NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako amewataka vijana waliopata mafunzo ya ukuzaji ujuzi katika vyuo mbalimbali nchini kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika na fursa za mikopo na vifaa kwa kujiendeleza kiuchumi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof.Joyce Ndalichako akiangalia shati lililoshonwa na mwanafunzi wa programu ya ukuzaji ujuzi inayoratibuwa na ofisi yake, alipowatembelea kujionea maendeleo yao katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) kilichopo Kasulu Mkoani Kigoma Januari 29, 2022. (Picha na OWM).
Ametoa wito huo leo Januari 29, 2022 mkoani Kigoma mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ambapo vijana wa programu hiyo wanapata mafunzo kwa vitendo na kusisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuona elimu hiyo inawanufaisha vijana.
"Mheshimiwa Rais tayari ametupatia fedha kwa ajili ya kununua vifaa ambavyo tutavigawa kwa baadhi yenu, na kwenye ofisi ya Waziri Mkuu kuna mfuko kwa ajili ya kuwawezesha vijana hivyo jiungeni kwenye vikundi ili mnufaike na fursa hizo niwambie tu mama hawezi kuwaacha vijana wake,”amesema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Prof.Joyce Ndalichako akiwa katika ziara yake ya kikazi kukagua maendeleo ya programu ya ukuzaji ujuzi inayoratibiwa na ofisi yake katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Isack Mwakisu kushoto kwake ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kasulu, Bw. Mbwelwa Chidebwe. (Picha na OWM).
Aidha, amesema progamu hiyo ni endelevu ambapo awamu ya kwanza imepangwa kugharimu shilingi za Kitanzania bilioni tisa kwa matarajio ya kuwanufaisha zaidi ya vijana 14,000 kote nchini.
“Kwa niaba ya vijana hawa nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake, kwa kweli amelitengeneza jeshi kubwa ambalo ninaamini kwa ujuzi huu tutapunguza sana utegemezi,”amesisitiza prof. Ndalichako.
Ameongezea kuwa, kundi la vijana ni muhimu katika jamii kwa kutambua mchango wake hivyo limepewa kipaumbele katika kuwajengea uwezo ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe Prof.Joyce Ndalichako akiangalia shati lililoshonwa na mmoja wa wanufaika wa programu ya ukuzaji ujuzi inayoratibiwa na ofisi yake, Bi. Lucy Isaya, alipowatembelea kuona naendeleo yao katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) kilichopo Kasulu mkoani Kigoma.
Alitumia fursa hivyo kuwaasa baadhi ya mafundi ambao wamepata ujuzi katika mfumo usiyo rasmi kutumia fursa ya kurasimisha ujuzi wao ili waweze kutambulika na kunufaika na fursa za kiuchumi zinazojitokeza nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Prof.Joyce Ndalichako akiangalia moja ya dawati lililotengenezwa na wanafunzi wa Programu ya Ukuzaji Ujuzi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu, wakati wa ziara yake kujionea maendeleo yao.
Baadhi ya vijana walionufaika na mafunzo hayo akiwemo, Aman Ahamad Rutta anayesomea masomo ya ufundi bomba na Mariam Hussein Ramadhani anayesomea ufundi umeme wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafunzo hayo na kuomba kuendelea kuwafikia kwa wingi ili kuendelea kupunguza changamoto za ajira na kuwa na vijana wenye uwezo wa kujikimu na kujiletea maendeleo yao.
“Kwa kweli Serikali imekuja kutufungua macho sisi ambao tulikuwa tumebaki kama kundi la mwisho mtaani, maana tumejifunza vizuri yaani ninaamini baada ya hapa mimi binafsi nitakuwa na sehemu nzuri ya kuanzia,”amesema Rutta.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Prof.Joyce Ndalichako akikagua moja ya dawati lililotengenezwa na wanafunzi wa Programu ya Ukuzaji Ujuzi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu ambapo kwa sasa wanaendelea na mafunzo kwa vitendo chuoni hapo, wakati wa ziara yake ya kujionea maendeleo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mheshimiwa Kanali Isack Mwakisu amewataka vijana hao kuzingatia mafunzo wanayoyapata ili yawasaidie kunufaika na fursa za ajira kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali wilayani humo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Prof.Joyce Ndalichako akizungumza na wanufaika wa Programu ya Ukuzaji Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi yake, alipowatembelea katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu Kigoma kujionea na kukagua maendeleo yao.
Naye Mkuu wa Chuo cha FDC Kasulu,Mhandisi Ramadhan Simba amesema katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo wamepokea vijana 257 katika fani mbalimbali ikiwemo ufundi wa magari, uashi, useremara na ushonaji.
AWALI
Katika ziara hiyo Waziri Prof,Joyce Ndalichako ametembelea vijana hao katika maeneo mbalimbali wanayopatiwa mafunzo kwa vitendo ikiwemo Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kigoma, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kasulu.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu akizungumza na wanafunzi wa Programu ya Ukuzaji Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi Waziri Mkuu wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Prof.Joyce Ndalichako alipowatembelea katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu Kigoma.
Programu hiyo ya kukuza ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu inatokana na utafiti wa Nguvu Kazi ya Taifa wa mwaka 2014 uliobaini kuwa asilimia kubwa ya watanzania wana ujuzi kwa kiwango cha chini.