Waziri Masauni awapa pole wananchi,wafanyabiashara Soko la Mchikichini Karume kufuatia ajali ya moto

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mhandisi Hamad M.Y.Masauni ametuma salamu za pole kwa wananchi na wafanyabiashara wote wa Soko la Mchikichini Karume jijini Dar es Salaam kufuatia tukio la moto lililosababisha kuungua kwa soko hilo leo Januari 16, 2022.
Mheshimiwa Waziri ameyabainisha hayo leo Januari 16, 2022 kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

"Nichukue nafasi hii kutoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, wananchi na wafanyabiashara wote kufuatia tukio hili la moto ambalo limesababisha madhara makubwa ambapo mali za wafanyabiashara wa soko hilo zimeteketea kwa moto.

"Aidha, niwaombe sana wananchi na wafanyabiashara wote wa Soko la Mchikichini Karume kuwa watulivu katika kipindi hiki ili kutoa nafasi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzzi na kubaini chanzo cha moto huo.

"Nichukue nafasi hii kuliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha moto huo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wataalamu na kamati iliyoundwa na Serikali (Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala) kuchunguza chanzo cha moto huo ili kudhibiti matukio kama hayo yasijirudie siku zijazo,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Mhandisi Masauni kupitia taarifa hiyo.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Mhandisi Masauni amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa kufanikisha zoezi la kuudhibiti moto huo usiendelee kuleta madhara zaidi katika maeneo jirani na makazi ya watu yanayozunguka soko hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news