NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel wamewaongoza maelfu ya waombolezaji kuaga miili ya waandishi wa habari watano waliopoteza maisha kwenye ajali ya gari.
Ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 14 na majeruhi wawili,ilitokea Januari 11, 2022 majira ya saa 12:30 katika Kijiji cha Shimanilwe, Kata ya Kabita wilayani Busega mkoani Simiyu ikihusisha gari namba SKT 8140 na gari aina ya Toyota Hiace lenye namba T 281 DER mali ya Lunyenya Kaswalala.
Waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni Ofisa Habari Mkoa wa Mwanza, Abel Ngapemba, Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Steven Msengi, Johari Shani wa Uhuru Digital,Husna Mlanzi wa ITV, Anthony Chuwa wa Daily News Digital pamoja na dereva wa gari hilo Paul Silanga.
Pia waandishi wawili Tunu Herman na Ivvany Charles wa Icon TV walijeruhiwa na wamelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando wakiwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) ambapo wanaendelea vizuri.
Miili ya marehemu hao imeagwa leo Januari 12, 2022 kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza majira ya saa 6:30 hadi saa 8:25 na kuibua vilio na simanzi kutoka kwa ndugu,jamaa na waombolezaji ambapo mwili wa Husna Mlanzi ulizikwa katika makaburi ya Kirumba.
Marehemu wengine miili yao imesafirishwa ambayo ni ya Abel Ngapemba na Steven Msengi (Dar es Salaam), Johari Shani (Arusha),Anthony Chuwa (Moshi) na Paul Silanga (Tabora) .
Akitoa salamu za pole kwa wafiwa na waombolezaji,Nape amewaagiza waajiri wote waliokuwa wakidaiwa mishahara na marehemu hao wahakikishe wanawalipa stahiki zao ndani ya siku saba kuanzia leo na watakumbukwa kwa kazi na uzalendo wao.
“Ni siku ngumu kidogo kwangu kama alivyosema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,ni shughuli yangu ya kwanza na ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari Kanda ya Ziwa,Mkoa wa Mwanza lakini kubwa pia kwa nchi yetu,”amesema Waziri Nape.
Amesema, kutokana na msiba huo mkubwa, amekuja kuwasindikiza mashujaa hao waliofia kazini wakitekeleza majukumu yao,pia wenzao wanafanya kazi hapa kwa huzuni nao wamekuja kuwasindikiza.
Nape amesema, Sheria ya Wanahabari na Haki zao iliundwa wakati akiwa Waziri wa Habari wakati huo,lengo lilikuwa kuifanya tasnia hiyo kuwa taaluma inayoheshimika na haki zao.
Amesema kuwa, amerudi nyumbani kusimamia sheria hiyo ya Huduma na Haki ya Habari na kuwahakikishia wana habari kuwa haki zao zitalindwa.
“Penye mapungufu yatarekebishwa ili kukidhi mahitaji na matakwa kwa kutengeneza mazingira ya kuwawezesha waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru,viwango na weledi,” amesema Nape.
Waziri huyo wa habari ametumia fursa hiyo kuwaagiza waajiri wote waliokuwa wakidaiwa mishahara na marehemu hao kuanzia leo wahakikishe wanawalipa hata kama ni kukopa wakakope.
“Natoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa na marehemu mishahara,kakope,kauze kama mwanahabari ambaye ni marehemu anakudai kakope ulimpe stahiki yake, kutolipa haki za watu (waandishi wa habari) ni kuvunja sheria,umemwajiri mtu mlipe yawezekana wanapitia hali ngumu,”amesema.
Ajali
Kuhusu matukio mengi ya ajali kwenye misafara ya viongozi kuwaandama na kuwagusa wanahabari, Waziri Nape amesema viongozi wa juu wameliagiza jeshi la polisi kupeleka taarifa za ajali hizo.
Ameeleza kuwa, lengo la kuhitaji taarifa ya ajali hizo itawezesha kuchukua hatua y kuweka itifaki ya kuwalinda wana habari ingawa zipo sababu nyingi.
“Serikali inataka kujiridhisha ni kwa nini ajali hizo zinawagusa wana habari na haya nitayasimamia na kuhakikisha yanatekelezwa,”amesema Nape.
Amesema, wizara inatoa pole kwa waandishi wa Mwanza, na kwamba marehemu hao watakumbukwa kwa kazi zao na hasiti kuwaita mashujaa kutokana na kufia kwenye uwanja wa mapambano wakipigania taifa lao ambapo alionyesha kuguswa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa upendo aliounyesha kwa wana habari.
Aidha, akitoa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan,Nape amesema kuwa ameguswa sana na msiba huo wa wana habari watano na anatoa pole kwa wafiwa,waombolezaji na wana habari wote.
Amesema kwamba walikuwa vijana wadogo na wazazi wao waliwekeza kwao na baada ya kuanza uwekezaji huo maisha yao yamekoma ambapo pia Rais Samia aliwaombea majeruhi wa ajali hiyo wapone,wainuke na kurudi kwenye majukumu yao.
Kwa mujibu wa Nape viongozi waliotoa salamu za pole ni Mkamu wa Rais, Dkt. Philipo Mpango na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Mwinyi,ambaye alimuomba Mwenyezi Mungu azipokee roho za marehemu hao na kuwaponya majeruhi, pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri wa wizara mbalimbali za serikali.
UTPC
Awali Mkurugenzi wa UTPC, Abubakar Karsan na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko walisema uwanja wa kufanyia kazi si mzuri kutokana na sheria zinazosimia tasnia ya habari na kuomba kuhakikisha maslahi ya wanahabari yanalipwa na kuhakikishiwa usalama wao.
“Haki na usalama wa wana habari ni muhimu,wenzetu wamelala pale,baadhi hawajalipwa stahiki zao hata wanaofanya kazi hapa,hatulipwi sababu ya waajiri hawana moyo wa kutulipa kwa kisingizio kuwa biashara imeharibika wakati tunakutana nao kwenye baa hizo za bia zinatoka wapi.
“Uwanja wa kufanyia kazi si mzuri sababu ya sheria kandamizi, Mkuu wa Mkoa (RC) Mhandisi Gabriel,amefanya huruma ya kutusaidia kwenye msiba huu na suala la usalama wa waandishi na maslahi yao hili liko kwako na yawezekana Mungu kakurudisha ukamilishe kazi hiyo,”amesema.
Mkurugenzi huyo wa UTPC ametumi fursa hiyo kumweleza Nape kuwa waajiri ambao marehemu baadhi wanawadai kabla hawajazikwa, Mwenyezi Mungu awafumbue vichwa vyao wawalipe.
Soko yeye amesema marehemu hao ni majemedari wa vita waliofia kwenye uwanja wa vita huku akirejea katiba ya nchi kuhusu haki ya kupata na kutafuta habari na kumuomba Nape aangalie namna ya kulegeza baadhi ya vifungu vya sheria kuhusu viwango vya elimu kwa wanahabari ikiwezekana wajiendeleze wakiwa kazini, lakini pia kuboresha maslahi yao.
RC
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema hana nguvu ya kuzungumza kutokana na msiba huo mkubwa ulioligusa taifa na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya marehemu hao kwani maisha yana mwanzo na mwisho na kamwe wana habari hao hawatasahaulika.
Amesema, heshima ya Mwanza na maendeleo yake yametokana na jeshi la waandishi wa habari mahiri,makini na wenye weledi wanaoipenda kazi yao na hilo amelishuhudia kwa miezi sita baada ya kuhamia Mwanza.
“Bila waandishi wa habari kazi zetu ni sifuri (hazitambuliki),marehemu hawa waliipenda kazi yao,walibeba na kutembea na kalamu zao,walitumia sauti zao kuhoji na kuziweka vizuri, hawakulalamika wala kunung’unika licha ya shida walizo nazo,”amesema Mhandisi Gabriel.
Amesema liko tumaini kwa waliojiandaa kumcha Mungu, hivyo awaondolee adhabu awape nafasi waliomcha kwa kushika imani na ipo siku tutakuwa nao tukitambua zawadi ya uhai tuliyopewa na kuwaomba waombolezaji na wafiwa wasikate tama kwani Mungu ametupa matumaini ya kuubeba msiba huo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema habari mbaya huletwa na wana habari na kila kazi ina mtego, hivyo ujio wa Waziri wa Habari kwenye msiba huo si bahati mbaya bali Mungu ana makusudi yake na kuwataka watumishi wa umma kutenda haki kwa watu wote.
“Watumishi wa umma tendeni haki, msidhulumu watu na heri kuiendea nyumba yenye msiba kuliko yenye sherehe, hivyo wote tumche Mungu tuitwe watakatifu.Hatutawasahau kamwe wana habari hao maisha yao yana mwanzo na mwisho ambapo jana ilimpendeza Mungu ikawa mwisho wa maisha yao,”amesema.
Dua
Katika kuagwa kwa miili ya marehemu hao kulitanguliwa na dua la sala kutoka kwa Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Sheikhe Hassan Kabeke,Mchungaji Charles Mkumbo wa TAG na Padri George Nzuri wa Kanisa Katoliki kutokana na marehemu kuwa imani za madhehebu matatu tofauti.
Sheikhe Kabeke akitoa pole kwa wafiwa, ndugu, jamaa na waombolezaji pamoja na serikali, alisema marehemu hao walifanya kazi ya kuitumikia jamii kwa moyo wa unyenyekevu.
“Lakini pia Mhandisi Gabriel,naomba Mungu amtie nguvu n ujasiri kwa msiba huu, pia Rais Samia katika kipindi hiki kigumu na katika kuliongoza taifa na kuwatumikia Watanzania,”amesema.
Kwa upande wake Padri Nzungu alisema waandishi wa habari wakiwemo marehemu waliofariki kwa ajali wanafanya kazi ya uaminifu na utakatifu ya kuwatetea haki za watu na kupatanisha licha ya mitikisiko wanayoipata.
Amesema hata Mungu aliwatumia watu mbalimbali kufikisha ujumbe kwa jamii, kazi ambayo pia inafanywa na wana habari nchini ya kuhakikisha jamii ifahamu mambo mengi yakiwemo ya maendeleo.
“Wana habari wanafanya kazi ya utakatifu,ni watu wa kupatanisha watu,wanaudhiwa kwa ajili ya haki, wanapata mitikisiko lakini Mungu anasema ufalme wa Mungu ni wao.
“Injili ya Mathayo inasema heri wenye huzuni watafarijiwa, heri wenye njaa maana watashibishwa,wenye moyo safi watamwona Mungu na watakaoudhiwa kwa ajili ya haki ufalme wa mbinguni ni wao,” amesema Padri Nzungu.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Julius Peter amesema walipokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko makubwa kutokana na kupoteza wanahabari hao wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi.
Amesema kazi ya Mungu haina makosa, ingawa tuliwapenda na tulitamani kuendelea kuwa nao lakini imempendeza Mungu kawapenda zaidi hivyo familia zao, ndugu,jamaa na marafiki waendelee kuwa watulivu na wavumilivu kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Tags
Habari