Waziri Mhagama aahidi kuimarisha utumishi wa umma kwa manufaa ya Taifa

NA JAMES K.MWANAMYOTO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema amedhamiria kuimarisha misingi ya utendaji kazi kwenye Utumishi wa Umma ili wananchi wanufaike na huduma zitolewazo na taasisi za umma nchini.
Sehemu ya Watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao Januari 11,2022 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo wa utendaji kazi anaouhitaji. 

Mhe. Jenista ametoa ahadi hiyo Januari 11,2022 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Idara za Uendelezaji Sera na Utawala wa Utumishi wa Umma.

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, ujio wake katika ofisi hiyo, sio wa kutengua torati, bali ni kuendeleza mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha Utumishi wa Umma.

“Ninaposema sijaja kutengua torati nina maana ya kuwa nimekuja kuongeza nguvu kiutendaji ili kumsaidia Mhe. Rais kuboresha Utumishi wa Umma na kuendeleza mazuri yaliyokwishafanyika na watangulizi wangu,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera na Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo wa utendaji kazi anaouhitaji. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi.

Waziri Jenista ameongeza kuwa, atatumia dhamana aliyopewa na Mhe. Rais kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma ili waweze kuwa na morali ya kutoa huduma bora kwa umma.

“Tunaona imani kubwa aliyo nayo Mhe. Rais kwa Watumishi wa Umma, hivyo nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kumsadia kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora, nitahakikisha Watumishi wa Umma wanafanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuendana na kauli mbiu yake ya KAZI IENDELEE.” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista amesema Mtumishi wa Umma ana mchango mkubwa wa kutimiza ndoto ya Mhe. Rais ya kuleta maendeleo kwa wananchi na ndio maana amekuwa akiwahimiza waajiri kuwapatia Watumishi wa Umma stahiki zao kwa wakati ili wawe na ari kiutendaji.
Sehemu ya Watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo wa utendaji kazi anaouhitaji. 

Mhe. Jenista ameanza vikao kazi na Watumishi wa Ofisi yake mara baada ya kuapishwa rasmi na Mhe. Rais kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news