kwa ujumla.
Waziri Bashungwa ambaye awali alimpongeza Mkurugenzi wa DART, Dkt.Edwin Mhede kwa kuiwezesha taasisi hiyo kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa zaidi ya asilimia 120, amesema DART ina kila sababu ya kuhakikisha mapato inayokusanya yanaongezeka na kuvuka wastani huo.
"Niwapongeze kwa hatua hiyo lakini sasa muone haja ya kuvuka zaidi ya malengo hayo ikibidi muweke malengo ya juu zaidi ya yale mliyojiwekea awali jambo ambalo ninaamini mnaweza kulitekeleza," amesema Waziri Bashungwa.
Amesema, nia ya Serikali ni kuona miradi hiyo inazidi kuleta tija nchini na baadaye iweze kuunganisha upatikanaji wa huduma za usafiri katika maeneo mengi ya ndani na nje ya Dar es Salaam hatua itakaloleta ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, alimtaka Mkurugenzi wa Wakala huyo kuhakikisha wanaendelea kubuni mbinu mbalimbali za utoaji wa huduma sambamba na kuona namna ambavyo watashirikiana na sekta binafsi katika utoaji wa huduma ili kuongeza.
"Wekeni mlango wazi kwa kuzishirikisha sekta binafsi ili tuone kama zitaweza kuleta suluhu katika utoaji wa huduma, nchi nyingi Duniani zinafanya hivyo," amesisitiza Waziri Bashungwa.
Awali, Mkurugenzi wa DART, Dkt.Edwin Mhede amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, Wakala umepanga kitumia kiasi cha sh. Bilioni 7.02 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vyake ambapo kati ya fedha hizo sh. Bilioni 6.72 ni matumizi ya kawaida na sh.milioni 298 ni kwa ajili ya ukarabati wa kawaida wa miundombinu ya awamu ya kwanza. Amesema, katika fedha hizo,shilingi Bilioni 2.25 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu na shilingi Bilioni 4.76 ni mapato ya ndani, ambapo katika kipindi cha Julai hadi Desemba, Wakala umekusanya sh.Bilioni 4.5 sawa na asilimia 128.43 ya malengo ya kukusanya sh.Bilioni 3.5.
Aidha, amesema kwa sasa wanaendelea na ukamilishaji wa miundombinu kutoka Gerezani hadi Mbagala ambayo hadi Desemba,2021 ujenzi wake ulifikia asilimia 44.4 na matarajio ifikapo Machi, mwakani mradi uzinduliwe na kuanza kutoa huduma.
Katika hatua nyingine,Mtendaji huyo wa DARTamesema kwa sasa wapo katika mkakati wa kuongeza mabasi 95 ili kufikisha mabasi 305 yanayohitajika katika awamu ya kwanza ya utoaji wa huduma ya usafiri.